Ikiwa hutaki mke apendeze au apendwe basi ungeoa sokwe

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, April 20  2016 at  15:12

Kwa Muhtasari

Wewe utakuwa gumegume kama tabia yako ni kukereka na kuchukizwa moyo mwenzio akipendeza na kupendwa.

 

EWE mume, kelele za mbu zisikunyime usingizi! Kwa nini wakereka na kuchukizwa moyo mwenzio akipendeza na kupendwa? Kaka zangu, dunia hii yetu ni gala iliyojaa vitu vya kumshikisha mtu homa ya matamanio.

Ni dunia iliyorembwa kwa ustadi wa Rabana na kutonewa vitu vinavyometameta sisemi waja wa hadhi.

Mkeo kupendeza na kuwashikisha watu hamu sio kosa linalostahili kejeli, dhihaka au matusi kila siku nyumbani.

Badala ya cheche za matusi na vita vya paka kupapurana, mke mwenye kupendeza na kupendwa anastahili pongezi na zawadi kwa kuwa mtu wa nidhamu, sifa na siha nzuri na hadhi ya kipekee!

Hizo ni sifa adimu kupatikana kwa mtoto wa kike karne hii!

Wewe hujui wangapi wanaishi na magogo eti wakiwadhania wanawake!

Hatekenyeki hashikiki hata ukimguza wapi! Mlevi chakari! Mwenye shombo utadhani mvuvi! Akizungumza, heri mtoto wa kuboboja! Kwa vyovyote vile, ridhikeni tu.

Ndio maana ya mguu kuteleza na mkono kushika shonde! Paja likinyelewa halikatwi!

Vimwana wa kupendeza na kupagawisha si haba.

Wenye sura za lulu, ngozi ya sufu na upole wa mwanambuzi ni kama nyota za anga. Lakini kumpata mke……mke!

Kwa maana halisi ya mke, ni majaaliwa!

Dunia ya leo ni kama shamba la mawaridi! Acheni kila mwenye macho aridhike na urembo uliozagaa! Kwa hivyo jifunzeni hekima na heshima ya kuishi ya watu.

Nawasihi wanaume wa leo wasitishe chuki na wivu wa kitoto.

Kweli kaka zetu wa leo, wanapenda vita na matusi yasiyofaa. Kupigia watu simu mkijifanya kuwakanya, kuwatahadharisha wasijekuza uhusiano wa karibu na mkeo, ni utoto na mume mwenye tabia hizi hana budi kukomaa kichwa!

Umekwishampata mke, nani wa kukupokonya? Chako ni chako, kamwe hupokonyeki! Akizidisha kero, mpe!

Atachoka na kukubwagia zito lako! Akizaa naye, mpe mtoto! Dawa ya mwenye njaa sio kumhini chakula!

Haileti raha kila siku kero kwa mke, eti anapendeza na anapendwa na watu.

Kila siku kelele za mbu, eti mke anasifiwa mtaani. Vita haviishi nyumbani, eti mke ni mkarimu. Leo vita na huyu, kesho yule.

Jamani, mke hachagui kupendwa bali tabia zake hupendeza na kuwavuta watu karibu naye.

Bora ukaoa sokwe basi

Ikiwa hutaki mkeo kupendeza na kupendwa kwa nini hukumwoa sokwe?

Angalau akionekana mtaani, watu wanakwepa na kujificha! Wivu na utoto usikutie wazimu bure. Mkeo kusalimiwa njiani hakutamchachusha kamwe!

Mja kupendwa ni Mungu kupenda! Hiyo ni haki yake. Dunia hii imejaa wanawake viboko wenye akili za samaki!

Ukipata mmoja anayependeza, acheni dunia iridhike! Msiharibu sura zenu bure bilashi kwa makunyanzi usoni.

Tahadhari msijekufa presha kwa kujifanya kupenda ilhali tabia zenu zachukiza.

Eti siku hizi wanaume hawali wakashiba. Kila mara jekejeke la jasho, roho mkononi akihofia mke kupendwa. Hatulii nyumbani, macho katumbulia kwenye simu ya mke.

Simu inapoita tu, yeye tarishi, “wewe nani?” Upumbavu ulioje! Na wewe ni nani mwenye kufikiri mkeo ni kijitoto cha kuchungwa kama kuku mgeni? Hata ukipata mjinga wa kukuvumilia, iko siku ya siku kero zako zitamfika shingoni!

Wengine wamevuka mipaka! Mume mwenye akili timamu anachukua simu na kutusiana na mwenzake. Mara wanaandikiana arafa za matusi na kutishiana maisha.

Kisa na maana? Anamtetea mkewe! Hataki mkewe kupendwa na kutamaniwa na watu wa nje! Hizo ni akili za mende!

Wewe una mke nyumbani, haja gani kupigana na mbu wasiokukosesha hata lepe la usingizi!

Wacha wenye kutamani waridhishe macho, wewe mpe mwenzako raha! Wakija kugutuka, ua la waridi limenyauka na vikembe sebuleni. Kwa nini kufa presha bure bilashi eti wazozana na watu ilhali kichuna ni wako chumbani; kazi kwako kumchuna utakavyo!

obene.amuku@gmail.com