Uvumilivu ni ngao, ukatili sio sifa ya mume kamili

Na MWANAMUME KAMILI - CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, November 26  2014 at  15:38

Kwa Muhtasari

Ukimwona mwanamume mwingi wa lalama na tetesi, mwepesi wa hasira na mpenda vita tahadhari kabla hatari.

 

UKIMWONA mwanamume mwingi wa lalama na tetesi, mwepesi wa hasira na mpenda vita tahadhari kabla hatari.

Sharti wanawake kutahadhari na wanaume wenye tabia na ishara za kinyama. Wanaweza kukukatizia maisha ungali mwana mbichi.

Isitoshe, wanaweza kukupa donda la maisha lenye uchungu na majuto. Heri upweke kuliko ubishi na mume wa leo. Ndio ushauri nitakaowapa wanawake vichwa vya ngiri na midomo ya kasuku

Utulivu na ustaarabu ni vigezo kamili vinavyodhihirisha ukomavu wa mwanamume. Ukomavu unadhihirika katika vitendo na matamshi ya mume.

Matamshi ya mwanamume kamili sharti  yahimize unyoofu, yashawishi uugwana, yashauri bidii, yasisitize uadilifu na uajibikaji maishani.

Sharti mwanamume awe mfano mwema kwa familia na jamii nzima. Lakini sivyo alivyo mwanaume wa leo. Hasira kama mkizi. Matusi na utashi. Vitisho na hila. Nani haukulizwa na kisa cha huyo mzee wa miaka sabini kumwua mkewe kwa kumkatakata kwa upanga? Hakustahili kufa kwa ncha ya upanga masikini nyanya huyo huko jimbo la Busia.

Sitaki kutonesha vidonda vya moyoni hasa kwa familia zilizohasirika kwa mauaji ya kinyama yaliyotekelezwa na magaidi huko Mandera. Hiyo ni ishara tosha kwamba wanaume wa leo hawana upendo wala hisia. Si watu tena!

Wangalikuwa watu wenye utu, wasingalitekeleza unyama kama ule. Mja mwenzio hana kosa, huwezi kumwonea hata chembe cha huruma? Vipi mwanamume anaweza kumpiga risasi kwa raha zake mja mwenzake, hasa mwanamke?

 

Mauaji ya kinyama

Visa vya mauaji ya kinyama vimeripotiwa katika maeneo mengi humu nchini. Mara mwanamume kanyonga mkewe baada ya ugomvi. Mara mwanamume kateketeza wanawe baada ya ubishi na mke.  Mara mwanamume  kateketeza nyumba kwa kumshuku mke.

Sielewi jinsi mwanamume anavyoweza kuwageukia wanawe na kuwachanja mili kwa kisu au kuwatumbukiza kwenye kindimbwi cha maji.

Nini hasa sababu ya mume kuwatesa wanawe kwa kosa wasilojua? Visa hivi vinadhihirish jinsi mwanamume wa leo alivyopungukiwa na akili sisemi kukosa hisia za kiutu!

Uvumilivu ni ngao! Ukatili hauna nafasi katika maisha ya mwamume kamili. Najua ugumu uliopo kwa wanawake wa leo kutaka radhi au hata kunyenyekea. Lakini hakuna kosa la kibinadamu linalostahili adhabu ya kifo, tena kifo cha panga au risasi kichwani!

Tuukomesheni ujahili na ujinga wa jicho kwa jicho.