Ana familia na anasisitiza kuwa anataka kunioa

Na SHANGAZI

Imepakiwa - Tuesday, January 16  2018 at  14:46

Kwa Muhtasari

Mwanamume mwenye mke na watoto watatu anataka kuanzisha rasmi mipango ya kunioa; nifanyeje?

 

SHANGAZI AKUJIBU

Ana familia na anasisitiza kuwa anataka kunioa

SHANGAZI nina umri wa miaka 24 na kuna mwanamume anayenipenda sana nami pia nampenda. Tatizo ni kwamba ana mke na watoto watatu. Anataka sana kunioa na hivi sasa anasisitiza twende kwa wazazi ili aanzishe mipango ya ndoa. Nitafanya nini na sitaki kumuacha?

Kupitia SMS

Inaonekana umeamua kuolewa mke wa pili kwani unajua mwanamume huyo ana familia na unasema hutaki kumuacha. Hata hivyo, kabla hamjaanza hiyo mipango ya ndoa ni muhimu ashauriane na mke wake ili ajue msimamo wako kuhusu suala hilo. Itakuwa kazi bure kwako kuolewa kisha upelekwe katika boma ambako hutakuwa na amani kwa sababu ya pingamizi za mke-mwenza.

Namtaka aliyekuwa mwalimu wangu ingawa ana mke

Shikamoo shangazi. Kuna mwanaume aliyekuwa mwalimu wangu ambaye namtamani ingawa tayari ameoa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ashakum si matusi lakini naona wewe umekosa adabu. Kama mwanaume huyo alikuwa mwalimu wako unafaa kumheshimu kwa sababu ni sawa na mzazi wako kwani alikulea kimasomo. Isitoshe, huyo sasa ni mume wa mwenyewe. Wanaume wamo tele duniani, tafuta wako.

Pasta ni mume wa mtu ila amekodisha nyumba tuishi naye

Shangazi hujambo? Nina mwanaume ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka minne sasa hata nimezaa naye mtoto mmoja. Hata hivyo, yeye ni mume wa mtu tena ni mhubiri wa kanisa ambako ninaabudu. Sasa amekodisha nyumba tuishi naye. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ni jambo la ajabu tena lenye aibu kwamba umekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mume wa mwenyewe tena mhubiri wako. Je, hayo ndiyo maadili ya maisha anayowapa katika kanisa lake. Yeye pia ni mhubiri feki na mnafiki kwani vitendo vyake ni kinyume kabisa na maadili ya kidini. Unayofanya ni makosa makubwa na kama kweli unahitaji ushauri wangu basi nakwambia umkome kabisa mwanaume huyo kwani ni mume wa mwenyewe na unahatarisha ndoa yake.

Kumbe safari zake ni za kuona mwingine!

Shikamoo shangazi. Nimekuwa na mpenzi kwa miezi miwili sasa na nimekuwa nikimpa chochote anachotaka. Amekuwa akisafiri mara kwa mara akisema anamtembelea shangazi yake lakini nimegundua amekuwa akienda kwa mwanaume mwingine. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Sasa umejua kwa hakika kuwa msichana huyo si mwaminifu kwako kama kweli amekuwa akimtembelea mwanaume mwingine na kukuhadaa kuwa anaenda kwa shangazi yake. Utaamua mwenyewe kama utaendeleza uhusiano na mtu asiye mwaminifu kwako.

Ninaishi na virusi na nahitaji mwenzangu tuanzishe familia

Shangazi pokea salamu zangu. Mimi ninaishi na virusi vya Ukimwi na sijaoa ingawa nimehitimu umri wa kuwa na mke. Sasa nakuomba unitafutie mwanamke aliye katika hali sawa na yangu kiafya ili nimuoe kwani ninaamini ninaweza kuwa na familia. Sitajali hata kama atakuwa na mtoto. Mungu akujalie uzidi kutushauri.

Kupitia SMS

Ni jambo la kutia moyo kwamba umekubali hali yako hiyo na unaamini kuwa unaweza kuishi maisha ya kawaida ukipata mwenzako. Ninaamini kuna wanawake walio katika hali na mipango sawa na yako maishani. Hata hivyo, sina uwezo wa kukutafutia kwani mke au mume huwa chaguo la mtu binafsi. Isitoshe, kazi yangu katika ukumbi huu ni kutoa ushauri tu. Ni matumaini yangu kuwa walio katika hali hiyo watasoma ujumbe wako huu na atakayevutiwa kuwasiliana nawe. Kila la heri.

Marafiki wanishauri nimuache mume

Kwako shangazi. Nina mume na tumejaliwa watoto wawili. Tatizo ni kuwa mume wangu hana kazi wala hashughuliki kutafuta. Sasa wanawake marafiki zangu wananishauri kwamba nimuache. Waonaje?

Kupitia SMS

Ni wajibu wa mwanamume mwenye nyumba kukimu familia yake na ninashangaa kwamba mume wako hashughuliki kutafuta kazi. Ingawa hujasema, ninaamini kuwa maisha ni magumu kwako na watoto wenu. Kama una hakika kuwa ukimuacha utaweza kuishi maisha nafuu au bora, ni heri ufanye hivyo.

Kama unalo swali lolote unalohitaji ushauri, tuma kwa nambari ya simu ya 21603 ukianza na neno SHANGAZI. Kila ujumbe unagharimu Sh10. Pia unaweza kutuma barua pepe kwa: taifa@ke.nationmedia.com / swahilihub@ke.nationmedia.com