Kula ushibe lakini tarajia kishindo pindi mnapokosana

Imepakiwa Wednesday August 5 2015 | Na CHARLES OBENE

Kwa Muhtasari:

Safari ya huba inavutia kwa wapendanao lakini linapozuka jambo ndipo utajua mwanamume wa leo kama dunia rangi rangile hasa pale dunia nzima itashiba hadithi jinsi ulivyo degi bovu tena kinu kisicho ukingo unaokaba mchi.

KILA mwanamke ameumbwa kwa namna ya kipekee na kutunukiwa vipawa visivyofanana na mwingine. Ole nyinyi kina yakhe mnaosumbukia tu miili inayozinga! Hivyo basi hakuna mke asiyependeka wala hakuna asiyependeza. Hutegemea hasa ukomavu wa mwanamume hali kadhalika lengo la uhusiano.

Sijui vipi kumjuza mwanamume wa leo! Mwanamke anastahili sio tu upendo wa dhati, bali pia imani thabiti kama ithibati ya upendo. Hakuna cha ziada anachothamini mke zaidi ya uthabiti! Yaani hakikisho tosha ya mstakabali mwema maishani. Hapa nazungumzia wanawake wa hadhi wanaojua maana na thamani ya kuvalia taji la mke! Aha! Kwenye harusi ya mamba wamo mijusi!

Lakini imani haiji kwa kuvizia wala haimo katika husiano za kisasa. Kwa nini? Kila mmoja yumo hayumo katika uhusiano. Isitoshe, kila mmoja analenga kujinufaisha binafsi sisemi kufaidi kwa jasho la mwingine, tena haraka iwezekanavyo. Utapeli huu ndio kizungumkuti kinachozungusha na kuyumbisha maisha ya wanawake kwa wanaume wa leo.

 

Dhana potovu

Kosa kubwa linalohujumu maisha ya wachumba na wanandoa ni dhana potovu kwamba wapo wanawake bora kuliko wengine. Kibaya chako chema cha mwenzio! Simameni kidete enyi mnaodedea maana mwilini mwa mke hakuna dango eti kila mmoja atalenga shabaha na kwenda zake! Na ikiwa utakwenda kwa raha zako, jamani mwenzio usimfedhehi kwa vijembe na kutangaza ulimbukeni wake! Ya siri ni siri!

Upendo unaposhamiri, wanaume wa leo hawachelei kudhihirisha furaha na bashasha ishara kwamba wapo ndipo, tena walipodhamiria kuwepo! Faraghani na hata hadharani hakuna linalofichika. Si mahaba vijiani, si kushikana vitangani si mwana kuliwa na kumla mwenzake!

Lakini subiri lizuke jambo ndipo utajua mwanamume wa leo kama dunia rangi rangile. Dunia nzima itashiba hadithi jinsi ulivyo degi bovu tena kinu kisicho ukingo unaokaba mchi! Na hilo ndilo tatizo kubwa la mwanamume! Mwingi wa vitimbi na sarakasi za mapenzi. Hadaa zote zinalenga tu kuliambua tunda na mwana kumwachia zigo la akili zito.

Tahadharini nyie wepesi kushawishika na hadaa za wanaume. Leo atakuimbia nyimbo za kukuloesha pangoni lakini kesho hutadiriki kutoka pangoni kwa fedheha alizokupa! Hapo ndipo utasikia, “alikuwa demu wangu yule!” Ole nyinyi mnaodhani hiyo ni sifa. Demu ni nguo mbovu na kuukuu iliyochanikachanika! Amekwisha kukuchana, kweli!

Majina ya kimahaba

Mwanamume wa leo atakusifu kwa majina ya kimahaba maana keshaona njia ya kutimiza haja sisemi kukupapasa paja. Atakufaidi kwa lishe na mavazi angalau kukuondolea shaka hasa nyinyi vicheche mnaopenda vibanzi kwa kuku choma! Kula na ushibe lakini tarajia kishindo punde tu mtakapokosana! Dunia nzima itajua jinsi hushibi hushibishwi!

Jamani kina dada, mwanamume sio mumeo na hathamirii kuwa. Hujui kwao naye hana haja kujua kwenu. Mmekutana kisadfa tu. Haja gani wewe kujipendekeza kama dawati lisilochagua makalio? Mume kama huyo ana haki gani kukutambalia na kukutandaza kama bustani?

Haya ndio mahaba yanayowapa wanaume nguvu kuwatenda kinyama kisha kuwakejeli kwenye mitandao! Anazo sababu zote kukuita kicheche au changudoa mbele ya umma maana keshakudona bila gharama.

Ole nyinyi mnaoshughulikia sana sura na ngozi kuliko akili na ubongo! Mwili na umbo lako litamzingua tu mwanamume kwa kuwa anasubiri sega kukoleza uki.  Yote hayo ni kwa muda tu dada! Ndio kwanza mkoko kualika maua.

Subiri kuchanwa na kuchambuliwa kama mhogo! Subiri vijembe na kebehi zitakazokutoa chozi!  Subiri kutangazwa na kusemwa kwa waja na wahujaji! Mwanamume dawa, tena sumu!

 

Share Bookmark Print

Rating