Mume wa leo ameweka mawazo katika korodani

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, January 21  2015 at  10:49

Kwa Muhtasari

Pesa zimekuwa adui sio tu kwa wanaume wa leo, bali pia kwa wanawake.

 

PESA zimekuwa adui sio tu kwa wanaume wa leo, bali pia kwa wanawake.

Zimekuwa sawa na uwele wa upele. Mwanaume akiwa nazo, huwashwa mwili akajiona mwenye raha isiyo kifani.

Ghafla anakuwa mtindi na mtiriri, raha yake kupapasa. Mwanamke naye akizikosa, anakuwa sawia na ngiri asojua njia yenye hatari na shari.

Hujawaona wanaume wenye pesa wanageuka jogoo kutweza na kutomasa kila kuku apitaye karibu nao?

Hujawaona wanageuka wafidhuli kama mbogo, kazi yao kugombana kama panya wanaoishi tundu lenye maji? Na wanawake je?

Wanasema heri kuuguza jeraha la moyoni na pesa kibindoni kuliko jeraha la tumboni kwa dhiki ya njaa. Falsafa yao!

Sijamwona hata mwanamume mmoja ambaye si msumbufu na msumbi baada ya kupata pesa. Kwa kawaida hujiona kafika kilele cha maisha yasiyo karaha.

Pesa humpandisha mwanamume wa leo madadi, akazama katika kilindi cha anasa sisemi kunaswa kwenye mitego ya mashangingi wala watu.

Pesa hulevya na kuwaacha wanaume bila tafakuri na tathmini ya maisha. Wangapi wamesahau na kutelekeza familia zao punde tu baada ya kupata pesa?

Wangapi wamepatikana mitaroni wakielea juu ya majitaka? Utamu wa pesa eti! Wangapi wamewaacha watoto wakiishi kwa maponeo wakahamia nyumba ndogo kwa mahawara kuponda raha na kula jasho lao?

Silaha ya kuwindana

Sitaki kulaumu pesa kama chanzo cha uozo katika jamii. Ndivyo walivyo wanaume wanaothamini pesa kuliko akili.  

Mwanamume wa leo ameweka mawazo katika korodani. Ameficha ubongo kwenye pachipachi za miguu.

Pesa zimekuwa silaha za kuwindana katika pori la mapenzi. Pesa ni chambo kunasia vimwana wenye pua za kunusa pesa.

Raha yao kubeba mikoba iliyojaa poda na wari kurembesha nyuso. Jamani watoto wa kike, tangu lini mwili ukawa chumo?

Imekuwa tabia ya wanaume kununua upendo kana kwamba ni bidhaa sokoni. Maelfu ya pesa zinapunjwa kuhongana kwa kusudi la kuhubiana.

Upendo hauna thamani tena kwa sababu bei yake tumekwisha ijua. Wenye pesa hawajali hawathamini tena hadhi, utu na nidhamu.

Wanaume wa leo hawajali kukuza utu na kumheshimu mtu. Ilmradi amekupa pesa, atafanya anavyotaka na kukufanya anavyopenda. Lipi litakalomzuia ilhali alikupa pesa ulizotaka?

Mtaliwa kinyama

Hapo ndipo njia panda alikofikishwa mtoto wa kike siku hizi. Pesa atazibeba, na maradhi vilevile. Ole nyinyi vimwana wa leo. Mwatafuta pesa? Mtazila lakini nanyi mtaliwa kinyama!

Watoto wa kike! Mume anakufadhili kututumua kifua chako ili akifurahie yeye. Anakuhadaa kuchubua ngozi angalau kufaidi weupe wa ngozi yako.

Kwani wewe huna akili kujua mbivu na mbichi?

Punde si punde utasalia na chuki na choyo huku umeparara kwa maradhi ya moyo na fadhaa za maisha.

Utu una thamani kuliko pesa.

Ndio sababu masikini ni wangwana kuliko wakwasi japo matajiri wana wafuasi; kupe wasio na utu; raha yao kujisabilia mikononi mwa wanaume kwa tamaa ya pesa!

Sina woga kufa na ukata wangu lakini simhini mtu utu kwa vichele vya pesa. Pendo lako si bidhaa, silipi hata shilingi!

obene.amuku@gmail.com