Mnawaposa wakiwa mbichi na kisha kuwadhalilisha katika uzee wao

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, December 17  2014 at  19:10

Kwa Muhtasari

Enyi wnaume wa leo, sikilizeni hizi sauti za kina mama. Sauti za ndani kwa ndani zinazoashiria sononeko moyoni. Sauti za wanyonge wakilalama jinsi nyinyi mnavyowatenda na kuwatendea unyama. Hivi ndivyo vilio vyao.

 

ENYI wanaume wa leo, sikilizeni hizi sauti za kina mama. Sauti za ndani kwa ndani zinazoashiria sononeko moyoni. Sauti za wanyonge wakilalama jinsi nyinyi mnavyowatenda na kuwatendea unyama. Hivi ndivyo vilio vyao.

“Madume na majibaba wa leo, hongera kwa kudhibiti dunia viganjani vyenu. Hongera kwa hadaa zenu. Kweli, uwezo ni wenu kututenda sisi wenzenu mtakavyo. Lakini kumbukeni zipo siku za mnyonge kucheka na mdhalimu kufikicha macho kwa kilio cha majuto! Zipo siku za laiti ningalijua….”

“Wanyonge wanyongeni lakini nafsi siwapokonye. Vifyefye mvifinyange lakini hadhi siwavue. Sisi binadamu kama nyinyi japo uwezo hatuna kuwatenda na kuwabonda licha ya kwamba mwatuburura chini kama mizoga. Maisha yalikusudiwa kuwa yetu wawili lakini nyie weveru mkajipa na kutufanya wajinga kula sahani moja na vibiritingoma mitaani. Tumesalia na sononeko huku nyie wenye uwezo mkiwanda kama gugumaji.”

“Mwanamume mwenzangu, uliniposa mwana mbichi, ya dunia siyajui. Ulinibembeleza kwa ahadi kochokocho na zawadi zilizonifumba macho. Moyo wangu ukauyeyusha kwa nyama ya ulimi ulonilisha. Ukaniambia dunia ni yetu, raha ni yangu nivae nipendavyo. Mbona leo wanidhalilisha,kunivua nguo na nafsi hadharani. Unavyojidunisha, nami mwenzio nasononeka kwa dhihaka za dunia”

“Kwako nilikuja na kizinda cha ujanani. Ngeu ikanichiririka kwa raha ulojipa. Mengi ukanifunza na kunifanya mjuvi wa mambo kwa raha yako.

Mbona leo wanifedhehi kunitukana usiku kucha? Umenigeuza mlinzi kukusubiri usiku kucha. Nyumbani waja kwa ridhaa, tena kwa wakati uupendao. Si mke wa kubembelezwa tena mimi ila umenigeuza mtumwa wa kutukanwa na kuzomewa…”

“Mimba umenibebesha na kuniachia malezi na nasaha. Kazi za sulubu umenifanyisha kuwakidhia wanetu. Wewe na vimwana, vimwana na wewe. Pesa unazo wala hazitufai kitu. Hatuli vyako, hatuvai wala kujifunika hata kanga uliyotununulia. Umetusahau na kututenga kama wenye ukoma, kosa lipi heri ule vitamu vya watamu nami sinifanye shubiri!”

“Vidonda vimenijaa tumboni. Kovu limenikaa kwenye kilindi cha moyo na chozi halinikauki shavuni? Dhuluma zako zimenikosha wala huna haja kunifanya mtu mbele ya watu. Ndio mapenzi hayo?”

“Umegeuka msaliti kunilisha sahani moja na wanawake wenzangu. Umegeuka msabasi kunidunisha mbele ya wenzako. Umegeuka kasuku kuniumbua kwa usemi wa kinyaa. Umenigeukia kunigonganisha na mahawara na mashangingi. Umenipokonya imani kwako kadhalika sina imani na maisha yangu tena. Lau si usalata wako nisingaliathirika hivyo!”

“Ulinitoa kwetu pasi na kovu kwenye ngozi yangu. Leo sihesabu tena alama ulizoniachia kwa kichapo kama bafe. Mimi si mwingi wa makosa ila wewe hukubali kukosolewa. Sisi wamoja, mbona kuniweka pembeni kama pembe zisizoweza kushuka chini ya kichwa cha ng’ombe?” “Umebaki kula na kuliwa na kina yakhe ambao katu hawakutufaa kitu. Mbona nisione uchungu? Mbona nisikuzike angalau nijue sina mwanamume?

obene.amuku@gmail.com