Siri ya kalameni Krismasi yafichuka

Na GRACE KARANJA

Imepakiwa - Saturday, January 16  2016 at  14:27

Kwa Muhtasari

Jombi wa mji huu wa Thika alijipata pabaya baada ya mkewe kugundua kuwa mwisho wa mwaka jana wakati wa likizo ya Krisimasi, alikuwa kwa mpango wa kando.

 

THIKA MJINI

JOMBI wa mji huu wa Thika alijipata pabaya baada ya mkewe kugundua kuwa mwisho wa mwaka jana wakati wa likizo ya Krisimasi, alikuwa kwa mpango wa kando.

Penyenye zilizotufikia zasema kuwa buda alimwambia mkewe kwamba alisafiri kwenda kuwaona wazazi mashambani kwa sababu alikuwa hajawaona kwa muda mrefu.

“Jamaa alikuwa amekaa miaka mitatu bila kuwatembelea wazazi na mkewe aliamini alikuwa huko,” mdokezi alisema.

Inasemekana kuwa, siku kadhaa kabla ya sikukuu jamaa alikuwa na furaha sana na kila wakati alitaja safari hiyo.

“Naona siku zinakawia sana na ninatamani kuondoka kwenda nyumbani kuwaona wazazi wangu,” kila mara jamaa alimwambia mkewe.

Siku ya kisanga juzi, jamaa alikuwa nje ya nyumba simu yake ilipopigwa na mkewe akaipokea.

“Mbona siku nyingi hujanipigia simu na vile ulinifurahisha likizo yote au umemrudia mkeo? Unaweza kunisahau haraka hivyo?” demu aliropokwa akidhani alikuwa akizungumza na jamaa.

Mama apigwa na butwaa

Mama huyo hakuamini masikio yake na alimpa mumewe simu.

“Haya ongea na huyu uliyemfurahisha wakati wa Krismasi, sikujua kwamba wewe unaweza kunifanyia jambo kama hilo. Ulinindanganya ulienda kuwaona wazazi wako ili ukaburudishe vimada. Ulidhani mimi ni mjinga kwa sababu sikutaka kujua kama ulifika nyumbani au la. Usijali leo nimekushika,” mama alimfokea jamaa.

Juhudi za jamaa kutaka kuzungumza na mpango wake wa kando hazikufua dafu mkewe alimnyang’anya simu na kumwonya kipusa dhidi ya kumchezea mumewe.

“Hata kama mume wangu alikuja kwako usifikiri umepata nafasi ya kumchukua. Keep off my husband,” mama alichemka.

Haikufahamika ikiwa mama alisamehe jamaa baada ya kugundua tabia yake.

Dondoo za Hapa na Pale ni visa vinavyojiri kila siku sehemu tofauti nchini na kimataifa. Tuma habari kwa:dondoo@ke.nationmedia.com/ taifa@ke.nationmedia.com au swahilihub@ke.nationmedia.com