Mwanamume gumegume hana shukrani hata chembe!

Imepakiwa Wednesday November 5 2014 | Na MWANAMUME

Kwa Muhtasari:

Jamani ewe mke mwingi wa chozi na masikitiko, mbona kujinyima usingizi wa pono eti walilia mwanamume aliyetelekeza nyumba?

JAMANI ewe mke mwingi wa chozi na masikitiko, mbona kujinyima usingizi wa pono eti walilia mwanamume aliyetelekeza nyumba?

Kwa nini ukonde bure kwa kuwazia na kumfikiria mwanamume aliyekwepa majukumu na kukuachia malezi ya watoto?

Badala ya chozi na sononeko, jinasue na jipe raha!

Walilia mtu angali hai, je mfu? Kuvunjika kwa mwiko sio mwisho wa upishi. Kuachwa na mwanamume ni kama champali kukatikia njiani. Nani kakatikikiwa champali akashindwa kufika nyumbani?

Ukweli wa mambo ni kwamba waweza kujitolea mhanga kumpa mwanamume mapenzi ya kilo, tena nafuu bila kero wala bughudha, lakini usishangae kumwona bwege akikutetesha kwa makeke na kelele kama kwamba hujamfaa kitu. Utampata madanguroni akitafuta uroda wa kupimiwa tena kwa malipo.

Waweza hata kujimega kwa kisu ukampa mikononi kijisehemu anachotaka lakini katu mwanamume wa leo haridhiki, hatulii, hamakiniki na hana shukrani. Hao ndio wanaume tunaolilia! Ni nadra kumpata mnyenyekevu, angalau mmoja aliye radhi kutulia nyumbani kwa maslahi ya wanawe.

Kama sio kwenye mabaa, wako mitaani na mijini kwenye vilabu vya pombe wakinywa na kula mfano wa fisi. Wako kwenye vijia vya gizani wakipokezana magonjwa ya zinaa na makahaba. Wako vigodani chini ya kivuli kwa hadithi na ngano za kisiasa huku mashavu yamejaa majani ya miraa.

Utampata mwanamume masikini nyasi. Ni mume jina tu. Anaishi sio kwa chakula bali maponeo. Anavalia shati na suruali moja akifua na kuanika utadhani mvuvi. Miguuni anavalia makubadhi yaliyolika nyayoni yakaemea ubavuni.

Ukishampa mapenzi na mwongozo akawa mtu mbele ya watu, ndiye wa kwanza kukugeukia na kukuponda kwa matusi yasiyoandikika.

Hawanitishii maisha hawa ndugu zangu. Wapo wanaume wenye misuli lakini chumbani hana jamvi sisemi kitanda. Hana kitu na hana uwezo wa kuwa navyo hivi karibuni! Hana mswaki sisemi dawa ya meno. Ole wewe mgeni mwenye meno ya kung’aa!

Mwanamke akajitolea kukuelimisha

Jamani wanaume wa karne hii, mna kichaa? Mwanamke akajitolea kukuelimisha kwa kusudi la kukufanya mtu wa hadhi. Mtoto wa mtu amekulipia karo na kukukidhia mahitaji. Lakini mwisho wa masomo unageuka mwenye mashobo usitake kumwona wala kumsikia.

Mtoto wa kike amekuvisha na kukulisha. Amekuvulia na kukufulia. Hakuna linalofanyika duniani ambalo hakuthubutu kwa maslahi yako. Mwishowe unashikwa na pepo wa huba na tamaa ya kipumbavu na kumwacha mwenzio eti hafai kitu! Kama kweli hakufaa kitu wala mtu, mbona muda wote ukamhadaa?

Sijui kujifanya wala kujipendekeza mbele ya watu. Wala sina moyo wa huruma. Sijui kabisa kumsamehe mtu.

Lakini mke wa kunifanya mtu mbele ya watu kwa nini nisimpe mwili, roho na nafsi? Kwa nini nisijitolee kufa kupona angalau kumfaa jinsi alivyonifaa? Nitaishi kwa yake maslahi.  Mwanishangaza wanaume wa leo!

mwanamume@yahoo.com

Share Bookmark Print

Rating