Kama hajatoa mahari hata sidiria asione ng’o!

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, October 7  2015 at  11:11

Kwa Muhtasari

Kama bwege halijakutolea mahari hata kanchiri halistahili kuona!

 

UKITAKA kitu cha mwenzio huna budi kuhakikisha kwamba mwenyewe yu radhi kukupa bila shaka wala shauku! Na hata ukipewa kwa hiari na huna haja nacho mbona usionyeshe uungwana na kukikataa?

Binadamu sio fisi asiyejua kukataa mzoga! Hekima ya mwanamume kamili hudhihirika pale anapokataa shinikizo za tamaa kutaka vitu ambavyo si vyake tena hajavitolea kitu! Lakini kitu gani hasa tunachozungumzia? Werevu nyie mshaanza kupinda midomo na kukonyeza nyusi! Mbona mawazo tayari mmekwisha yaelekeza kuko huko mnakopenda kufikiri hasa tunapotaja neno kitu?

Jamani wenzenu wanaumia moyoni. Kisa na maana? Vyao kuliwa bila yao ridhaa! Wanakeketeka maini kufyonzwa asali na utamu wake - kisha kuachwa masega makavu yasiotamanika wala kupendeka! Wanawake wanadhalilika kwa tabia za wanaume kupenda kuonjaonja na mwishowe kutoweka kama upepo wa kusi. Kulikoni?

 

Subira   

Mwana wa mtu amejizatiti kuhimili ujana angalau kukomaza paja sisemi kututumua bonge la kifua! Mwana mwadilifu tena mrembo wa kutamanika amekwisha kuzingua na kukuteka mawazo. Jamani mwanamume nini kinachoshikisha homa na ashiki kama beberu usije subiri angalau uchumba ukatononoka?

Subira ni tajriba ya mwanamume kamili. Haistahimiliki katu mwanamke kugeuzwa chungu cha mboga kila mpishi kuonja onja kabla hata mchuzi kukolezwa. Hizi tabia za onjaonja mwishowe humpotezea mtoto wa mtu muda sisemi kuachwa mataani akisubiri ndoa ambayo inakuwa hadithi ya paukwa pakawa! Desturi na hekima ni moja: chungu umekwisha tumbukiza ndani mkono huna budi kupakua!

Jamani watoto wa watu haya mambo mtu havutwi kwa kamba! Hata nyie wenyewe hamtaepuka lawama. Iweje mwana na hadhi zako wajisabilia mikononi mwa bwege bila akili na tafakari? Kwa kukosa stara na stahamala wajipeleka kichinjoni na kisu mkononi!

Mwanamume rafiki tu lakini mtoto wa kike hana haya kujipeleka nyumbani kwake usiku; kwapani ametundika mkoba uliosheheni chupi tu. Hajakuchumbia wala kukuposa lakini huna haya kumwachia bwege mwanya kukutambalia na kukuzinga mwili! Mtu ambaye si mumeo atafika vipi kwenye pachipachi zako? Hata woga ni kinga!

Kituo cha mtaani!

Mtoto wa kike, utaonjesha wangapi kabla kuolewa? Mwishowe unabaki kituo cha mtaani, uwanja wa mazoezi hasa! Makinikeni kudumisha hadhi ya mwanamke! Kama bwege halijakutolea mahari hata kanchiri haoni!  Ole nyinyi wepesi kupembejwa! Mtabaki na hadithi midomoni tu!

Msimamo usiodedea ni guzo tena ngao. Asikudanganye mtu kwamba mwanamume kumvulia na kumwonyesha shanga za kiunoni ndiko kuharakisha ndoa! Siku zote mwenye kuonja kutoka chunguni hana hamu kula tena!

kiamua kumpa kabla ya ndoa basi usiwe na shaka kwamba mlaji kala mara ya mwisho!

Mwenye kukupenda hana haja wala tamaa kuonja onja. Jamani wanawake wa karne hii, msikereke mnapopewa nauli kurudi kwenu usiku wa manane.  Huyo ndio mume anayekuthamini na kuheshimu hadhi ya kike! Najua vicheche walivo wepesi kukata kauli!

Mwanamume kamili huwa na kasi kuchumbia mwana wa mtu na kumposa kabla hata fikira na harakati za mwana kutiwa nakshi. Nyie ambao kwanza mnataka kuonjeshwa kabla ya posa mlizaliwa wapi? Kuonja onja kabla ya ndoa ni hatari mno. Mambo yanaweza sadifiana embe dodo likaja kuwa ngoe. Sasa ugwadu wa ngoe utaupeleka wapi?