Mwanamume ni kudhibiti matamshi na fikra

Na MWANAMUM

Imepakiwa - Tuesday, November 11  2014 at  15:52

Kwa Muhtasari

Mwanamume si ndevu, kwani hata mbuzi anazo! Mwanamume kamili ni akili tulivu, mawazo chanya na vitendo vya hadhi.

 

MWANAMUME si ndevu, kwani hata mbuzi anazo! Mwanamume kamili ni akili tulivu, mawazo chanya na vitendo vya hadhi.

Mtulivu asiye mwingi wa makeke ndio mwanamume wa kukufanya mtu.

Hao waliomeza kanda na wanaotapika maneno ni makubadhi sisemi viatu!

Utamtambua mwanamume kamili kutokana na jinsi anavyojizatiti kudhibiti sio tu kinywa na ulimi bali pia hisia na fikira potovu.

Wacha watu wakuite maji ya mtungi lakini wasijue yaliyokuziba kifua.

Ndio maana kasuku hana uwezo wa kuoa licha ya kuwa mwingi wa maneno!

Bila shaka tunasikitishwa na wanaume majisifu. Yaani kina yakhe wasiojua kufyata vinywa na kudhibiti ndimi zao.

Neema ya ulimi hali kadhalika uwezo wa kuzungumza sio halalisho kwa mwanamume kupayuka na kuboboja kivoloya. Waishi wajisifu, ukiwa mfu waliohai watasema nini?

Mbele ya watu mwanamume kamili ni mnyamavu, msikivu na mtulivu. Hutumia muda wake kushika mawili-matatu kati ya mengi yanayosemwa.

Hawa wa leo wamempiku kasuku! Wanajifanya kujua kila kitu na kila neno. Hawaambiliki. Hawasemezeki. Hawashauriki. Nyumba haikaliki kwa kero na ubishani.

Mwanamume king’ang’anizi hatari! Anaweza kukupa shinikizo la damu kwa vijimambo tu.

Kinachowasha ndimi zenu nini? Jambo lisilowahusu mwaliteka na kujenga mada ya ugomvi kwalo. La mapenzi, mnalibeba begani na kujifanya mlivyo wembe wa kukata. La mekoni, mke hatoshi.

Sasa kila kitu ukijua wewe, mbona hilo la himila na kuzaa likakushinda?

Na sio kuzungumza tu inayoudhi.  Baadhi yenu mko tayari kutetea hoja zenu kwa ncha ya upanga.

Jamani nani anataka kuolewa na mwanamume asiyesikia wosia wala nasaha? Mie sikondi kwa kuzomewa na kubezwa siku zote. Kama ni asali zeeka nayo!

 

Kosa la nyumbani mnalitoa nje

Kuna hatari kubwa kuishi na mwanamume kasuku. Upendo hupungua na kukatika mara moja! Rahisi sana kutibua amani kwa ugomvi. Maamuzi ya nyumbani hayana maafikiano. Hakuna kujitolea kwa maslahi ya wawili. Hizi ndizo sababu za wengi kuchepuka na  kutafuta hifadhi na liwazo kutoka nje ya ndoa!

Woga ni ngao. Unyamavu ni hekima. Jamani tabia za kuwavua wenzenu hadharani mtaziacha lini? Kosa la nyumbani mnalitoa nje na kulijadili kwenye vikao vya walevi. Hizo tabia za wasusi na wasukwa, nyie wanaume mwazitoa wapi? Shombo na ulimbukeni wa mwenzio sio hoja ya kujadiliwa vijiweni.

Hata kama mkeo ni gogo lisilokwea na kushuka nyakati za haja za watu wazima, mbona msiyamalize hayo chumbani? Kweli hiyo ni hoja ya kujadiliwa kwenye kumbi za walevi?

Mpaka makeke ya ulingoni mwataja? Hizo ni akili za mwanamume au za samaki kumeza chambo?