Mume kamili ni dafina ya hekima na ustaarabu

Imepakiwa Wednesday August 20 2014 | Na CHARLES OBENE

Kwa Muhtasari:

Mwenzio atakuvumilia hadi lini ilhali wamchanja kwa maneno na mabezo kama ukuni?  Kama ni lazima mume kusema, basi toa mwongozo mara moja na waachie wenye meno kutafuna mabuyu. Kelele kila siku nyumbani kwani wewe chiriku au kasuku?

MZAHA mzaha wa mwanaume wa leo hutunga usaha. Jamani sisi watu wazima, mbona kuishi kama vijitoto visivyojua maana ya maisha? Tuzingatie mipaka ya mzaha tusije juta kuachwa tumezubaa kwenye mataa kwa sababu ya ulimbukeni! Kiboko cha adhabu kwa mume kichwa pumba ni kumwacha na kilio cha mbwa mdomo juu!

Nasema hivi kwa kuwa wanaume wa leo wamezidisha mzaha na michezo hadi mambo kuwaharibikia na maisha kukorogeka! Mwanamume umekomaa; mtu mzima mwenye familia lakini ungali katika vikundi vya vijana wanaobaleghe ukishiriki tabia za kudunisha mno.

Hukosi barabarani mkifukuzana na mabanati wa kidato cha pili au kwenye vikundi vya magenge wanaosuta wapita njia! Mume wa mtu, ati! Jamani kuhesabu magari au kukagua waliobeba na waliobebeshwa kamwe haiwezi kumpa mtu riziki au kumwondolea ufukara!

Isitoshe, wewe wa kwanza kusonya na kumfokea mke punde tu unapokosa chakula nyumbani! Mume we! Hutaki kufanya kazi na huna pesa kukidhikia familia, wataka kula vya nani? Familia hula jasho la mume. Hakuna haja kumwachia mke mzigo wa kuwalea watoto na kukulea wewe mtu mzima!

Badala ya kwenda viwandani wanakokwenda wanaume wenye misuli kupanga foleni kwa ajili ya riziki angalau kuvumbua kidogo cha kukidhi mahitaji ya watoto,  mume yuko vijijini akizurura mitaa kama mbwa koko. Mitaani watafuta nini? Wenzako mwakutana wakichuuza njugu na mahamri, wewe huoni haya kubeba na kutembeza mwili bure? Mume mzigo ni dhiki maishani.

Kama lazima kugombana nyumbani, angalau mara moja na sababu iwe ya haja! Lakini mume wa leo ana ulimi mwepesi kama nyaya za gita! Guswa kidogo tu, sauti kama mwehu! Hajui kutulia, kutathmini na kutafakari kwa kina juu ya lolote.  Jambo linalopasa kutatuliwa taratibu kwa mazungumzo mume, atalijengea hoja na nyumbani hakukaliki! Hizo tabia za ujanani sizo za mume kamili.

Mwongozo

 Mwenzio atakuvumilia hadi lini ilhali wamchanja kwa maneno na mabezo kama ukuni?  Kama ni lazima mume kusema, basi toa mwongozo mara moja na waachie wenye meno kutafuna mabuyu. Kelele kila siku nyumbani kwani wewe chiriku au kasuku?

Napenda sana mume msikivu hasa akiwa mbele ya watu. Yaani mwenye kupima uzito wa maneno anayotoa au mwenye kutafakari hatari ya maneno anayotamka. Mwanamume kamili ni dafina ya hekima na ustaarabu! Akizungumza moja tu, hukuacha na la maana! Si kuboboja kama kwamba kapagawa!

Hawa wa leo ni kama samaki; raha yao kudakia kila kitu kinachotupwa kindimbwini.  Mwanamume amesikia jambo lisilomhusu likisemwa lakini atalidakia na kuligeuza lake! Mume mjuvi wa kujifanya kujua kila jambo ni kero. Na huyu akiwa ndani ya nyumba humfanya mke kujichukia! Ya jikoni anayajua yote. Ya hamamuni anayajua juu chini. Ya chumbani, yeyé gwiji! Na sio kujua tu, anataka kukuonyesha anayajua yote! Sasa kazi ya mke ipi?

Heshima ya mume kamili ni kutambua hadhi na kumpa mwenzake nafasi yake ndani ya nyumba. Hizi ndoa za mwajificho tena za matani na mzaha hazifai kitu! Mwenzio kusononeka ni wewe kutaka.

mwanamume@yahoo.com

Share Bookmark Print

Rating