Usiamshe majirani, kisa na maana umenyimwa uhondo

Na CHARLES OBEME

Imepakiwa - Wednesday, October 28  2015 at  10:58

Kwa Muhtasari

Badala ya kuzua vioja nyumbani, jamani tuvumiliane! Badala ya makeke na mateke ndani ya ndoa, tuukuzeni unyenyekevu!

 

BADALA ya kuzua vioja nyumbani, jamani tuvumiliane! Badala ya makeke na mateke ndani ya ndoa, tuukuzeni unyenyekevu!

Maisha ya mke na mume ni kama wimbi la bahari.

Yaweza kuwa tulivu na ya kufurahisha au yaweza kugeuka kimbunga chenye dhiki na bughudha.

Yote hutegemea hekima na ukomavu akilini mwa mke na mume ndani ya uhusiano.

Inampasa mwanamume kuelewa kwamba zipo nyakati za hisia kupanda na kushuka. Kuna wakati wa kununa kama kiza la alfajiri au kumwaya furaha kama mwezi mchanga.

Zipo nyakati za kutulia na za kuchacharika kama ndama. Mabadiliko hayo huathiri pakubwa uhusiano na hisia za huba.

Mwanamume kamili hana budi kuelewa na kuvumilia mkewe ili kuepuka mitafaruku na mizozano chumbani kila siku.

Kakangu, unapoamka majogoo kurai haki na mwenzio akakupuuza au akakataa na mali yake, usijenge hoja kubwa wala usiamshe majirani kwa makonde au kusonyasonya.

Hiyo siyo mara ya mwisho nyie kuamkia kitanda kimoja. Vuta kumbukumbu mara ngapi mke amekupa raha kwa ridhaa yake mwenyewe bila vituko vyako? Kwa nini uzue kasheshe kwa jambo ndogo kama hilo?

Kumbuka huba sio hewa inayompa mja uhai wala chakula kirutubishacho mwili. Mwanamume kamili anaweza kuvumilia hadi siku ya ridhaa.

Hiyo ni ishara ya upendo. Kwa nini mume ambake mke na kumkosea heshima?

Wakati mwingine, nishati za mwili hugoma kutoa cheche. Usilazimishe mambo kwa vitisho kama kwamba dunia yaisha.

Wala usimshike mwenzio koo na kumdhulumu! Hizo sio tabia za mwanamume kamili. Kumbuka, maisha ya raha ni kubembelezana.

Zipo siku mume hufika nyumbani jioni na kukumbana na makunyanzi usoni mwa mkewe huku midomo imeganda – hasemi hacheki, hasikii hahisi! Hakuna haja ya bakora, dhihaka na matusi.

Kakangu, usiharibu mambo kwa kuuliza maswali ya balagha au kutamka mambo ya kitoto. Kufanya hivyo ni kumshika bafe mkia! Vumilia na heshimu hisia za mkeo, naye atakuheshimu. Wahaka wake ukiyeyuka, mambo ni mteremko hadi asubuhi!

Kosa kubwa mno la mwanamume wa leo ni kulazimisha mambo. Mara anamshurutisha mkewe kumchangamkia wakati amezongwa na mambo yake.

Nani kasema ni lazima mke akueleze yote yanayomzonga moyoni na kumtatiza akilini? Je, akikueleza anavyojuta kuolewa nawe au anavyokuvumilia- wewe na ujinga wako, utacheka naye tena?

Vichwa vya wanawake vimesheheni makubwa, hivyo usithubutu kulazimisha ulimi wake kukutemea shubiri ya maisha!

Badala ya kuzua vita kwa sababu ya huba, tuvumiliane!

Imekuwa mazoea kwa wanaume wa leo kukasirika na kulalama hasa wanapohisi wamedhulumiwa faraghani.

Labda mke ameshindwa kutekelza wajibu wa chumbani ipasvyo. Iweje wamfanyia mwenzio dhihaka na madharau kana kwamba hujawahi kushindwa jambo maishani?

Ubinafsi na madharu sizo tajriba za mwanamume kamili! Badala ya kuzua vita kwa sababu ya huba, tuvumiliane!

 

wanamume@yahoo.com