Usiwe mzito kutafakari na mwepesi wa kunena

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, December 31  2014 at  15:04

Kwa Muhtasari

Napenda sana wanaume labizi wanapokutana na kuzungumza juu ya mambo kadha wa kadha. Mikutano baina ya waja ndiyo huchangia ukuaji wa akili na ukomavu wa fikira sisemi kuimarisha maisha ya mwanamume. Chuma hunolewa na chuma.

 

NAPENDA sana wanaume labizi wanapokutana na kuzungumza juu ya mambo kadha wa kadha. Mikutano baina ya waja ndiyo huchangia ukuaji wa akili na ukomavu wa fikira sisemi kuimarisha maisha ya mwanamume. Chuma hunolewa na chuma.

Napenda vilevile kusilikiza mazungumzo baina ya wanaume wepesi wa akili; wenye nasaha, hekima na taadhima. Napenda kubadilishana mawazo na watu; wadogo kwa wakubwa wenye ujuzi wa miaka na mikaka angalu kujifunza mbinu za kukabiliana na changamoto za maisha.  Siwezi kuwa mwanamume jalili pasipo hekima ya hao walionitangulia duniani. Wala sitaki kukumbana na maajabu ya dunia yatakayoniacha na kimako! Penye wawili hapaharibiki neno. Hiyo ndio hekima inayostahili kwa mwanamume kamili.

Kutia doa
Tatizo linalonikera ni kwamba wapo wanaume wanaopenda kujidunisha kwa tabia za kutia doa maisha ya wengine. Midomo kufunguka tu, mwanamume hutema cheche za chuki. Kazi yao hasa kukosoa, kudhihaki na kudunisha familia, wapenzi au hata wanawake ambao kila siku huwavulia na huwalilia. Mwanamume kasuku ni hatari mno. Wanaume hawa huchukua kosa la mke na kulifanya mada ya mazungumzo. “mke wangu mwingi wa shombo hunichefua badala ya kunifurahisha.”

“Mke wangu aliasi uroda nami labda amempata mwingine bora kuniliko” “Mke wangu limbukeni wa chumbani, hajui kitu!” “Mke wangu kilindi cha bahari, urefu na upana sina habari”

Mwanamume! Hata kama mkeo hulala chumba kingine mbali nawe, hayo ni mambo ya chumbani ambayo kamwe hayawezi kujadiliwa katika kongamano. Hayo ni ya wawili ambayo yanastahili kutatuliwa nanyi wawili. Tatizo kubwa kwa wanaume wa leo ni ulimi mwepesi kunena lakini ubongo mzito kutafakari kwa kina. Mambo ya ndoa si mzaha wa kupakana tope. Hekima ya mwanamume kamili ni kujua yapi yanayostahili kujadiliwa hadharani na yapi ya faraghani. Tendo la ndoa lina siri zake ambazo kamwe hazitoki nje ya kuta nne. Hii ni kwa sasabu kufichua siri hizo yaweza kuathiri kabisa uhusiano na kusambaratisha ndoa. Akija kujua mkeo kwamba yeye ndiye mhusika katika hadithi zenu, hutamwona wala kumwonja tena.

Jamani wanaume! Hata kama mwenzio hatosheki kula vyako, kuna haja gani kuwahadithia watu ambao hawajui umbo la paja sisemi upeo wa nyonga? Kwani huoni uwezekano wa kuwashawishi kina yakhe kukusaidia angalau kumtosheleza huyo uliyedai hatosheki?

Nilikuwa kwenye daladala nikasikia mume akimweleza rafiki yake, “nduru za mke wangu chumbani zimenichosha. Sijaanza shughuli, tayari yuko juu kama kengele!” Nikamgeukia na kumshauri kwa upole, ajaribu uroda na maiti! Wanaume wengine hawajui tofauti kati ya almasi na mawe.