Sihadaike na umbo, mke mwema ni tabia si sura

Na MWANAUME KAMILI- CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, December 10  2014 at  10:00

Kwa Muhtasari

Mume wa leo balaa! Anavyozuzukia maumbile ya wanawake, utashangaa na kubaki kinywa wazi mdomo juu! Daima, tabia za mke ndizo kigezo cha kwanza! Utamjua mke mwema kwa tabia zake. Kama ni sura, hata chura anapendeza macho

 

Mume wa leo balaa! Anavyozuzukia maumbile ya wanawake, utashangaa na kubaki kinywa wazi mdomo juu! Daima, tabia za mke ndizo kigezo cha kwanza! Utamjua mke mwema kwa tabia zake. Kama ni sura, hata chura anapendeza macho
Mambo ya kuchanganywa na kuchanganyikiwa, tuwaachie wapishi wa pure! Ndio wanaojua vipimo vya mahindi kwa maharagwe vinavyounda angalau chakula kinacholika. Mwanamume kamili ni akili timamu.
Wewe mwanamume, mbona wachanganyikiwa na kuchanganywa na maumbile? Jana rangi ya ngozi! Leo sura! Kesho miguu! Kesho kutwa, umbo! Mtondo, uzito wa paja. Mtondogoo, sijui nyusi na kope? Jamani watafuta mke au sanamu ya kutundika sebuleni kufurahisha wenye macho?
Msijesahau kwamba sura ni kama ua linalochanuka asubuhi na kunyauka magharibi. Umbo halidumu wala halisitiri penzi. Punde si punde mashavu yatamomonyoka. Ngozi itaparara. Kifuani hamtabaki kitu ila malapulapu. Kama ni miguu, heri kuoa meza! Kuzuzukia sura zenye ucheshi, bashasha na tabasamu kama wanavyofanya wanaume wa leo ni ulimbukeni na uzuzu ambao daima huja na majuto.

Uzuri wa mkakasi
Nionyesheni mwanamke hata mmoja mwenye tabia mbovu aliyedumu kwenye ndoa kwa sababu ya kuwa mrembo wa kumithilishwa na malaika. Nionyeshe mwanamke hata mmoja aliyenogesha huba na upendo chumbani kwa kutumia sura yake nzuri! Ndoa kudumu ni tabia ya mke!
Sura si kitu, si chochote! Sijaona ratili inayopima uzuri wala ubovu wa sura ya mtu. Ole nyinyi kina yakhe mnaobagua wenzenu kwa misingi ya sura zao. Sura ingalidumu na ingalikuwa na thamani ya haja, basi shilingi isingalitoka mfukoni! Mwanamke ni tabia nyoofu. Kama ni sura, tuiachieni shilingi! Kama ni rangi tushamwona kinyonga, hiyo yako si kitu!
Mimi ningali mzazi! Sijamaliza mbegu zote kwenye koka wala sijui uzuri au ubovu wa sura fiche nilizobeba. Sijui uzito wa paja wala urefu wa miguu ya binti zangu. Na sitaki kujua! Jukumu langu kama mzazi ni kukuza binti wenye tabia za kunatia. Mwanangu utamposa nyumbani kwangu wala sio kwenye baa!Tabia zao jukumu langu, sura kazi ya Mungu.
Dunia ya mke anaitawala Mchina! Sihadaike na umbo. Huwezi kuwa na hakika na maumbo yaliyoviringa wala nywele zilizoshuka kama singa za farasi. Kucha, kope na nyusi si zake! Lau si viatu, mwenyewe mbilikimo! Uzuri wa mkakasi ndani kipande cha mti!
Kweli maisha kinaya! Waliopo hatuwataki, na wanaotaka tuwape tunawakagua na kuwabagua. Heri kuona kwa moyo kuliko uzuzu wa jicho!


obene.amuku@gmail.com