Wanaume ndio wanachochea mavazi duni ya kina dada

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, September 2  2015 at  19:10

Kwa Muhtasari

Wanaume hushawishika na kujazibika kama wehu hasa wanapowaona wanawake wameacha maungo wazi kama mende.

 

AKIPENDA mume mke hana pingamizi! Wanaume ndio chanzo cha vituko na mavazi duni tunayoyaona mitaani hasa kwa kina mama na binti zetu.

Sina haki kuwahukumu wala sababu kuwatetea lakini wakati mwingine tunawalaumu wanawake bure bilashi. Lau wamaume wangaliwajibika kukuza maadili, yote yangeepukika!

Wanaume wa leo ndio wanaopotosha na kuwasukuma wanawake kufanya mambo ya aibu, na kuvaa vijiguo vya fedheha visivyomsitiri mke! Vipi? Tunashawishika na kujazibika kama wehu hasa tunapomwona mwanamke kaacha maungo wazi kama mende. Washajua jinsi ya kuwatia wazimu. Sasa wameamua kuvua nguo za hadhi na kuvivalia hivyo vitambaa?

Mwanamume kamili hana budi kumpa mke mawaidha na mwelekeo utakaomfanya mtu wa hadhi mbele ya watu, tena mke wa thamani! Ishara ya upendo ni kudumisha nidhamu na heshima. Mwenye kukuridhia kuvalia kama hawara si mwanamume ila gumegume! Katika kufanya hili, wengi watasema kwamba wanaonewa na kudhibitiwa na wanaume. Lakini heri mwanamume anayekuonya kuliko anayekunyonyoa.

Jamani, aibu kwa mtoto wa kike ni ngao! Angalau ajue vipi vya kuficha na vipi vya kufichua! Lakini leo, wengi wanasukumwa na wanaume kuvalia mavazi wasiyojua maana. Mtoto wa mtu na dodoki zote nje. Amevalia wari si wari! Mwenyewe hawezi hata kuinama. Ndani ya gari kuketi balaa! Wakiulizwa wanasema wanavalia angalau kuwafurahisha wanaume wanaowafadhili. Isitoshe, watu wazima wananunuliwa vijiguo vya watoto wadogo.

Mbona kumridhia mke aliyevalia vibaya?

Kwa nini mwanamume kumridhia mke kuvalia kijiguo kama kwamba hajui sehemu nyeti za kike zi wapi? Isitoshe, mumewe huna haya kumtembeza barabarani na kijiguo kilichokaa juu ya makalio utadhani mkia wa mbuzi! Heshima hiyo kweli? Watoka nyumbani na mke kwenda kupanda gari la umma, lakini mke hawezi kuketi bila kipochi pajani! Kwa nini kuona haya ilhali ulijua wazi athari ya mavazi duni uliyovalia?

Sauti ya mwanamume kamili ni sheria! Ukisema umesema! Kama mke hajavaa nguo ya heshima na stara, hatoki nyumbani! Ndiyo hadhi ya mwanamume! Akivalia vibaya, mwambie ukweli kuliko kumficha! Lakini sivyo mambo ya leo. Kila mke anavalia anachopenda na kwenda anakotaka. Mume hasemi kitu.

Kaka zangu, nawapasha mpashike! Lazima wake zenu waache kuvalia nguo za chumbani barabarani. Eti kwenda na wakati? Maumbile ya kumfaidi mumeo ndiyo sasa raha ya wapita njia! Hadhi na thamani ya mke ipi? Ndiyo sababu kuu uchumba wa siku hizi umekosa neema. Mume hajakuoa na tayari hakuna siri asojua mwilini mwa mke! Mkiachwa mataani mwasema mwaonewa!