Mnaoita wanaharamu, nani kawaharamisha?

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, August 12  2015 at  13:18

Kwa Muhtasari

Haramisheni tendo siharamisheni watoto!

 

UKIPENDEZWA na boga sibague majani yake! Lililompata mburukenge jangwani laweza kumfika mamba kidimbwini. Situmie mzigo wa mwenzio kama kiboko cha kumdhalilisha.

Mapenzi ni muamana tena ridhaa baina ya watu wenye utu wala sio watu wenye uchu. Haramisheni tendo siharamisheni watoto! Sistahimili watu wazima kuzozania malezi ya mtoto asiye na hatia.

Kweli, kupenda ni sawa na kutembea kwenye kiza totoro lisiloruhusu jicho kupenya na kuona mbele ya ncha ya pua. Mja aliyegubikwa na wingu la penzi hana uwezo kuona ukweli sisemi kutathmini hatari inayomkabili mbele. Lau wanaharamu wangalijua ubaguzi na dhuluma zinazowasubiri wasingalithubutu kuzaliwa wakiwa hai! Hata hivyo Mwenye kukupa mwana atakupa na fungu lake! 

Wenye mizigo ya malezi ya wanaharamu si haba. Nasema nao – wao hao waliojasirika kubeba misiba ya ujanani – zao la ulimbukeni kujifanya wajuaji katika dunia ya waja wepesi kula vya watu kabla kutokomea na kuwaachia zigo la malezi. Kama hujanipata wewe ni koroma vuta subira kupevuka na kuwa nazi!

Tatizo ni kwamba wanawake kwa wanaume hudanganywa tena huhadaika wakaingia kwenye uhusiano au hata kuolewa na kuoa wenzao ambao mwishowe hukataa kuwajibikia “wanaharamu!” Jambo hili lanipa uchungu wala sina nguvu kuhimili chozi. Kovu la kuumwa na joka halijanipona. Ndio maana ung’ong’o wanizulia vimbimbi mwilini.

Malofa hawa wanajifanya kupenda boga lakini kamwe hawataki kuwajibikia majani yake. Vipi? Vipi utamwoa mwanamke na mwanawe; mwishowe ukamgeukia mwana na kumdhulumu huku unatarajia mapenzi kutoka kwa mamake?

Eti kwa sababu mke amekwisha kukuzalia “wanahalali” sasa unawaona “wanaharamu” si watoto! Kweli? Zindukeni. Mapenzi utakayompa huyo mwanaharamu ndio utakayovuna wewe! Ndugu zangu, simezi mate bure. Hujaona dunia na vimbwanga vyake!

Wajua tena dhuluma wanazopata hawa watoto wanaoitwa wanaharamu – siijui nani kawaharamisha! Si vijembe si dhihaka. Si makonde si mateke. Si kubaguliwa hadharani. Si kunyimwa haki na mahitaji ya kimsingi!

 

Lazima kutoa chozi

Eti mwanaharamu hapati kitu hajakitolea chozi. 

Simdhulumu “mwanaharamu” na kumdekeza “mwanahalali!” Urefu wa mti si ugumu wa kunge. Waweza kukataa jiwe mwishowe likawa msingi kukufanya mtu mbele ya watu. Niulizeni mimi mwana mpayukaji – kakopolewa katika mapenzi ya ujanani, kazaliwa ndani ya dhiki na kulelewa kwenye vichaka vyenye miba. Sisemi kitu zaidi ya hapo!

Ndugu zangu, mabikira si haba. Jipe raha kuufungua dibaji na kulisoma buku lako wewe na wewe pekee. Hakuna haja kumpa mke vikwazo na vitisho eti kwa sababu unamwajibikia mwanaharamu wake. Dunia ni huru na mwanamume ana uhuru kumtafuta mke asiye na watoto. Lakini situmie ila kumdhulumu na kumkwaza “mwanaharamu” asiyejua mwanzo na mwisho wa mapenzi yenu.

Mungu si Athumani. Hujui na hutayajua yaliyo mbele. Simdhulumu “mwanaharamu” na kumdekeza “mwanahalali!” Urefu wa mti si ugumu wa kunge. Waweza kukataa jiwe mwishowe likawa msingi kukufanya mtu mbele ya watu. Niulizeni mimi mwana mpayukaji – kakopolewa katika mapenzi ya ujanani, kazaliwa ndani ya dhiki na kulelewa kwenye vichaka vyenye miba. Sisemi kitu zaidi ya hapo!