Uungwana wa mume halisi ni unyamavu na usikivu

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, September 16  2015 at  13:48

Kwa Muhtasari

Inakera mno hasa kumwona mwanamume mpayukaji mwepesi kupaza sauti na kugombana kwa vijimambo vinavyoweza kutatuliwa taratibu tena chumbani.

 

UNYAMAVU ni hekima, tena ngao kwa mwanamume kamili! Nyie mnaodhani mwanamume ni ndevu kwani hamjaziona za beberu? Nani alisema kwamba kila jambo au tofauti nyumbani lizue ubishani na vurugu?

Eti mwanamume mmoja alishikwa na kichaa na kuteketeza nyumba na mali kwa sababu mke wa kugombana naye alifunganya virago na kumwachia nyumba! Jamani tangu lini ugomvi ukawa chakula cha mja? Hizo ndizo akili za baadhi ya ndugu zetu!

Inakera mno hasa kumwona mwanamume mpayukaji mwepesi kupaza sauti na kugombana kwa vijimambo vinavyoweza kutatuliwa taratibu tena chumbani. Na sio kupaza sauti tu inayochukiza na kukera, hata vita mbele ya watoto hudunisha hadhi ya wanandoa sisemi kukoleza chuki ndani ya nyumba. Hamna budi kufikiria tena hasa nyie kina yakhe walevi wenye mazoea kugeuza nyumba ukumbi wa masumbwi!

Utamtambua mwanamume kamili kutokana na jinsi anavyojizatiti kudhibiti sio tu kinywa na ulimi bali pia hisia na fikira potovu. Heri kukejeliwa na watu lakini wasijue yaliyokuziba kinywa. Kidomodomo sio tajriba ya mwanamume kamili! Ndio maana kasuku hana uwezo wa kuoa licha ya kuwa mwingi wa maneno!

Tunasikitishwa vilevile na wanaume majisifu. Yaani kina yakhe wasiojua kufyata vinywa na kudhibiti ndimi zao. Neema ya ulimi kuzungumza lakini katika njia inayokuza heshima.

Kila kitu ndani ya nyumba lazima mwanzo ni yeye na mwisho vilevile. Wajisifu ungali mtu wa pumzi, jamani ukifa watafanya nini walio hai? Tenda mema wachia watu mwanya kuona wema na kutononoka. Sifa nzuri lakini sio sifa za kujitakia.

Mbele ya watu, ungwana wa mwanamue kamili ni unyamavu, usikivu na utulivu. Wanapozungumza wadogo kwa wakubwa, mwanamume kamili hana budi kutumia muda wake kushika mawili-matatu kati ya mengi yanayosemwa. Lakini sivyo tabia za ndugu zetu wa leo.

Kuzua kero raha yao

Kasuku hana ushindani! Wanajifanya kujua kila kitu na kila neno. Hawaambiliki hawasemezeki. La ajabu ni kwamba, ndivyo walivyo hata ndani ya nyumba. Raha yao kuzua kero na ubishani tu wala hakuna la maana linalosemwa!

Na sio mazungumzo tu yanayoudhi. Ndimi za wanaume wa leo hazijui kubaini na kubana matusi. Wanazungumza kinyaa hata mbele ya watoto. Isitoshe, wako ange kutetea hoja zao kwa ncha ya upanga.

Jamani nani anataka kuwa mke wa mwanamume asiyesikia wosia wala nasaha? Mke yupi yuko radhi kukonda mwili kwa kuzomewa na kubezwa siku zote na mwehu asiyejuakunyamaza?

Kosa kubwa analofanya mwanamume wa leo ni kujifanya kujua! Siku zote kujishaua. Kitu kidogo cha mume kumezea moyoni, dunia nzima itasikia. Akipandishwa cheo, mtu hamezi mate. Akinunua gari wapita njia walaani kwa tifuo la vumbi. Hata kutunga mimba wakunga hawali wakalala kwa vijembe na ngebe. Jamani si debe tupu ndilo litikalo?

Kuna hatari kubwa kuishi na mwanamume king’anganizi. Rahisi sana kutibua amani kwa ugomvi. Maafikiano nyumbani nadra kupatikana. Hizi ndizo sababu za wengi kuchepuka na kutafuta hifadhi na liwazo kutoka nje ya ndoa! Ikiwa mume mbishani kwa nini mwanamtu asitafute sikio la kunenea?

Hawa watu wajuvi balaa! Mwanamume mjuvi haishi shaka. Mwepesi kutunga hadithi na kubuni fikira za kitoto hasa kumsingizia mwenzake. Kila jambo analodhani kwake ndilo! Shaka za nini ndani ya ndoa ilhali mtoto wa mtu hukumwokota chakani! Isitoshe, shingo ya kuku wewe mlaji hukuipata wajua wangapi wachinjaji?