Hebu niambieni, sababu za kuoa wake wawili ni nini hasa?

Imepakiwa Wednesday August 26 2015 | Na CHARLES OBENE

Kwa Muhtasari:

Furaha ya mke ni kumtunza ipasavyo ili kumwondolea ujuha, ushamba na utoto aliolelewa nao; angalau kumfanya mtu mbele ya watu!

WAHENGA walituonya kwamba, ari ikithiri huhasiri. Isitoshe, mshika mawili moja humponyoka!

Kwa hakika, tamaa na hamu ya uroda kwa wanaume wa leo zatufedhehesha na kutuzidishia dhiki katika familia.

Utamu wa mke sio huba na usuhuba pekee. Furaha ya mke ni kumtunza ipasavyo ili kumwondolea ujuha, ushamba na utoto aliolelewa nao; angalau kumfanya mtu mbele ya watu! Ili kutimiza lengo hilo ipasavyo, mwanamume kamili anahitaji mzigo unaobebeka. Mke mmoja pekee ni mzigo usiochukulika. Je wa pili?

Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba, kaka zetu wanaishi maisha ya sina sinani. Eti dunia haina shaka raha i mbinguni! Hawajali kifo hawaogopi mauti. Raha wanaponda na karaha kumumunya! Huo ndio ujinga wa samaki kufuata chambo! Sikutarajia kuwaona wanaume mwenye akili wakitanguliza mbele tamaa na ari ya kutaka kumiliki himaya ya wanawake. Hatima ya tamaa ni mauti

Vinywa vya waja vingali vikipovuka na mjadala kutokota. Wanaume wanateta kwamba sheria zinawadhulumu kwa kuwanyima nafasi murua ya kuoa idadi ya wanawake wanaotaka. Wanataka kuridhiwa kuoa si wawili si watatu si wanne. Maajabu hayaishi duniani. Ajabu ya wanaume kulilia kitanzi!

Sababu ya kutaka kuoa wanawake wengi ni ipi? Eti idadi ya wanawake ni maradufu ile ya wanaume. Hivyo basi sharti kila mume ajizolee wawili watatu angalau kupunguza mahambe na mashangingi wanaoranda mitaani bila madume! Eti wanataka kuwapa wanawake kazi za nyumbani ili kudhibiti vibiritingoma wanaovuruga nyumba za watu.

Wazo nzuri ila mbinu mbovu! Hiyo siyo akili ya mwanamume kamili. Ninakataa katakata, nakemea kwa nguvu zote fikira hizo potovu. Napinga mawazo hayo duni ya wanaume wa leo. Hizo ni fikira za kitoto, tena zinazoongozwa na tamaa. Kabla hujampa mwingine kazi za nyumbani, yule mmoja aliye nyumbani umemfanyaje?

Katika dunia ya leo; dunia isiyo na hali wala mali; dunia ambayo kila kitu ni ghali; mwanamume atafanyia nini wanawake wawili? Atawalisha na kuwavisha vipi? Atatoshelezaje mahitaji lukuki ya wanawake wa leo? Kaka zangu hebu nikawajuze! Mke hali akashiba chicha na jasho la gizani. Msitangulize tamaa ya kutaka majumba mengi ya uroda ilhali wenyewe ni masikini mende.

Kinaya

Nikitazama wanawake walioolewa hivi leo; naemewa kwa huzuni! Lakini mume wake yuko hai; tena anatafuta mke wa pili! Hizo ni ishara tosha kwamba wanaume wameshindwa kumtunza hata mmoja! Je, wa pili na wa tatu wataishi vipi?

Wanaishi kwa dhiki huku wakila kwa kudura za Mungu. Wanavaa mavulio, tena zilizochanika. Nyusoni ni mabonde ya chunusi, moyoni ni huzuni na mawazo tele. Ngozi imejaa vipele. Nywele ni kama chaka. Kwani hao wamaotaabika si wanawake? Wa kunyonga huwezi sembuse wa kuwinda?

Walioolewa wanasaga meno kwa mzigo mzito wa malezi.

Hawamwoni mume wa kuwapa nguvu na kuwaunga mkono. Inahuzunisha kuwaona wanawake wakitafuta vibarua vya kufua nguo au kupiga deki nyumbani kwa mabwenyenye ndipo watoto wale.

Eti lazima mke ajichuuze kwa wenye pesa ndipo wanawe wasome. Hao wanaotaabika si wajane. Dume liko hai; tena linatafuta mke wa pili! Hizo ni ishara tosha kwamba wanaume wameshindwa kumtunza hata mmoja! Je, wa pili na wa tatu wataishi vipi?

 

Share Bookmark Print

Rating