Mke tuliyeachana amenitenganisha na watoto

Imepakiwa Wednesday January 31 2018 | Na SHANGAZI

Kwa Muhtasari:

Tuliachana na sasa amenikataza kuwaona au kuwasiliana na watoto tuliozaa pamoja; nifanyeje?

SHANGAZI AKUJIBU

Mke tuliyeachana amenitenganisha na watoto

KWAKO shangazi. Nilikuwa nimeoa lakini mke wangu akaniacha kwa sababu ya fitina za majirani. Alirudi kwao na huko akaolewa na mwanaume mwingine. Hata hivyo, waliachana majuzi sasa yuko kwao. Tatizo ni kuwa amenikataza kuwaona au kuwasiliana na watoto tuliozaa pamoja. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kama ameachana na mwanamume aliyemuoa na sasa yuko kwao, hana sababu ya kukuzuia kuwaona au kuwasiliana na watoto wenu kwa sababu hiyo ni haki yako. Ushauri wangu ni kuwa utumie utaratibu wa kisheria kupitia mahakamani ili upate rasmi ruhusa ya kuwaona watoto wako.

Hataki kuniambia SMS ni za nani

NINA umri wa miaka 27 na mimi ni mwanafunzi wa chuo kikuu. Nina mpenzi ninayempenda sana. Hata hivyo, nimekuwa nikiona SMS za kimapenzi katika simu yake kutoka kwa mwanamke mwingine na nikimuuliza haniambii chochote cha maana. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Maelezo yako yana maana kwamba mwenzako ana mpenzi mwingine wa pembeni lakini hajakubali wala kukataa. Kuna uwezekano mkubwa kwamba ana mwingine na ndiyo maana anakosa cha kukuambia kwani anajua akikuambia ukweli utakasirika na kumuacha. Badala ya kuendelea kuwa gizani, ni heri ujiondoe katika uhusiano huu.

Nilimtoa mbali sana, sasa amenitema

HUJAMBO shangazi? Kuna mwanaume tuliyependana miaka miwili iliyopita akiwa bado chuo kikuu ingawa mimi ninafanya kazi. Nimekuwa nikimsaidia kwa mahitaji yake ya kifedha hadi akamaliza masomo na akapata kazi. Ajabu ni kuwa punde tu baada ya kupata kazi aliniacha akashikana na mwanamke mwingine. Ninajuta sana kwa muda na pesa zangu ambazo nilitumia kwa ajili yake. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ni ajabu kwamba mwanamume uliyemsaidia alipokuwa na haja ameamua kulipa hisani yako kwa kukutema kimadharau kwa sababu ya mwanamke mwingine. Ushauri wangu ni kwamba usijute. Badala yake, jaribu juu chini umsahau, utapata mwingine.

Anitafuta na tayari nishapata mwingine

SALAMU shangazi. Mpenzi wangu niliyekuwa nimempa moyo wangu wote alikatiza mawasiliano ghafla bila sababu na akabadilisha namba yake ya simu. Nafikiri alipata mwingine na hakutaka kuniambia ukweli. Mwezi uliopita nilishtuka aliponipigia simu baada ya miaka mitatu akidai eti bado ananipenda ilhali nimeshapata mwingine. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Uamuzi wako utategemea ni nani unayempenda zaidi kati yake na uliye naye sasa. Kama utamchagua yeye, hakikisha amekupa sababu za kutosha za kutoweka na kupuuza simu zako kwa miaka yote hiyo. Labda unavyosema ni kweli kwamba alikuwa amepata mwingine na huenda wamekosana na ndiyo maana ameamua kurudi kwako.

Asali ya pembeni imenitia kichaa

NIMEOLEWA kwa miaka miwili na nina mtoto mmoja. Hata hivyo nimeshindwa kumuacha mpenzi wangu wa awali na tumekuwa tukikutana na kufanya mambo yetu pembeni. Ninajua kwamba mume wangu akigundua nitakuwa mashakani lakini mahaba ninayopata kutoka kwa mwanaume huyo siwezi kuyapata kwingine na sidhani ninaweza kumuacha. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Sielewi ni kwa nini ulimuacha mpenzi wako wa awali kama kweli ndiye anayekupa mahaba unayostahili. Pili, ni vyema kwamba unacheza na moto ukijua unaweza kukuchoma. Utajua kuwa huo ni mchezo hatari pale mume wako atakapojua kuhusu vituko vyako ama utakapopimwa uambiwe una Ukimwi. Shauri yako!

Nitaacha masomo ili niolewe?

HUJAMBO shangazi? Nina umri wa miaka 22 na ninasomea udaktari katika chuo kikuu. Mpenzi wangu ni daktari na tayari anafanya kazi. Sasa anataka tuoane lakini mimi naogopa kwani bado ninasoma. Nimeshindwa kuamua na ndiyo sababu nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni vyema kuwa unatambua umuhimu wa masomo yako yakilinganishwa na uhusiano wa kimapenzi. Ninaamini hofu yako ni kuwa ndoa itaathiri kwa kiwango fulani umakinifu wako katika masomo. Hiyo ni kweli. Ushauri wangu ni kuwa umwelezee mpenzi wako wasiwasi wako na umsihi akupe muda umalize masomo ndipo muanze maisha pamoja. Kama anakupenda atakubali. Akikataa, itabidi uamue lililo muhimu kwako kati ya masomo na ndoa kisha ukate kauli.

Kama unalo swali lolote unalohitaji ushauri, tuma kwa nambari ya simu ya 21603 ukianza na neno SHANGAZI. Kila ujumbe unagharimu Sh10. Pia unaweza kutuma barua pepe kwa: taifa@ke.nationmedia.com / swahilihub@ke.nationmedia.com

Share Bookmark Print

Rating