FATAKI: Ni makosa kupima uzuri wa binti kwa msingi wa rangi ya ngozi na makalio yake

Na PAULINE ONGAJI

Imepakiwa - Thursday, November 30  2017 at  14:52

Kwa Muhtasari

Mojawapo ya mambo ambayo yaligonga vichwa vya habari juma lililopita ni uzinduzi wa kibao Melanin chao Sauti Sol kwa ushirikiano na msanii Patoranking kutoka Nigeria.

 

Kibao hicho kinazungumzia fahari ya kuwa na ngozi nyeusi huku wasanii hawa wakilimbikizia sifa mabinti wa Kiafrika weusi.

Bila shaka lazima upongeze wanamuziki hawa kwa kwenda kinyume na ada mara nyingi ambapo tumesikia wasanii wa asili ya Kiafrika wakiwasifu wanawake wenye ngozi nyeupe au ‘yellow yellow’.

Ukisikia kibao hiki redioni una kila sababu ya kufurahia hasa ikiwa wewe ni mwanamke wa Kiafrika, kwani angaa unapata kusikia ujumbe tofauti kabisa kumhusu mwanamke mwenye ngozi nyeusi.

Lakini tatizo linawadia unapopata fursa ya kutazama video. Picha za uchi na masuala ya ngono ndizo zinatawala hapa, ambazo kulingana nami zinaonekana kushusha hadhi ya mwanamke mweusi kwa kuhusisha urembo wake na utupu au uzinzi.

Ni sawa na hizo video za baadhi ya nyimbo za wasanii kutoka Jamaica ambazo zimekuwa zikitawala kwenye baadhi ya matatu nchini na ambazo kwa kawaida huonyesha wanawake weusi wakinengua wakiwa nusu uchi.

Tazama video za nyimbo za repa, ujumbe ni huo huo wa wanawake kunengua wakiwa nusu uchi huku akiwa amevalia hizo nywele za kubandika na kujipodoa kupindukia kana kwamba hana ubongo wa kumwezesha kuwa na ujuzi mwingine.

Tangu enzi za utumwa mwanamke mweusi amekuwa akichukuliwa kama chombo cha ngono. Licha ya hatua ambayo imepigwa na wanawake wa asili hii katika taaluma mbalimbali, bado uzuri wetu unazidi kupimwa kwa misingi ya ngozi, nywele na makalio makubwa.

Wanawake weusi wameafikia mengi katika taaluma za kimasomo, elimu, udaktari, uandishi na kadhalika na kuwapima kwa misingi ya makalio, rangi ya lami na nywele ni sawa na matusi.

Bila shaka tunatambua nia njema ya Sauti Sol na Patoranking katika harakati za kumuinua mwanamke wa Kiafrika ambaye amepambana tangu jadi kudhibitisha urembo wake katika ulimwengu ambao uzuri wa mwanamke unapimwa kwa kutumia mizani ya mwanamke mzungu, lakini ukweli ni kwamba wasanii hawa walipotoka na kushusha zaidi hadhi ya mwanamke wa Kiafrika.

Nakiri kuwa huenda kibao hiki kitachangia pakubwa katika kuwafanya wanawake wa ngozi nyeusi kujikubali na kujipenda, na hivyo kuzuia visa vya wanawake kuchubua ngozi zao, ila kuna wanawake ambao wana hiyo ngozi nyeusi, ni warembo, na hata wana hayo makalio makubwa lakini wameshamiri katika taaluma mbalimbali.