Tuwaepushe vijana kuzama katika lindi la ufuska

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, January 6  2016 at  10:31

Kwa Muhtasari

Bila kujali raha leo, karaha kesho, kila kukicha vijana wanazidi kuzama katika kilindi cha ufuska na matumizi ya dawa za kulevya.

 

HERI tuwape vijana elimu badala ya kuwatapeli kwa mahaba yasio kitu.

Vijana wa leo wako hatarini na changamoto zainazowakabili si haba! Pamoja na kutelekezwa, vijana wanayumbishwa na anasa sisemi kughilibiwa na matapeli wanaowahadaa.

Ni wajibu wa mwanamume kamili kumakinika angalau kuwapa vijana elimu badala ya kuwafilisi nafsi bure!

Ukweli ni kwamba ukahaba na ufuska unashirikisha vilevile vijana wa shule na vyuo.

Kila kukicha, vijana wanazidi kuzama katika kilindi cha ufuska na matumizi ya dawa za kulevya.

Raha leo karaha kesho. Wanawake kwa wanaume wakongwe ndio kwanza wanaendesha na kuvuruga maisha ya vijana wadogo bila huruma.

Vijitoto vivulana vidogovidogo vya akili na mili, vinagaragazana kwenye madanguro na madege, mashangingi yaliyokauka mili na mifupa.

Iweje wazee hawa kukiuka desturi, heshima na hadhi ya wazazi na kutokomeza vijitoto hivi visivyojua kitu?

Chambo 

Silaumu vijitoto hivi kwa kutojua tofauti kati ya embe bivu lenye utamu na bichi lililojaa ugwadu!

Hawana kabisa mtu wa kuwaonya na kuwakanya.

Isitoshe, wamelelewa wakiziona na kuzisoma tabia hizi potovu kutoka kwa mama na baba zao, mbona wasiwe gwiji wangali wachanga?

Pesa ndiyo chambo inayotumika hasa kuwavulia vijana na kuwatokomeza katika baharí ya anasa.

Hata samaki wana akili kuliko vijana wa leo.

Angalau samaki anaweza kukwepa mtego wa chambo.

Lakini vijana wa leo hawawezi kukwepa mtego wa shilingi.

Siwalaumu katu kupenda pesa. Ndio elimu tuliowapa.

Vijana wametelekezwa wajilishe, wajivishe na kujikidhia mahitaji wenyewe.

Kazi nazo adimu. Mbona wasizame katika ufuska?  Mtoto wa kike humvishi wala humlishi kitu.

Hawezi kuvalia matambara ilhali jibaba liko radhi kumfadhili. Hata sumu ukiwapa watakula tu!

Wa kuwakanya nani ilhali baba na mama wako mbioni kushindania ufuska pembeni.

Wazazi wamefeli katika majukumu ya kuwakuza na kupigania maslahi ya watoto.

Wasichana wanahimilika wakiavya kivoloya.

Mwana wa kike hajui hata kuhesabu siku za hedhi. Akidhurika ndipo lawama huelekezwa kwa masikini mtoto.

Baba na mamake walikuwa wapi kumpa adabu na adhabu kali kabla hajaingia masihara ya ufuska? 

Kwa kukosa ushauri, tumefanya watoto wetu kuwa vicheche wanaotoswa kulia kushoto kama magunia la viazi.

Wenyewe wanyonge wa kunyongwa na yeyote mwenye mikono.

Tungaliwapa nguvu za masomo na nasaha, nani angewaendesha kama farasi?

Tuwape elimu kabla kuwapa mahaba! Ndio wajibu wa mwanamume kamili.