Mie kigae kidogo, katu sibishani na mfinyazi

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, January 14  2015 at  13:07

Kwa Muhtasari

Binadamu hajui thamani yangu! Sina haja wala kusudi kumkadiria. N’naridhika nilivyo! Natosheka moyoni.

 

BINADAMU hajui thamani yangu! Sina haja wala kusudi kumkadiria. N’naridhika nilivyo! Natosheka moyoni.

Sina ukamilifu, lakini naridhika kwa umakinifu alonituza Muumba. Mie kigae kidogo katu sibishani na mfinyanzi.

Wiki hii, nimekutana na watu wa ajabu waloniacha nimeachama.

Kwanza, nilikumbana na mwanamke wa ajabu. Shungi la nywele alilobeba lingempa farasi soni. Lakini zilikuwa gushi. Uso wake uling’aa kwa weupe wa ajabu.

Lakini mikono na miguu yake ingemfanya mamake mzazi kulia kwa uchungu.

Weusi ulikinzana na weupe na kumpa madoadoa ya pundamilia.

Nikakutana tena na janadume, barobaro mwenye misuli ting’inya.

Nywele zake kazitia rangi aina ainati. Kajipodoa na kujirembesha usingejua ni mwanamume lau misuli na kifua mlazo.

Athari za kemikali

Ngozi yake iliyometa juani ilidhihiri athari za kemikali zinazochubua na kubadili rangi ya ngozi.

Mwendo wake wa madaha uliwaacha wanaume wakishangaa jinsi dunia ilivyowakengeukia.

Sijui kapewa sijui kajipa ya Mchina! Lakini janadume lile lilijaliwa zigo la matuta yaliyojaa nyuma na ambayo yalipanda na kushuka kwa kila hatua aliyochukua.

Begani katundika kipochi. Mpaka leo sijaamini kwamba hakuwa mtoto wa kike.

Vilevile, sijaamini kwamba alikuwa mwanamume kamili.

Bura yangu sibadili na rehani. Alivyoniumba Muumba ndivyo alivyokusudia, ndivyo alivyodhamiria! Sina haja kung’ang’ania ya dunia kwa raha ya waja wasio na haja nami ila kunitafuna kama mua.

Hata nikipembejwa pajani, katu sibadili maumbile. Sipo katika harakati za kutafuta ukware kwa kujichubua ngozi na kujiumbua mwili. Binadamu wa leo wanasikitisha!

Sitafuti umaarufu

Nitajipa hamasa kuboresha hali na hadhi yangu. Katu sizidishi hangaiko kutafuta umaarufu na muhtaramu.

 Hata madodo ya kifuani yakimung’unywa mwishowe hulala sembuse mimi kijitu cha mchangani?

Rangi yangu ya jongoo ndio hadhi yangu. Ufupi wangu kama mahindi ya Katumani ndio nguvu yangu.

Ufyefye wangu wa ndama ndio kwanza hunizidishia wepesi.

Ole nyinyi mnaojaribu kukosoa kazi ya Maulana. Ole nyinyi mnaong’ang’ania jinsia. Mtashiba kemikali na kuzitapika lakini kamwe raha mtaisikia tu kama taarifa wala hamtaishika.

Binadamu haridhiki na maumbile

Ni ajabu kwamba binadamu wa leo haridhiki na maumbile yake. Wenye nywele za hudhurungi ndio kwanza wanazitia rangi. Si nyeusi. Si kijani. Si nyekundu. Si samawati.

Tazama vichwa na miili ya wanawake kwa wanaume na utashangaa jinsi binadamu walivyokosa na kujikosea heshima.

 Akili zangu timamu na firidi. Sitaki kung’ang’ana kuyapika mawe kwa kuni mbichi.

Kwa sasa mwatafuta raha na mvuto wa dunia. Subirini papo hapo mtakuja jionea yaliyomfika mwendazake MJ.

Hewa ya kuchunjwa haikutosha kumpa pumzi. Pua lilikataa katakata kutulia likabaki kutiwa na kutolewa... Sijui mashtaka aliyosomewa mbele ya Muumba.

 Lakini najua alituaga akiwa mwingi wa majonzi na majuto. Laiti angalijua yaliyomsubiri, asingalibadili ngozi yake ya mpingo.

obene.amuku@gmail.com