Kula raha kiholela kwaweza kukuachia shubiri kinywani

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, July 8  2015 at  16:53

Kwa Muhtasari

Mwanamume kamili, siku za mavuno sisahau kujenga ghala. Sisahau hekima ya kula kidogo; na kidogo kibindoni.

 

RAHA ya mwanamume ni kula jashole! Hivyo ndivyo walivyosema wazee wa jadi wenye hekima. Baada ya tangatanga juani, kila mja hufurahia kula mazao ya juhudi na matunda ya bidii yake. Na mwanamume wa leo ni mja anayependa kula vyake! Mimi sina kinyongo wala gere mtu kula vyake. Lakini ipo siku ya mume asiye na akili kula mawe!

Dunia ya leo haina uhakika na mwanamume hana uwezo kuihakiki. Kula raha kiholela kwaweza kumwachia mwanamume ladha ya shubiri kinywani. Nawe usiwe limbukeni kuuliza; vipi?

Tazama waliozama wasiibuke katika kilindi cha ufukara japo walikuwa watu miongoni mwa watu. Walikuwa navyo tena vingi usiweze kuvihesabu.

 

Kidogo kibindoni

Mwanamume kamili, siku za mavuno sisahau kujenga ghala. Sisahau hekima ya kula kidogo; na kidogo kibindoni.

Huna budi kujenga hazina thabiti na kuekeza katika miradi inayolipa. Mwanamume kamili ni ishara ya uthabiti na maisha mema kwa familia.

Hivyo basi chuma mali, hifadhi kwenye hazina ya familia na ekeza kwa manufaa ya siku za usoni. La sivyo wewe ni miongoni mwa hao watakaofanyiwa mchango wa mazishi!

Ngao ya mwanaume kamili ni nguvu za wanawe. Inasikitisha mno kuona wanaume wa leo wakila raha na mashangingi ilhali watoto waliozaliwa kwa mapenzi ya mume wanatanga wasijue nani baba nani mjomba!

Kila mwisho wa mwezi, mabaa yamejaa wanaume walio radhi kutumbuiza makahaba badala ya kuekezea watoto.

Madanguro hayaishi sura za wanaume walio mbioni kunusa na kubisha milango za pachipachi utadhani wanasaka uhai!

Nachukizwa na hali ya leo. Huku miji imejaa bashasha za wanaume wenye pesa, vijiji hakwishi vilio vya wanawake na watoto waliosononeka kwa kutelekezwa.

Hawana kitu. Si nguo si chakula si malazi si nyumba. Usidhani ni wajane na wanao! Ni mabibi ya wanaume wasiotoka kwenye mabaa. Ni familia za wanaume wanaoranda kwenye vijia vya giza wakifukuzana na makahaba.

Binadamu si makinda

Binadamu sio makinda eti watavuna kutoka shamba la mhisani. Mtoto anahitaji zaidi ya maponeo na mifupa tunayonunua angalau kuwahadaa kwayo! Mwanamume wa leo anazo nguvu za kujitosheleza. Tatizo ni ulimbukeni na utapiangono. Hatuna muda kuwakuza wanetu lakini tuna wakati wa kukesha kwenye mabaa tukiponda raha na kupapasana na makahaba! Kinaya cha maisha ya mwanamume wa leo!

Mwanamume kamili hujitahidi kula na familia wala sio kula na kulisha mashangingi!  Kula ni lazima. Lakini kula na ulishe jamaa na familia watakaomakinika kuunyanyua mwili wako baada ya kuondokewa na roho.

Usile nao kina yakhe wanaokuimbia nyimbo za hadaa kwa lengo la kuvuna masurufu kutoka kibindo ulichokitolea jasho. Angalau watoto na mke wako watavimba macho kwa kwikwi mazishi yako!