Mke mwema ni hekima, sio paja lichumalo hela

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, July 22  2015 at  10:14

Kwa Muhtasari

Mapenzi yamegeuzwa biashara; huba ndio bidhaa, mwanamke ni muuzaji na mwanamume ni mnunuzi.

 

NDOA sio mnara wa Babeli; kila mwenye kinywa kupaza sauti na kusema kwa raha zake! Ndoa sio soko la mnada; kila muuzaji kuchuuza kwa uwezo wa koo lake!

Ndoa ni maisha ya raha wawili kuridhiana, kupendana na kupendezana.  Nachukizwa mno nanyi wenye vijembe midomoni raha kuropoka kama nyuki mwenye usena. Mke mwema nguvu zake hekima wala sio paja lichumalo hela.

Madaraka ya kuongoza na mamlaka ya udhibiti wa familia zipo mikononi mwa mwanamume kamili. Nasema yote kwa ukakamavu tena kwa heshima ya hadhi nikitambua umuhimu wa mwanamke katika familia. Nafasi yake ni ya kipekee na jukumu lake ni maalum! Hilo halihitaji mjadala. Tatizo ni kwamba mwanamume wa leo amekwisha mzoesha mwanamke tabia zinazodunisha uchumba na kuchefua ndoa.

Zipi hasa tabia hizi? Mwanamume wa leo amezoea hasa kumhonga mwanamke ili kushawishi hisia zake na kupata anachotaka kwa njia rahisi tena za mkato. Si zawadi za thamani si ziara za kitalii si pesa taslimu si mahaba ya hadaa si ahadi za uongo. Vyote vimechangia usalata na mahaba yanayotanguliza pesa na maslahi mbele.

Kama sio hongo, mwanamume wa leo mwepesi kufidia mwanamke kwa “kazi nzuri katika jukwaa la mahaba!” Baada ya burudani mwanamume hachelei kutoa “shukrani za dhati” kama ithibati ya upendo. Tatizo hasa ni kwamba kuhongana na kufidiana kumeibua mapenzi hadaa yanayozingatia mahitaji na maslahi kuliko uhalisia na hisia.  Mapenzi yamegeuzwa biashara; huba ndio bidhaa, mwanamke ni muuzaji na mwanamume ni mnunuzi. Asiye na mikwanja aeleke baridi!

Kulikoni siku hizi? Mafunzo ya unyagoni yamepuuziliwa mbali na mambo ni huru huria. Kila mwenye mali yupo sokoni na mwenye haja yu radhi kutia guu mnadani ilmuradi mfuko unamtosheleza. Siwalaumu nyie mnaofanyia mili biashara. Mbona mtu afe njaa na mgodi kaukalia?

Utapeli huu ndio kwanza umechangia watu kuoana na kuzalishana pasipo kusudi wala lengo madhubuti. Leo wataoana kwenye magoma na harusi za kufana na kesho watatifuana kwa mapanga na magumi.

Sina kinyongo

Sina kinyongo kwenu mnaokula nyevu. Lakini niepusheni zenu fedheha na vitimbi vya ndoa za hadaa.

Asiye na hamu hawezi kuiona tamu. Lakini vitamu vi wapi katika tunu za mahaba yasiyo heba? Vilivyodhaniwa vitamu  ndivyo hivyo tunavyovinunua tena kwa mikopo ya benki. Lau sio fedha utamu wangeupata wapi wanaume wa leo?

Nyie wenye pesa sikilizeni kwa makini. Nanyi wenye mali na mili tulieni nikawajuze ya hekima. Mihogo ya kuchemsha ni tamu licha ya kuwa haina viungo wala vikolezi! Mwanzo wa tamu  ni hamu. Utamu wa uchumba upo kwenye hamu ya ndoa.  La msingi ni kuheshimiana, kuelimishana na kufaana kila hatua maishani.  Mahaba ya kulipia hayana hadhi wala ladha. Acheni ugumegume.