Mke si kinu kutwangwa kwa mchi wa maneno

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, January 7  2015 at  12:05

Kwa Muhtasari

Chambilecho wahenga, dharau ni dhara! Mwanamke sio jimbu lipitishalo maji ya mvua na majitaka vilevile. Kila jambo – bovu na baya lavurumishwa kwake! Kila tusi – haluli na hasiri laelekezwa kwake!

 

CHAMBILECHO wahenga, dharau ni dhara! Mwanamke sio jimbu lipitishalo maji ya mvua na majitaka vilevile. Kila jambo – bovu na baya lavurumishwa kwake! Kila tusi – haluli na hasiri laelekezwa kwake!

Mke sio kinu kutwangwa kwa mchi wa maneno! Shamba lenye kwekwe halistawishi mimea sembuse binadamu?

Jamani wanaume! Ugomvi, vituko na visanga vya kila siku vinaweza kummomonya mke akabaki gofu asiyethaminika. Hivyo basi kila mke anastahili heshima na taadhima. Anastahili malezi na mapenzi. Huu ndio ukweli unaopaswa kukita akilini mwa kila mwanamume kamili. Mwaka mpya mawazo mapya.

Bila shaka tumekumbana na kushuhudia madume yenye ufidhuli na bezo lisilo na mipaka. Raha yao kuwafanyia wenzao vitendo vya kususuwaa.  Hawaambiliki, hawasemezeki. Wamejaa ghiliba na ghururi. Si watu wanaoweza kutumaniwa! Ndugu zangu wenye tabia hizi potovu, makinikeni na staarabikeni!

Badala ya kufuswa na kufyonzwa kwa cheche za matusi kila siku; mwanamke mwenye bidii kukuza uhusiano na kuimarisha ndoa anastahili hiba, hidaya na himidi. Vijizawadi vya kumchahawiza na maneno matamu ya kumlainisha moyo. Anahitaji limbikizo la sifa na pongezi kochokocho kwa juhudi za kila siku. Hiyo ndio mbolea ya mke.

 

Muondolee hatihati

Kumpa mke hiba na hidaya ni njia ya kudhihirisha upendo wa dhati.  Ni njia ya kumpongeza kwa jasho alilotiririsha kustawisha na kufanikisha nyumba. Kumhimidia mke humchangamsha mbele ya wenzake. Vilevile, humwondolea mke hatihati na kumfanya kutulia nyumbani kwake. Nani asiyependa heba kama hiyo?

Kinaya cha mwanamume wa leo ni kwamba hana haya kula na kunywa na mahawara vilabuni ilhali mkewe amekauka midomo kwa njaa na kiu. Mwanamume wa leo hana soni kufuja sisemi kuvunja kingo za hazina kuwatumbuiza mashangingi wanaokula na kutafuna nguvu za wanaume vichwa pumba.

Yote haya ni kwa shangwe za hangahanga sisemi jazba za mpito wanazopata wanaume kutoka kwa vibiritingoma. Mwanamume kamili ni mwingi wa taadabu, tena mwenye kukuza taadhimu. Sifa zake adimu ndizo tija ziletazo raha kwa familia. Hivyo basi mbona kuzidisha vilio kwa vitendo vyenu vya kihuni?

Mwanzo wa mwaka huja na dhiki kwa watoto na wanawake. Huu ndio wakati wanaume huasi nyumba na watoto na kukimbilia nyumba ndogo. Watoto wa mashangingi wakifadhiliwa masomoni tena katika shule za hadhi, masikini wana wa mtu watahangaikia mavumbini na kususurika vijijini.  

Hakuna haja kujifanya mwanamume nyumba ndogo ilhali wewe ni gumegume nyumbani kwako. Kukuza dharau ndani ya nyumba yaweza kuzidisha madhara na kuleta maangamizi.  Bila shaka natumai mwaka mpya utaleta mabadiliko kitabia na kifikira.