Ukarimu wetu waume umeibua sampuli ya wanawake wasiojua shukrani ni kitu gani

Na CHARLES OBENE

Imepakiwa - Wednesday, November 8  2017 at  11:39

Kwa Muhtasari

DUNIA ya leo imejaa wanaume wasiopenda kufanya la tija. Uzembe huo ndio mwanzo wa maafa kwa vizazi vijavyo! Tuyaweke wazi mambo yalivyo.

 

Mwanamume mwenye pesa ndiye mla raha! Nyie wengine ni kama mende mnaobahatisha maisha kutafuna ukavu wa mwiko!

Kwa mwanamume mwenye pesa huenda heshima na mahaba kochokocho. Nyie walalahoi hamna budi kuvumilia kulambatia vidondokavyo kidevuni.

Zindukeni nyie mnaotarajia wanawake kula na kushiba mate. Mke – hasa mke wa kisasa hana muda kumchumbia mwanamume asiyewajibikia maisha yake binafsi na ya familia yake.

Kwa kuzembea wazazi, vijana wa leo wamelazimika kuvumbua mbinu za kujikimu kimaisha. Huo ndio ukweli! Vijana wa leo wako radhi kunogesha mahaba na chochote si yeyote ilmuradi kibindo kinajazwa masurufu! Hizi tabia za mahambe sijui majahili ndizo kwanza zimechangia kuongezeka mikasa ya watoto kuzaa watoto.

Lawama kwa nani?
Ukosefu wa pesa umechangia pakubwa hali kuzorota ndani ya familia za leo. Badala ya upendo kusheheni, ndoa za leo zinasifika kwa wingi wa lawama na tetesi; vituko na vimbwanga. Kisa na maana? Pesa! Wazazi wamekuwa wakewenza wasiopatana kwa kuzozania pesa!

Nyumba zenu zinakera. Mwanamume haishi kusonya; usoni makunyanzi kama ngozi ya chatu. Mwanamke naye vijembe na ngebe.

Midomo juu kama mkusi wa jogoo. Mwana-mtu hamezi mate sisemi fundo la hewa! Jicho na sikio liko nje kuvizia zinakokwenda pesa za mumewe.

Vipi mtakuza watoto wa hadhi na heshima wanaopenda watu ikiwa nyinyi watu wazima ndio kwanza mnapenda pesa kuliko watu?

Wivu umekuwa jina la pili la mwanamke wa leo! Heri kukubali yaishe! Lakini mbona wasiwe wenye wivu? Wenye navyo wanahofia kupokonywa waume zao! Nao wanaume wa leo ndio nani? Mume wa mtu hadiriki kula vyake. Anataka kupenda na kupendwa na wanawake lukuki.

Kwa nini mkewe asiingiwe na wivu wa kitoto, angalau kutetea maslahi na haki zake? Wenyewe wanasema mume ni mali ya mke eti!

Isitoshe, mke amezoea kupewa na kupewa. Mwenyewe hajui shamba wala soko. Vyote vinampata ameketi kitako! Licha ya biashara kuzagaa wengine wamekuwa viti kushinda sebuleni tu.

Hata biashara ya kijungumeko hawataki kusikia! Wanategemea ujira wa mume angalau kujipa chakula na mavazi. Usitaje mavazi! Wanavaa nguo - sio mavulio - kama wanavyofanya wanaume wa leo.

Sasa vijanajike wameiga hizo tabia. Hawana haja kusoma wala kusomeshwa. Kwa nini mtoto wa mtu ataabike shuleni ilhali anayo macho yanayohitaji wanja sisemi uso unaohitaji poda? Heri urembo kuliko akili! Paja la mwana limezoea kudedea hewani aupate wapi muda wa kuvunja shingo maktabani? Mwana hutazama kisogo cha nina!
Tumekuwa wanaume vichwa pumba, tena mabahili wanaokesha kwenye vilabu vya walevi. Hatuna haya kunywa na kula mshahara ilhali jamaa wanashinda kumeza mate tu. Isitoshe, wanaume wa leo wako mbioni kutafuta na kuwafidia wao hao wanoshinda sebuleni.
Tatizo kubwa ni sisi wanaume tuliopotoka. Tumewazoesha kula vitamu vya tunu tena kwa ukarimu bila kuvitolea jasho. Tunawapa wanawake pesa bila hata kuitishwa. Tunawalipia kodi ya nyumba tena katika mitaa za kifahari ilhali sisi wenyewe tuko mapipani tu.
Tunawazawadia tena vya thamani na kuwafakamia hata kabla kufahamiana. Ukarimu wa mwanamume wa leo umeibua sampuli ya wanawake wasiojua shukrani. Unaweza kujitahidi kumpa kila kitu - roho, nafsi na mwili lakini katu haachi njia dhalala.

Dezo haina ghali. Lawama ni kwa mume wa leo. Tumezoea kuwalipia na kuwafidia kwa kila kitu wala hatuna haja kuwapa elimu angalau wakachuma vyao! Mbona kuwalaumu wanapotetea haki yako!

Dunia hii yetu haina haki. Eti dume la mtu limakinike na ukuli juani. Halafu mwenzake ale ashibe na asiposhiba anaweza kutoa vitisho vya talaka au hata kumpa mumewe kichapo cha ujinga! Ndiyo mapenzi hayo!

Hivyo ndivyo mlivyotaka nyie wanaume mliozoea kuwapa mashangingi pesa kama fidia baada ya kuwafanyia upuzi huo mnaoita mapenzi!

Mwanamume wa leo kukosa mali anaitwa gumegume. Akiwa na mali ndiye mume! Mimi sijamlipa mtu kabla kuona jasho mwilini. Sitaki kujua jasho kutokana na shughuli zipi, lakini nataka kuona jasho! Huo ndio upendo!


obene.amuku@gmail.com