Wanaume wa leo hawajui kusema la!

Na MWANAMUME KAMILI

Imepakiwa - Tuesday, October 28  2014 at  15:27

Kwa Muhtasari

Mtihani wa mwanamume sio mchezo! Ole wenu nyinyi wanawake wenye kudakia uhusiano kama daladala!

 

MTIHANI wa mwanamume sio mchezo! Ole wenu nyinyi wanawake wenye kudakia uhusiano kama daladala! Shauri zenu wenye pupa wanaokimbilia nyumbani kwa mwanamume kutafuta hifadhi na vichele vya masurufu! Usije juta kugundua umebaki gogo la mzinga na makapa yasio na asali!

Wanaume wa leo hawajui kusema la! Kila kitu wanakitia kinywani japo mara kwa mara hawana haja kula kushiba. Hivyo basi ni wajibu wa mwanamke anayetaka kuolewa na kudumu kwenye ndoa kuwa makini kutambua mitihani atakayokumbana nayo nyumbani kwa mwanamume.

Miaka saba na zaidi kwenye uchumba na mwishowe utapakia nguo na kwenda zako. Hakuna mwanamume kamili atakuoa hujapita mtihani. Hilo sahau kama ulivyosahau nyonyo udogoni. Sisemi kwa kejeli au ufidhuli, lakini ndio ukweli wa mambo. Mwanamke anahitaji maandalizi kabambe asijeachwa kwenye mataa na kilio cha mbwa mdomo juu! Jongea utahiniwe!

 

Rundo la vyombo

Kwanza, mwanamume akikualika nyumbani kwake ukumbane  na rundo la vyombo vilivyojaa mabuu na nguo chafu chini ya kitanda usihadaike kwamba ni mchafu na mvivu. Alijua waja. Angalihofia aibu angalifua na kuosha vyombo!

Pili, unapoingia chumbani ukasikia mwanamume anampigia simu “mama wa usafi” aje kupiga deki na kuosha nyumba kwa malipo, usidhani mwanamume hataki kukuchosha wewe totoshoo!  Anataka wazo kutoka kwako, angalau uonyeshe kuwajibika! Akifika “mama wa usafi” kushika kazi zozote ukiwa nyumbani humo, huna chako. Utaliwa na kutemwa kama pipi iliyokwisha ladha! 

 Tatu, ukikuta nyumba imejaa vyakula aina ainati na apendekeza mwende kula mkahawani, tafadhali nawe usiwe mpumbavu kuanza kumtajia vibanzi na kuku choma! Usirembue macho eti mume anakujali sana. Ni mtihani wa mke kuandaa chakula kitamu kwake!

Nne, siku moja akupe miadi kwenda ziara za porini au kutalii mikoa halafu unapofika kwake unamkuta kajikunyata kama jongoo kitandani. Isitoshe, anakuomba pesa za kumtumia mamake au dadake! Mwanadada, usikunje sura kwa kero wala usianze kuzungusha mboni kama lumbwi! Onyesha unavyomjali na unavyowajali watu wake!  

Tano, unapomtembelea mwanamume ukakuta anapika au anafanya usafi nyumbani, usiketi na kubonyeza kiungambali. Eti wewe na runinga ilhali mwenzako yuko jikoni analizwa na vitunguu! Ukiomba kumsaidia anakujibu,”endelea kutazama runinga, namaliza kazi!” Halafu makalio unayajaza kwenye kochi! Kweli siku zako zinahesabika! Mweleze jikoni ni kwa mke! Mwondoe hapo haraka. Posa utalipiwa mara mbili!

Sita, tuliza kichaa na wazimu wa ujana! Dhihirisha ukomavu na stahamala – vigezo vya mke mwema!

Akizungumza, tulia! Akitoa jicho, nywea! Domodomo eti humezi mate? Mbishani, wewe husikii na hushauriki? Simu, huachi kupiga na maswali ya kitoto? Vituko hivi havikupi mwanamume kamili! Na ukimpata haishi nawe!

Ama wewe ni wa kuteta tu maana hujapigiwa simu au hujaandikiwa arafa hata moja siku nzima! Acha kujipenda! Utaishia kulia chozi kwa wivu wa kitoto bure bilashi! Mke mwema hafichiki!  

Saba, mwanamume akikuvua nguo za juu tafadhali jifunze kumsisitizia kwamba wajitunza na hutaki masihara kabla ya ndoa. Wengi wenu ndio kwanza mtaacha nguo zote sebuleni mkatembea nyumba nzima uchi kama kumbikumbi! Adabu hiyo ni ngao, hadhi na hesima kwa mawanamke. Siku zote tunashinda na vicheche nje, hata nyumbani? Mke mwema lazima ajue vya kubana! Na ajue wapi pa kubanua!

Nane, makinika unapokwenda kwake angalau ubebe vitu vidogo kama nyanya na vitunguu. Usiwe mwanamke wa kujaza tu chupi na vipodozi kwenye mkoba! Hizo ndizo akili wanazochukia wanaume.

Tisa, wakati mwingine nenda kwake na kaseti zenye nyimbo za injili angalau ukipika uwafukuze mashetani kwa nyimbo za kutuka Rabuka. Ukifanya hivyo mwanamume ataona tofauti kati yako na wale mashangingi wanaoimba kinyaa na utashi kwenye vilabu vya walevi.

Kumi, tuliza kichaa na wazimu wa ujana! Dhihirisha ukomavu na stahamala – vigezo vya mke mwema! Akizungumza, tulia! Akitoa jicho, nywea! Domodomo eti humezi mate? Mbishani, wewe husikii na hushauriki? Simu, huachi kupiga na maswali ya kitoto? Vituko hivi havikupi mwanamume kamili! Na ukimpata haishi nawe!