Upendo ni kudumisha heshima kabla jazba

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, September 23  2015 at  16:02

Kwa Muhtasari

Lau wanaume wa leo wangaliwajibikia kukuza maadili, nani asingalikuwa na mke mwema?

 

SINA haki kuwahukumu wala sababu kuwatetea wanawake wa leo. Lakini wakati mwingine tunawalaumu na kuwasingizia makosa bila sababu wala tathmni. Lau wanaume wa leo wangaliwajibikia kukuza maadili, nani asingalikuwa na mke mwema?

Lawama na laana si dawa ya ulimbukeni! Uerevu hukita akilini sio kwa uchungu wa bakora bali kwa upendo usiopinda shingo. Mke mwema hujifunza wema kutoka kwa mumewe. Kama mwana anavyotazama kisogo cha nina ndivyo mke huerevukia vitendo vya mumewe. Sasa ni wazi kwamba wanaume wanavuna anachopanda!

Kwa vitendo vya ajabu sisemi tamaa ya kustaajabisha, wanaume wa leo ndio huchochea maovu na kuwapotosha wanawake kufanya mambo ya aibu. Tunashawishika na kujazibika kama wehu hasa tunapomwona mwanamke kaacha maungo wazi kama mende.

 

Ugumeugume

Sasa wenzenu washatambua jinsi ya kuwapagaza wazimu. Wameamua kuvua nguo za hadhi na kuvivalia hivyo vitambaa kwa raha zenu! Ole nyinyi mliodhani mwapanda mbegu za chenza; sasa mwavuma ndimu!

Mwanamume kamili hana budi kumpa mke mfano mwema! Mawaidha na nasaha zitakazomfanya mtu wa hadhi mbele ya watu, tena mke wa thamani! Ithibati ya upendo ni kudumisha nidhamu na heshima kwanza kabla kutanguliza mbele jazba.

Mume mwenye kumridhia mkewe kuvalia kama hawara bila shaka ni gumegume! Jamani, aibu kwa mtoto wa kike ni ngao! Angalau ajue nini ya kuficha na wapi pa kufichua! Lakini leo mambo mzongo! Mtoto wa mtu hana aibu kuzianika dodoki zake kwa ridhaa za mume.

Kwa nini mwanamume kumridhia mke kuvalia kijiguo kama kwamba hajui sehemu nyeti za kike zi wapi? Isitoshe, mume huna haya kumtembeza barabarani na kijiguo kilichokaa juu ya makalio mfano wa mkia wa mbuzi! Heshima hiyo kweli?

 

Kipochi pajani

Watoka nyumbani na mke kwenda kupanda gari la umma, lakini mke hawezi kuketi bila kipochi pajani! Kwa nini kuona haya ilhali ulijua wazi athari ya mavazi duni uliyovalia?

Sauti ya mwanamume kamili ni kama sheria! Analosema mume linatekelezwa kwa heshima na staha! Kama mke hajavaa nguo ya heshima na stara, hatoki nyumbani! Ndiyo hadhi ya mwanamume!

Mke mwenye kupenda kujidunisha dawa yake uwazi. Akivalia vibaya, mwambie ukweli kuliko kumficha! Lakini sivyo wanavyofanya wanaume wa leo. Kila mke anavalia anachopenda na kwenda anakotaka. Mume hasemi kitu. Isitoshe, wanashabikia kinyaa na uchi

Maumbile ya kumfaidi mumeo ndiyo sasa raha ya wapita njia! Hadhi na thamani ya mke ipi? Ndiyo sababu kuu uchumba wa siku hizi umekosa neema. Mume hajakuoa na tayari hakuna siri asojua mwilini mwa mke! Mkiachwa mataani mwasema mwaonewa!

Sifa za mnyama ni kufanya mambo bila tafakari. Sisi binadamu, mbona tabia za kinyama? Sasa hivi mijini hajulikani nani mke wa mtu wala nani mwana wa kulishwa chambo. Mavazi wanayovalia changudoa kwenye vijia vya usiku angalau kuvutia wateja ndiyo mavazi tunayoridhia mchana wa jua! Jamani tatizo nini kufikia hatua ya kugeuka hayawani na akili tunazo?

Kwa mtindo huu wa kutembea uchi mkidhani ndiyo njia za kuwafurahisha wanaume, poleni sana!