Marafiki wa mpenzi wanamchochea aniache

Na SHANGAZI

Imepakiwa - Saturday, January 20  2018 at  18:03

Kwa Muhtasari

Mpenzi wangu amebadili ghafla mipango yetu ya ndoa baada ya kushauriwa na marafiki zake atafute mwanamume mwenye kazi nzuri kwa sababu mimi ni kibarua tu; nishauri.

 

SHANGAZI AKUJIBU

Marafiki wa mpenzi wanamchochea aniache

VIPI shangazi? Mpenzi wangu amebadili ghafla mipango yetu ya ndoa, sasa hanitaki tena. Kisa ni kwamba ameshauriwa na marafiki zake atafute mwanamume mwenye kazi nzuri kwa sababu mimi ni kibarua tu. Nampenda sana, sijui nifanye nini. Nishauri.

Kupitia SMS

Sielewi sababu ya mwenzako kubadili nia yake ghafla kama kweli anakupenda kwa dhati. Inaonekana yeye pia amekuwa katika uhusiano huo shingo upande kwani ana haki ya kujiamulia anachotaka maishani hata bila kushawishiwa na marafiki. Kama ameshamua kukuacha itabidi ukubali uamuzi wake.

Maisha ya ndoa ni sawa na jehanamu!

SHANGAZI nimeoa lakini wakati mwingine hujuta kwamba nilioa mke niliye naye. Sababu ni kwamba ni msumbufu sana, sina amani kabisa nyumbani ni kama kwamba naishi jehanamu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni kweli ndoa inaweza kugeuka jehanamu inapokuwa yenye mateso na dhuluma. Wakati mwingine ni vyema kwa wahusika kukabili ukweli kwamba hawawezi kuishi pamoja na kuachana roho safi. Mwelezee mke wako unavyohisi na pia umshauri kuhusu talaka.

Bila shaka ananitaka

KWAKO shangazi. Kuna mrembo ambaye amenasa moyo wangu na inaonekana yeye pia ana hisia kwangu kwani tunapokutana hunichangamkia sana utadhani tumejuana kwa muda mrefu. Nishauri.

Kupitia SMS

Tunaambiwa kuwa mapenzi ni kikohozi hayafichiki. Kutokana na maelezo yako ni wazi kuwa umeona dalili za mwenzako kuvutiwa kwako kimahaba. Hatua unayofaa kuchukua sasa ni kumdokezea hisia zako ili naye apate nafasi ya kuungama iwapo anahisi vivyo hivyo.

Nahofia dada yangu atatumiwa atemwe

MAMBO shangazi. Nimegundua kuwa dada yangu ameshikana na mwanamume ambaye ninajua ana msururu wa wasichana na nina hakika anataka kumtumia tu. Nahofia kumwambia kwani sijui kama atanisikiza ama atasema ninaingilia maisha yake binafsi. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Sidhani ungependa kuacha dada yako aendelee kutumiwa vibaya na mtu ambaye unajua kwa hakika hana mienendo mizuri. Ni muhimu umwambie ili aweze kufanya uamuzi wake kuliko ukose kumwambia kisha uje kujuta baadaye akifikwa na mabaya.

Ameahidi kumuacha mkewe kisha anioe

SHIKAMOO shangazi. Nimekuwa na uhusiano na mwanamume ambaye ameoa. Amekuwa akiniambia hana raha katika ndoa yake na anapanga kumtaliki mkewe kisha anioe. Hata hivyo, nimechunguza na sioni dalili zao kuachana kwani wanaishi tu kwa furaha. Nishauri.

Kupitia SMS

Mwanamume huyo ni muongo na anataka tu muendelee na uhusiano wa kando kwa manufaa yake. Kama kweli hana furaha katika ndoa yake angekuwa ameanzisha utaratibu wa talaka. Usikubali kuendelea kutumiwa kwa ahadi zisizo na msingi.

Nilikosea kutoboa siri ya mume wa rafiki?

KWAKO shangazi. Nina rafiki yangu ambaye mumewe amekuwa akitembea na wanawake wengine mtaani ingawa yeye hajui. Juzi nilimfumania katika maskani ya burudani na nikampigia simu rafiki yangu kumwambia. Alikuja wakagombana sana na tangu hapo ananichukia sana nahofia anaweza kunidhuru. Je, nilikosea?

Kupitia SMS

Hata kama mwanamke huyo ni rafiki yako, nahisi ulikiuka mipaka kwa kitendo chako hicho kwani hata unaweza kuwafanya wavunje ndoa yako. Kuna usemi kuwa pilipili usiyoila haifai kukuwasha. Ndoa ni jambo la kibinafsi kati ya wahusika na ni makosa kwa watu wengine kuingilia.

Naogopa tutaoana kisha mkewe arudi

KUNA mwanaume tunayependana na tumekubaliana atanioa. Lakini nimesikia alikuwa na mke na wakaachana. Sasa naogopa huenda mke wake akarudi na kunipata kwake. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Badala ya kutegemea habari za kuambiwa, ni muhimu umuulize mwanaume mwenyewe. Kama kweli alikuwa na mke, thibitisha kutoka kwake na ikiwezekana kutoka kwa jamaa na marafiki zake kwamba wameachana kabisa na hakuna matumaini kwao kurudiana.