Kumbikumbi pia hujawa na aibu, sembuse binadamu

Na MWANAMUME KAMILI - CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, November 19  2014 at  17:06

Kwa Muhtasari

Nguo za mtu huficha siri. Wala hakuna mwenye radhi kufichua siri hiyo ila mwenyewe kwa hiari. Nalemewa kwa shehena ya soni na aibu kufuatia visa vya wanawake kuvuliwa nguo hadharani! Jamani hata kumbikumbi hujawa na aibu, sembuse binadamu.

 

Nguo za mtu huficha siri. Wala hakuna mwenye radhi kufichua siri hiyo ila mwenyewe kwa hiari.

Nalemewa kwa shehena ya soni na aibu kufuatia visa vya wanawake kuvuliwa nguo hadharani! Jamani hata kumbikumbi hujawa na aibu, sembuse binadamu?
Jamii zetu sio tena makazi ya waja wenye huruma na upendo. Kweli, tunaishi pamoja na hayawani, wanyama wa porini waliokosa sio tu hisia bali pia utu. Wanaume  zumbukuku – majuha – vichwa  pumba – waliochukua sheria mikononi mwao na kumfanyia unyama masikini binti wa mtu jijini Nairobi hali kadhalika Mombasa wanapaswa kutafutwa kwa kurunzi na kuchukuliwa hatua kali za kisheria. Napendendekeza adhabu kali kuwapa adabu.
Ikiwezekana, wanaume hao wazunguke jiji bila nguo angalau hata sisi tufurahie kuona hivyo vibanzi walivyobana pachipachini.

Baadhi yenu mkivuliwa mtajificha kwenye vidimbwi vya maji taka! Ndivyo! Jicho kwa jicho hupoofusha dunia. Heri dunia iliyojaa vipofu kuliko kuishi wa wanyama wasioheshimu nafsi na siri za wenzao. Mimi mwingi wa hamaki. Walinilazimisha kuona mambo sijazoea kuona ila kwa chabo, tena kwa ncha ya jicho tu.

Nadra kuona mambo haya. Hata nikiwa na radhi na hiari ya mwenyewe, bado mwili hujawa na vimbimbi!

Uhawayani
Sasa akili timamu za watoto wetu sio zao tena. Washaingiwa hofu, shauku na jazba. Wanatembea wakinyatanyata. Wanahisi kama kwamba hata wao wamevuliwa hadharani! Najua anavyohisi masikini mwanangu ila tu hawezi kunieleza! Aliona niliyoyaona. Alihisi nilivyohisi. Sote tulifikicha macho kuficha mhemko uliojaa moyoni. Wanaume wa leo sawa na hayawani!
Sio mara ya kwanza wanaume kufanya vitendo vya kihayawani kama hivyo. Imekuwa kama desturi hasa. Inawezekanaje wanaume watu wazima, tena wazazi waliozaa kuamua kwa pamoja kumteka na kumvua mwanadada hadharani?

Hilo halikutosha. Walimnyanyua hobelahobela, wakampapasa na kumtomasa sehemu nisizoweza kuzitaja. Yote hayo yalitendeka kwa manufaa ya wanaume waliofurahia sinema ambayo kwa hakika walipeza mno.
Mwasingizia tu mavazi duni ili kujiondolea lawama kwa ujuha mliotenda. Mwanamume wa leo hawezi kumwona mwanamke mbele yake asiwazie ila.

Hata kama kila mwanamke atavishwa kanzu inayomfunika tokea utosini hadi nyayoni, macho ya wanaume wa leo yatapenya na kutafuta walichobeba wanawake vifuani na makalioni.
Nani kawahadaa na kuwapa fikira potovu kwamba mavazi ya kike yanawalenga? Makahaba wamejaa mijini sio kwa kufurahia kuzizima mili kwenye baridi.

Ni biashara iliyofanikishwa kwa kuwepo wanunuzi si haba. Mmewazoesha kwa kuwalipa vichele vya pesa kuwatumbuiza wakiwa uchi wa mnyama kwenye majukwaa ya vilabu vya densi. Mbona leo kuwafedhehi mchana kwa kuwavulia nguo?

swahilihub@ke.nationmedia.com / mwanamume@yahoo.com