Wamrukia ndugu yao kufuatia kifo cha baba

Na BENSON MATHEKA

Imepakiwa - Wednesday, January 13  2016 at  10:14

Kwa Muhtasari

Kizaazaa kilitokea hapa Miwani, Machakos jombi alipotandikwa na ndugu zake wakidai alifahamu kilichosababisha kifo cha baba yao.

 

MIWANI, Machakos

KIZAAZAA kilitokea hapa Miwani, Machakos jombi alipotandikwa na ndugu zake wakidai alifahamu kilichosababisha kifo cha baba yao.

Inasemekana kuwa familia ya marehemu, majirani na marafiki walifika mochari iliyoko eneo hili kuchukua mwili kwenda kuuzika.

Hata hivyo, walipomwona ndugu yao walipandwa na hasira na kumtaka kuondoka.

“Unafanya nini hapa? Na unajua kilichomuua baba yetu. Ondoka mara moja, hatutaki kukuona,” ndugu zake walimwambia.

Jamaa aliyekuwa ameegesha gari la kifahari hatua chache kutoka mochari alikaidi agizo hilo na kusema alikuwa na haki ya kuhudhuria mazishi ya baba yake.

“Ni baba yangu aliyenizaa na niko hapa kumpa mkono wa buriani. Hamna haki ya kunizuia,” akasema.

Ndugu wapandwa na hamaki

Lakini matamshi yake yalionekana kuwachemsha zaidi ndugu zake waliomlaumu kwa kukosa kushiriki mipango ya mazishi.

“Sasa ndio amekuwa baba yako eh? Ulikuwa wapi tulipokuwa tukiandaa mazishi? Wacha hayo, hukumtembelea alipokuwa akiugua, tena ulisema wakati wake wa kufa ulikuwa umefika kumaanisha ulijua kilichomuua. Toka hapa na wewe sio ndugu yetu na usikaribie tulipo.”

Mambo yaliharibika alipojaribu kusongea gari la kubeba maiti lilipokuwa ndugu zake walipomuinua juu na kumtandika.

“Shetani ya mtu wewe, hautaendelea kusumbua familia yetu,” walimfokea.

Dondoo za Hapa na Pale ni visa vinavyojiri kila siku sehemu tofauti nchini na kimataifa. Tuma habari kwa:dondoo@ke.nationmedia.com/ taifa@ke.nationmedia.com au swahilihub@ke.nationmedia.com