Mke wangu ametoroka na rafiki yangu wa mtaani

Imepakiwa Tuesday February 6 2018 | Na SHANGAZI

Kwa Muhtasari:

Mwanamke ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka miwili alihama ghafla mtaani bila kuniambia na mwanamume rafiki yangu pia amehama na nimechunguza nikagundua wameenda kuishi pamoja; nifanyeje?

SHANGAZI AKUJIBU

Mke wangu ametoroka na rafiki yangu wa mtaani

HUJAMBO shangazi? Mwanamke ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka miwili alihama ghafla mtaani bila kuniambia. Mwanamume rafiki yangu pia amehama na nimechunguza nikagundua wameenda kuishi pamoja. Sikujua kuwa wamekuwa na uhusiano hata mwanamke huyo ana mimba ya mwanaume huyo! Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kutokana na maelezo yako, ni wazi kuwa mwanamke huyo amekuwa akikudanganya kuwa ni wako huku akimgawia asali rafiki yako. Hatua yake ya kushikana na rafiki yako huyo na kupata mimba yake ni ishara kamili kuwa amemchagua yeye na hana haja nawe. Huo ni uamuzi wake na huwezi kumlazimisha akurudie. Kubali na uendelee na maisha yako.

Alinihadaa nikaenda shamba, sasa ameoa

HUJAMBO shangazi? Nimeolewa na ninampenda sana mume wangu. Mwaka uliopita alinidanganya niende kwetu na mtoto wetu na akaahidi kuja kunichukua. Lakini baada ya wiki mbili alinipigia simu akaniambia ameoa mke mwingine. Sijarudi kwake na pia ameacha kugharamia mahitaji ya mtoto. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ni wazi kwamba mume wako aliamua kuchukua njia ya mkato kukutaliki. Ni jambo ambalo amekuwa akipanga na hatimaye amefaulu kwa sababu sasa uko kwa wazazi wako naye ameoa mke mwingine. Ingawa amekuacha, unaweza kumpeleka kortini ili alazimishwe kugharamia malezi ya mtoto wenu.

Aliniambia hajaoa ila tetesi zasema kaoa

KWAKO shangazi. Nina umri wa miaka 21 na kuna mwanaume tunayependana sana. Tulipokutana mara ya kwanza nilimuuliza iwapo ameoa akaniambia hajaoa. Hata hivyo, hivi majuzi mtu fulani aliniambia ameoa na nilipomuuliza tena akakana kabisa. Sasa nimechanganyikiwa, sijui ni nani anayesema ukweli. Nishauri.

Kupitia SMS

Kutokana na maelezo yako, mpenzi wako amekwambia mara mbili sasa kuwa hajaoa na unafaa kumwamini hadi utakapothibitisha habari za aliyekwambia kuwa ameoa. Jinsi pekee ya kujua ukweli ni kwenda kwao nyumbani na kuwauliza jamaa zake. Ikiwezekana, fanya hivyo.

Baada ya kunitusi eti nina sura mbaya, ananiomba msamaha

SHIKAMOO shangazi! Mwanaume ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka miwili tuligombana majuzi na akanitusi akisema mimi ni sura mbaya hata hajui amekuwa akitafuta nini kwangu. Nilimpenda kwa moyo wangu wote na matamshi yake hayo yaliniuma sana moyoni na nikajiambia kuwa sitawahi kuongea naye tena maishani. Siku mbili baadaye nilishangaa aliponipigia simu kuomba msamaha eti matamshi yake yalitokana na hasira. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Mtu anaweza kusema chochote anapokuwa na hasira. Kama mwenyewe ndiye aliyeomba uhusiano huo na kuungama kuwa anakupenda haiwezekani kwamba umegeuka kuwa sura mbaya baada yenu kukosana. Isitoshe, amekuomba msamaha na kukwambia hayo yalitokana na hasira. Jaribu kumuelewa.

Ninapenda burudani hadi siridhiki hata na mume mmoja

HUJAMBO shangazi? Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 28 na sina mpenzi kwa sasa. Sababu ya kukosa mpenzi ni kuwa ninapenda sana burudani na kila ninapokuwa na uhusiano huwa siridhiki inabidi nitafute pembeni na nikigunduliwa ninatemwa. Je, nina kasoro?

Kupitia SMS

Siwezi kuita tabia yako hiyo kasoro kwa sababu watu wameumbwa kwa namna tofauti na labda hayo ndiyo maumbile yako. Hata hivyo ni tabia mbaya kuweka mbele mambo hayo katika uhusiano. Kuna tofauti kubwa kati ya mapenzi ya dhati na tamaa.

Mume mpenzi wangu haamini ni yeye tu

HUJAMBO shangazi? Nina mpenzi ninayempenda kwa dhati. Ninaishi mbali naye na amekuwa akinishuku kuwa nina wanaume wengine. Nimemhakikishia kuwa ni yeye tu lakini hataki kuniamini. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Sijui mwenzako anataka umwambie nini tena kama umemhakikishia huna mwingine ni yeye tu na hataki kuelewa. Mwambie kama hakuamini ahamie unakoishi ili thibitishe mwenyewe.

Kama unalo swali lolote unalohitaji ushauri, tuma kwa nambari ya simu ya 21603 ukianza na neno SHANGAZI. Kila ujumbe unagharimu Sh10. Pia unaweza kutuma barua pepe kwa: taifa@ke.nationmedia.com / swahilihub@ke.nationmedia.com

Share Bookmark Print

Rating