Nyege ni kunyegezana, kwa nini asiwe mke wako?

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, February 4  2015 at  12:02

Kwa Muhtasari

Mwanamke wa kunifanya mtu mbele ya watu kwa nini nisimpe mwili, roho na nafsi yangu? Kwa nini nisijitolee kufa kupona angalau kumfaa jinsi alivyonifaa? Kwa nini nisimfanye mke na mtu wa hadhi. Nyege ni kunyegezana.

 

PENZI tamu haliuzwi dukani wala kuchuuzwa kitandani. Thamani yake haijui sarafu wala noti; katu hainunuliki! Penzi kama halua, haijui ladha wala vilombamchuzi. Ole nyinyi wajanja mlozoea kuhonga na kuhongwa.

Wanadamu ni wajanja na mwanamume wa leo ni mjanja upeo wa ujanja! Hivyo basi tahadharini enyi goigoi, kina yakhe mnaopenda kuzoa vya bure. Makinikeni kutafuna na kula vyenu halali msije lizwa chozi kwa majuto na sononeko moyoni. Vya mwanamume wa leo, huli ukala mara mbili! Na iwapo utakula, nawe ni mliwa. Mwana kindakindaki ndiye huzoa kisonoko.

Mbona mwalalama na kulialia enyi mnaolilia wanaume? Mbegu mbovu mlizopanda harabu ya shamba! Ukweli wa mambo ni kwamba waweza kujitolea mhanga kumhonga mwanamume kwa shehena la mapenzi, tena mapenzi yaliyonoga bila kero wala bughudha, lakini kama wewe ni wa kuachwa utaachika na kilio cha mbwa mdomo juu.

Mwanamume hajakupa hata ukucha nawe huna soni kumzawadi mwili, roho na nafsi. Mwanamume hajui hata kitovu chako nawe huishi kujishaua kama ndama. Hajatangaza kusudi kukuoa nawe mtoto wa kike mwingi wa kilimilimi huna aibu kuvibeba vijiguo vyako hadi nyumba ya mtu. Akikutema kama mate jinsi wafanyavyo madume wa leo utamlilia nani?

Waweza hata kujimega kwa kisu ukampa roho yako lakini katu mwanamume wa leo haridhiki na hadiriki kula akashiba! Hana shukurani. Ukimpa hujampa yote sawa.  Ni nadra kumpata mwanamume anayejua maana na anayetambua hadhi ya upendo. Wanataka kuonja kabla kula na wakisha shiba huna chako mwana wa mtu. Ole ninyi wenye kuhonga.

Sijui wanajenga majumba ya nini? Kama sio kwenye mabaa, wanaume wa leo wako vilabuni wakinywa na kula kama fisi. Usiku kucha wako kwenye vijia vya giza wakizini na kula uroda na mahawara. Wako vijiweni wakila miraa utadhani mbuzi.

Kumhonga mwanamume wa leo ni kazi bure. Ukimtaka hayupo nyumbani. Akiwa nyumbani anashinda sebuleni hadi majogoo. Chumbani ni mwingi wa usingizi kama mzoga. Jukwaani  ni goigoi asojua mbinu wala nyenzo za mwana kumpa kumbo! Ole wewe mwana mtu mwingi wa hongo!

Wengi wetu masikini nyasi. Mwanamume jina.  Midomo ni sisi na sisi ni midomo. Matamshi ni utashi. Hatuna mbele wala nyuma. Lakini unyenyekevu uupate wapi? Kama vidonda, twavuja vinywani. Ndivyo walivyo wanaume wa leo. Ukishampa mapenzi na mwongozo akawa mtu mbele ya watu, hakumbuki tena ulikomtoa! Hakusazi kwa matusi na utashi. Hongo ya mapenzi ni ya nini ikiwa mtu hajui kukunyenyekea wala kukutumikia?

Mabwege hawa ndiyo kwanza wajeuri wasioambilika. Wakisaidiwa hawakumbuki. Wakipendwa hawamakiniki. Wakitoshelezwa hawaridhiki. Iweje wang’ang’ania kumpa mapenzi mtu mfano wa mzoga?  

Sijui kughilibu mapenzi wala kujipendekeza mbele ya mwanamke. Wala sina moyo wa huruma. Sijui katu kumsamehe na kusahau maovu ya dunia. Lakini mwanamke wa kunifanya mtu mbele ya watu kwa nini nisimpe mwili, roho na nafsi yangu? Kwa nini nisijitolee kufa kupona angalau kumfaa jinsi alivyonifaa? Kwa nini nisimfanye mke na mtu wa hadhi. Nyege ni kunyegezana.  

obene.amuku@gmail.com