MWANAMUME KAMILI: Vichuna mlivyojiweka bahari kwa yeyote apigaye mbizi, ndoa sasa zitadumu vipi?

Na DKT CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, November 1  2017 at  06:42

Kwa Muhtasari

JINSI vipigo vya ngoma vinavyobadili mrindimo ndivyo tulivyo sisi majisifu tunaopenda kuponda wenzetu ila hatutaki kubadili ulimbukeni wetu. Hii yetu ni dunia ya kulalama na kulaumiana.

 

Wanawake wa leo wepesi kuwalaani wanaume majahili wanaopenda kula vyao na kutokomea gaizani! Lakini nadra kwao kutathmini kwa kina sababu za kuongezeka hawa walaji wa njiani.

Madume vilevile wepesi kuwalaumu vimwana ambao haja yao ni kujilimbikizia masurufu pasipo haja kujenga kiota. Awe mke ama mume, hakuna aliyeradhi kukubali kosa na kujijenga upya! Sivyo anavyofanya mwanamume kamili.

Tatizo kubwa ni kwamba hizi ndoa za kupanga zimekuwa si tukizi tena. Ndio kwanza hali ya kawaida waja wa leo kukutana vilabuni na kuamka asubuhi wakiwa mke na mume.

Uchumba ni sawia na mtihani-mwigo unaolenga kutathmini uwezo wa mtahiniwa kukabiliana na mtihani halisi.

Wachumbianao wanaweza kujipima kwenye mizani ya ungwana ili kujielewa barabara, kujirudi na kubadili mienendo na tabia ipasavyo kabla kujitoza kilindini kuogelea na nyangumi, papa na mamba wanaojifanya wanadamu katika maisha ya leo.

Kusudi la uchumba ni moja – kumwandaa mke au mumewe na kumfanya binadamu anayeweza kustahimili mapigo na mapapo kwenye ndoa! Ajabu ya leo ni kwamba hata vimwana wenyewe wanaona uchumba kama mtihani mgumu wasiotaka hata kuiga!

Isitoshe, licha ya mishikemishike ya miaka na mikaka wanaume kuvuana na wapenzi wao; watu kuvumiliana; bado hakuna afadhali katika ndoa za leo. Wanaopapurana mahakami ni wengi kuliko wanaobembelezana maabadani. Kulikoni?

Ajabu ya ndoa za leo! Ugomvi unazuka hata kabla kivumbi cha harusi kutulia. Makofi kwa makonde yanaporomoshwa watu wakiwa kwenye pilkapilka za fungate na viungo kukataa kuungama.

Mwishowe waliopendezana wakapendana wanabaki kuwa mahasidi vita kupigana na usaha kutumbuliana! Hicho ndicho kinaya cha ndoa za leo.

Sijui na sina haja kujua nani wa kulaumiwa. Nijuavyo ni kwamba wapo wanaume ambao wenyewe hawajielewi tena hawataki kujua. Wanazo akili ila hawataki kuzitumia.

Wapo vilevile wanawake wasiojali utu – mtoto wa mtu kujitunza na mali yake kutilia poda na nakshi kabla kumkabidhi mume ufunguo wa asali kugema kwa raha yake!

Maisha ya vichuna wa leo yako wazi kama lango kuu na wenyewe wako radhi kudakia uhusiano wowote kama daladala ilmuradi wamekwisha kuzinusa ishara za ukwasi! Mtoto wa mtu hana subira kupima kilindi cha moyo wa mume.

Badala yake anakuwa bahari huru huria – kila mpiga mbizi kuzama na kuibuka apendavyo! Huo ndio ujinga wa nzi kufia kidondani!

Tatizo kubwa zaidi ni kwamba vimwana wa leo ndio kwanza mahambe waliokosa hekima maishani. Mwanamume kamili si kitanda cha sufu au runinga sebuleni! Haistahimiliki kwamba mke wa karne hii anazuzukia televisheni na mazulia kwenye sebule ya mume!

Mwanamume asiyetimiza vigezo alivyoweka mke asione hata shanga kiunoni! Kufanya hivyo ndiko kuelekeza wanaume kujiweka pazuri kimadili.

Ndiko kuandaa mwanamume kamili! Ole nyinyi wenye pupa mnaokimbilia nyumbani kwa mwanamume kutafuta vitanda vya sufu! Mwisho wa siku utalalia na kulilia jamvini! Wapo wanaume wasiojua kumhurumia mke.

Tahadhari mwanamtu usijekuwa funzo kwa wengine!

Laiti wanawake wa leo wangalijua thamani ya mke wasingalichezea shilingi shimoni. Huwezi kunata kama kupe sisemi kujisabilia mikononi mwa janadume ambaye hajaonyesha lengo kukuposa.

Mwanamume hajafika kuwasabahi wazazi wako wala hana lengo kufika kwenu lakini kijanajike na mikoba begani akibandika na kubandua miguu kucha kutwa nyumbani kwa mawanamume. Ujapo temwa si wewe wa kwanza kuwalaani wanaume waovu?

Mwanamtu usijehadaika kwamba mume wa leo anatekwa kwa mapigo ya paja. Nasema hivi kwa sababu wapo vichuna wanaojua mno kuchuna ila hawana akili nyumba kustawisha! Hapo sahau kuolewa! Heri ule ukizihesabu siku! Sina kinyongo watu kula vyao.

Lakini nawaelezeni ukweli bayana!

Mwanamume wa leo nadra kukuposa mwanamtu mzoefu wa vyakula vya mikahawani! Wewe na vibanzi na vijipaja vya kuku. Badala ya mapishi nyumbani eti wewe ndiye mjuvi wa vyakula vya kufunga! Mbona usiachike? Makinika unapokwenda kumtembelea mume angalau ukabebe vitu visivyo vya kawaida mkobani – nyanya, vitunguu na dania!

Si rahisi mwanamume wa leo kumtia kapuni lakini inamjuzu mwanamke kuwa makini na kujiweka thabiti akilini angalau asijeachwa sega kavu lililokwisha tambaliwa na wagemaji! Dunia siyo yenu tena nyie vichuna mnaotafuta vya bure.
Dunia ya leo ipo mikononi mwa wanaume!

Wanaume wa leo wamekwisha kuwa hayawani, mwanamtu huna budi kujiweka thabiti! Enzi za babu kulikuwa na wanaume wangwana.

Akina sisi tusiosalia leo ni miongoni mwa watu wanaotaka vya kunyonga tu. Si wachinjaji hasa! Kila kitu tunakitia kinywani japo hatuna haja kula kushiba.

Hivyo basi ni wajibu wa mwanamke anayetaka kuolewa na kudumu kwenye ndoa kuwa makini kutambua mitihani atakayokumbana nayo katika maisha ya wanaume wa leo. Kutemwa au kuposwa ni mke kependa kupenda!


obene.amuku@gmail.com