Raha za kuhubiana na kukwepa

Na MWANAMUME KAMILI

Imepakiwa - Thursday, October 30  2014 at  13:48

Kwa Muhtasari

Mwatudunisha mno kwa zenu raha za kuhubiana na mwishowe kuwakwepa wenzenu kama wenye maradhi.

 

Sura jaamali ni majaliwa.

Msinione sura mbovu mkadhani hakunipa Rabana.

Wala msidhani raha yangu kununa na kukereka kama sokwe mwingi wa nyege.

Nyie wanaume wa leo mwatuvunjia heshima.

Mwatudunisha mno kwa zenu raha za kuhubiana na mwishowe kuwakwepa wenzenu kama wenye maradhi.

Acheni niyatoe moyoni angalau msitishe hizi tabia za kuwapachika mimba wanawake ambao hawana haja kulea wala uwezo wa kuwatunza watoto.

Mwanamke kushika mimba asiyopangia wala kuhitaji inazidisha hatari ya uavyaji.

Wataavya, mpende msipende!

Mimba hizi za kiholela zinachangia pakubwa kuwepo watoto mitaani wanaoishi na kula mapipani.

Sio kosa lao kuzaliwa.

Ni kosa la mume na mke ambao hawakuchukua tahadhari.

Binadamu wa leo si watu.

Wanajua lakini hawataki kujua!

Ni kosa kwa mwanamke kutanguliza tamaa ya mwili na kushindwa kutumia akili.

Ni kosa la mwanamume ambaye kwa kupenda raha ya kufunga magoli hushindwa au hukataa kuchukua tahadhari kuzuia karaha ya matokeo mabaya ya mechi.

Wengi wa wanaume wa leo ni sampuli hii.

Wanakula raha na kila janajike lakini hawataki kamwe kulea watoto ambao ni mazao ya ulimbukeni wao.

Ndio sababu ya kesi mahakamani zisizokwisha.

Kukidhia mahitaji ya watoto nje ya ndoa imekuwa kama biashara; kila mmoja akitafuta mnofu mzito sisemi gala la kuchumia.

Ole nyinyi wenye kula uroda na kukwepa alfajiri!

Sitazungumzia sana uzembe na ujuha wa baadhi ya kina dada kujipendekeza na kujidekeza kwa wanaume wakijua wazi hatari ya ngozo za kiholela!

Naambiwa eti ni udhaifu wa kike kushindwa kukataa vya bwerere vikiwemo mimba na magonjwa ya zinaa.

Shauri ni lao!

Paka kubeba nundu la ngo’mbe ni ridhaa yake.

Mtu hujikwaa mara moja!

Mbona msijue mbinu wanazotumia wenzenu kuwanasa?

Mwanamke usiyemhitaji maishani wafanya nini naye chumbani kwako?

Nionyesheni mume aliyekufa kwa kupeza huba?

Lazima mwanamume kamili awe na mpangilio maishani.

Ajue wa kula na kusaza!

Mwanamke usiyempangia mema ya usoni anashinda kwako siku kadha akifanya nini?

Mwenzio umfyonze ladha kisha umteme kama ganda la mua!

Hata kama kajileta mwenyewe kama wanavyofanya kina dada wa leo, mbona usimwitie babake?

 

Kuokotana vilabuni

Mwanamumue kamili hufanya maamuzi ya busara.

Sitisheni tamaa na mdumisheni hadhi!

Hizi tabia za kuokotana kwenye vilabu vya walevi mtazikoma.

Nyote walevi tena vichwa pumba.

Saa ngapi mtakumbuka kinga?

Heri ukose kichwa lakini bakisha punje la ubongo angalau kuzuia majuto.

Kuna wanawake watu wazima wanaojua kuzihesabu siku za hedhi.

Japo ni wachache kama vidole vyangu.

Eti wamesoma lakini somo hilo liliwapita kama unyunyu wa baharini.

Chaka limekujaa nyetini na mambo ya mimba hujui?

Iweje wajua kula usijue kushiba?

Angalau tafuteni wanaojua kubana siku za kubana.

Achaneni na visichana visivyo na akili.

Jamani wanaume wa leo, shida zenu mwajitakia wenyewe.

mwanamume@yahoo.com