Mabusu ya nini vijiani kwa mtu mliyeachana ujanani?

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, September 30  2015 at  20:34

Kwa Muhtasari

Kama sio kufa, wengi wenye tabia za kulamba mate yaliyotemwa wamejikuta taabani wamenaswa wakanata mitegoni.

 

MAISHA ni uamuzi. Ufanisi wa binadamu hutegemea sana maamuzi mema na maafikiano ya hekima baina ya waja. Tatizo linalotusumbua ni kwamba wapo wanaume wenye kero na tamaa; tena wepesi kukurupuka na kuchepuka kutoka kwenye ndoa wakisingizia vijisababu vya kitoto.

Tatizo sio kukurupuka, bali kurudiarudia kinyumenyume na kushiriki huba zenye kumbukizi tu hali mapenzi yalikwisha tamatika. Wenyewe wanasema mwanamume huruma! Huruma ya nini ilhali mate yalikwisha toka kinywani?

 

Ukiyatema, usiyalambe

Kama sio kufa, wengi wenye tabia za kulamba mate yaliyotemwa wamejikuta taabani wamenaswa wakanata mitegoni. Wanaume kwa wanawake wameuana! Wengine wameambukizana magonjwa ya zinaa. Wangapi wamehujumiana kwenye ndoa kwa sababu ya kuamsha hisia zilizokwisha lala? Kama yana ladha, usiyateme! Ukiyatema, katu usiyalambe! 

Mwanamume kamili ni yule mwenye msimamo na anayeweza kusimama kidete bila kudedea au kudondokwa mate. Ije mvua lije jua! Licha ya hekima zote walizojaaliwa, wanaume wa leo zumbukuku kabisa! Hawajui mbinu wala njia za kutamatisha mapenzi yaliyokwisha tamataika! Hawajui vipi kwenda mbele! Mwishowe, wanajikuta kwenye misururu ya donadona na kumbukizi tu wala hakuna chochote zaidi!

Wewe mtu na nyumba yako. Mwenzako mliachana ujanani! Mwakumbatiana nini vijiani? Mabusu ya nini kwa mtu ambaye kweli hamna chochote kilichosalia ila hekaya tu? Eti mwakumbuka mambo ya kale? Huo ni mwanzo mbaya na mwisho wake ni hujuma kwenye ndoa sisemi kufumana mishale. Isitoshe, tabia hizo za kulambalamba mate yaliyokwisha temwa ndizo zinazochochea fujo, vurugu na talaka katika ndoa za leo. Siku zote, mwanamume hawezi kuwa mjanja zaidi ya mwanamke. Mgala mwue haki mpe! Lakini mwanamume kamili anaweza kukataa kutekwa na vishawishi vya kike. Anaweza kukataa kumbukizi za mahaba ya ujanani. Anaweza kusahau kabisa joto la pachipachini enzi za ujanani.

 

Kulenga mbele

Mwanamume kamili anaweza kulenga mbele na kuyaongoza maisha yake bila kurejelea kuonja na kuonjeshwa asali ya ulimbukeni! Hiyo tu ndio ngao ya kujikinga na mishale ya werevu na wajanja wanawake wa leo. Wanawake hawasahau uchungu wa kutemwa kama mate yenye ugwadu! Hata wanapokubali kudonwa, lengo lao sio mwana kutiwa nakshi! Ni njia moja ya kulipiza kisasi. Ole nyinyi wenye tamaa! 

Kaka zangu, hamna budi kuchanuka na kuzinduka kutoka lepe hilo la usingizi. Kuna wendawazimu wengine wanaosafiri masafa ya mbali eti kujuliana hali tu na aliyekuwa mpenzi wa awali. Hata ng’ombe hajipeleki kichinjoni, seuze binadamu mwenye akili? Kama yana ladha, usiyateme! Ukiyatema, katu usiyalambe!