Wanaume wengi wamegeuka debe tupu

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, January 28  2015 at  10:39

Kwa Muhtasari

Wanaume wa leo hawajui kufunga vinywa au kuvuta subira. Hawajui stara kunyenyekea mbele ya watu. Wamegeuka debe tupu linaotika!

 

HAKUNA roho isiyokongwa kwa sifa nzuri. Kila mja hutaka kusikia maneno ya kunogesha, tena ya kumwondolea mtu taharuki na wasiwasi! Maneno yaliyotonewa nakshi ndio kwanza humpa mtu raha na kumwongezea hamu na hamamu ya maisha. Watu wazuri hutambulika kwa sifa nzuri. Na sifa nzuri zinaambatana na unyenyekevu.

Japo sifa za mtu ndizo humwangazia, twahuzunishwa mno na tabia za madume majisifu. Inachukiza upeo wa chuki kumwona mwanamume asiyejua stara ya ulimi. Midomo kufunguka tu, vijembe! Si mali, si rasilimali si maumbile. Mungu kakupa kila kitu kisiri. Iweje unawashwa midomo kututangazia? Mwanamume kuchuuza jina ni ulimbukeni. 

Jamani raha gani kuhadithia umma uwezo na nguvu zako?  Isitoshe, kuna haja gani kujichocha na kujishaua mbele ya vimwana? Kama kunena lazima, tueleze udhaifu wako. Tusimulie ulivyo juha, jura lisiloshika! Hilo ndilo gumu kuliona. Walivyosema wahenga, halua si haluli! Situjazie nta masikioni kusikiza mapepe yako. Mbona kutunywesha masuo nasi tuna vinywa kunywa yaliyo safi?

 

Stara

Wanaume wa leo hawajui kufunga vinywa au kuvuta subira. Hawajui stara kunyenyekea mbele ya watu. Wamegeuka debe tupu linaotika! Tabia hizi zinadhihirika hasa katika harakati za kujinasibisha. Mtoto wa mtu anayejua hadhi na heshima ya kike kamwe hatekenyeki kwa vijembe vya kijuha. Kumtongoza mwenzio kwa kujipalia sifa za uongo ni sawa na kumpa muye! Hujampa kitu ng’o!

“Mimi ndiye mkurugenzi wa kampuni hiyo maarufu!” “ Nilikuwa wa kwanza kuliendesha gari hilo!” Aha! Sifa za mwezi twaziona wala hatujamsikia akitamka neno. Wewe mja tu, una nini ambayo sharti ututangazie?  Kama mali, hakuna tajiti kuliko kanchiri. Humiliki himaya ya kifua tena kimyakimya!

Midomo inayokiriza kama simu hudunisha mwanamume. Ndivyo walivyo hawa wa leo. Wamegeuka kasuku kunya rasha ya maneno. Mwanamume kamili hana haja kupuliza tarumbeta mbele ya vimwana. Tabia za wanaume majisifu zinawapa wanawake jelezi na jekejeke bure. “Sisi tuna macho yanayopenya acha kuona! Hakuna haja kujinadi kitoto; kama unavyo, vitaonekana wazi.” Hiyo ndio kauli ya wanawake.

Hekima kwa mwanamume kamili ni usikivu na utulivu. Sifa za kujipa si sifa. Hawa wa leo wamempiku kasuku! Hakuna kitu wala jambo wasilolijua. Hawaambiliki hawashauriki. Hawawezi kukupa nasaha ila unyarafu tu.

Wawa hawa majisifu wana tabia ya kudakia mambo kivoloya. Mwanamume hawezi kumpa mwanamke nafasi angalau ayafanye mambo ya kike. Anajua kila kitu. Litaje, silitaje analijua. Mke ni wa nini ikiwa wewe ni mjuvi wa kila jambo? Kama kweli sifa unazo, mbona kuzitangaza? Kilichopo ki wazi. Kisichopo sikilazimishe!

obene.amuku@gmail.com