Walishana bakora kukosa kuelewena kuhusu ukali wa pombe

Na AMIMO ZACCHAEUS

Imepakiwa - Wednesday, May 18  2016 at  09:59

Kwa Muhtasari

Kulizuka hali ya taharuki katika boma la mama pima mmoja wa hapa Wire, Oyugis walevi walipoanza kulishana bakora baada kukosa kuelewana kuhusu ukali wa pombe waliokuwa wakiteremsha.

 

WIRE, Oyugis

KULIZUKA hali ya taharuki katika boma la mama pima mmoja wa hapa Wire, Oyugis walevi walipoanza kulishana bakora baada kukosa kuelewana kuhusu ukali wa pombe waliokuwa wakiteremsha.

Kulingana na mdokezi, walevi hao walikuwa wakiburudika kwa mama pima pale mmoja wao alipoanza mjadala akidai pombe hiyo haikuwa kali kama ya siku iliyotangulia.

“Leo ni kama imeongezwa maji ama nini wenzangu? Hii sio kali kama ile ya jana! Nateremsha na bado sipati stimu,” alisema jamaa moja.

Kilichomshangaza ni kwamba, hakuna aliyemjibu, badala yake, wenzake  waliendelea kuchapa dozi wakiagiza kinywaji zaidi.

Inasemekana kuwa jamaa aliyelalamika, alichukua bakuli iliyokuwa na pombe na kuiangusha akisema pombe hiyo haikuwa na ladha.

“Nimewaambia pombe si kali na ni kama hamsikii. Kwani midomo yenu imewekwa nini kiasi kwamba hamuwezi kugundua pombe imeongezwa maji,” jamaa alilalamika huku akimwita mama pima.

Mama pima atolewa kijasho kwa maswali

Mama pima alipofika jamaa alimkabili kwa maswali magumu.

“Kwani siku hizi unaongeza pombe maji kwa nini? Unajua nakulipa kwa huduma yako na hivyo basi ningependa nipate dhamana ya pesa yangu. Yaani nataka ile inawasha koo yangu,” alisema mzee huyo.

Kwa hasira, mmoja wa walevi wengine walimwambia aachane na ujinga na kuondoka badala ya kusumbua watu.

“Unajua wewe una ujinga mwingi sana ukilewa.Unasemaje pombe si kali ilhali umelewa.Kama haujalewa si uamke uende kwako nyumbani?” akafoka jombi mmoja.

Wawili hao walianza kubishana na haikuchukua muda kabla ya mmoja kumwangushia mwenzake bakora mgongoni.

“Jinga wewe! Chukua hiyo. Nyinyi ndio mnaharibu biashara hapa,” alimfoka huku akimwambia mama pima amrudishie jamaa pesa zake. Mama huyo alilazimika kuwafurusha walevi wote na kufunga mlango akiogopa ghasia.