Mpenzi wa awali anatishia uhusiano wangu mpya

Na SHANGAZI

Imepakiwa - Saturday, December 30  2017 at  13:03

Kwa Muhtasari

Niliyemuacha ameanza kumpigia simu mpenzi wangu akidai bado ananipenda na atafanya juu chini kunipata; nishauri.

 

SHANGAZI AKUJIBU

Mpenzi wa awali anatishia uhusiano wangu mpya

VIPI shangazi? Nilimuacha mpenzi wangu nilipogundua alikuwa akinicheza na wanaume wengine. Nilipata mwingine tunayependana sana na sasa tunapanga ndoa. Lakini niliyemuacha ameanza kumpigia simu mpenzi wangu akidai bado ananipenda na atafanya juu chini kunipata. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni makosa kwa mpenzi wako wa zamani kuanza kuingilia uhusiano wenu ilhali mliachana tena kutokana na tabia zake mbovu. Ingawa hujasema alitoa wapi nambari ya simu ya mpenzi wako, itabidi umtafute umkanye viklali akome kuwaingilia. Akikataa mchukulie hatua za kisheria ili akomeshwe.

Simuelewi mpenzi wangu, mara hii ana furaha kisha hasira!

SHIKAMOO shangazi! Kuna msichana anayedai ananipenda lakini ni kigeugeu kama kinyonga, kwani leo utapata ana furaha tele, kesho ana hasira za mkizi ambazo sijui kiini chake. Hali yake hiyo inanitia wasiwasi. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ni vigumu kuishi na mtu usiyeweza kuelewa au kutabiri hisia zake kama huyo mpenzi wako. Itakuwa vyema umwelezee unavyohisi kuhusu hali yake hiyo uone kama atajirekebisha. Asipobadilika utaamua iwapo unataka kuendelea naye ama mtaachana.

Anataka nimuoe mke wa pili na alinikataa wakati nilimtaka

HUJAMBO shangazi? Mwanamke niliyetaka tuwe wapenzi alinikataa na nikaoa mwingine. Juzi nilikutana naye akaniambia amegundua ni mimi tu anayependa na anajuta ni kwa nini alinikataa. Sasa anataka nimuoe mke wa pili. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Nashangaa unahangaika kuhusu mwanamke huyo ilhali wakati ulimtaka alikukataa. Pili, hujui amekuwa wapi kwa miaka yote hiyo; labda ameponda raha na wanaume hadi amekosa wa kumuoa na sasa ameamua wewe ndiye mwokozi wake. Ningekuwa wewe singepoteza wakati wangu kwake. Utaamua mwenyewe.

Ninajuta nilimtusi kwa kumshuku

SHANGAZI nilimkosea mpenzi wangu kwa kumtusi nilipompata nyumbani kwake na mwanamume wanayesoma pamoja chuo kikuu na nikadhani wana uhusiano wa kimapenzi. Nimechunguza na kugundua hakuna chochote kati yao. Nimemuomba msamaha lakini amekataa na hata amekatiza mawasiliano. Nampenda sana na sitaki kumpoteza. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Kuna usemi kuwa hasira ni hasara. Ulifanya makosa makubwa kumtusi mpenzi wako kwa kumpata na mwanamume mwingine na kuamua kwamba ni wapenzi. Wakati mwingine utajifunza kudhibiti hisia zako. Inaonekana kitendo chako kilimkasirisha mpenzi wako na ndiyo maana amekatiza mawasiliano. Mpe muda labda hasira zikitulia atakubali kuzungumza. Inawezekana pia ameamua huo ndio mwisho wa uhusiano wenu.

Nahofia kijana huyu atateka hisia zangu

Nimeolewa na ninampenda mume wangu. Hata hivyo, kuna kijana tunayefanya kazi pamoja ambaye ananitaka na ninaamini ana mapenzi ya dhati kwangu. Nahisi kwamba muda si mrefu atanasa hisia zangu na sitaki kumkosea mume wangu. Nitamuepuka vipi?

Kupitia SMS

Kama hujui, ninakufahamisha kwamba hata kama umeolewa utaendelea kukutana na wanaume wanaokutaka. Wewe ni mke wa mtu na ni lazima uwe na msimamo katika maisha yako ya ndoa. Hata kama kijana huyo anakupenda kwa dhati, huwezi kuolewa na wanaume wawili kwa wakati mmoja. Njia pekee ya kumuepuka ni kuacha kumpa nafasi ya kuendelea kuelezea hisia zake kwako.

Maneno na vitendo vyake havionyeshi kuwa ananipenda

SHIKAMOO shangazi! Nina uhusiano na mwanaume fulani lakini ninashuku penzi lake kwangu. Sababu ni kuwa maneno na vitendo vyake havitoshi kuthibitisha penzi lake kwangu. Nahisi kama ninajipendekeza kwake kwa sababu hata mara nyingi ni mimi ninayempigia simu. Nishauri.

Kupitia SMS

Kama wewe ni mtu mzima, unaweza kujua iwapo mwanamume anakupenda kweli au anakuchezea akili. Jihadhari naye kwa sababu kuna wanaume wenye tabia ya kuwahadaa wanawake kwa lengo la kuwatumia tu. Ni muhimu ujue kwa hakika kuwa anakupenda. Hakuna haja ya kuishi na mtu asiyekupenda.

Kama unalo swali lolote unalohitaji ushauri, tuma kwa nambari ya simu ya 21603 ukianza na neno SHANGAZI. Kila ujumbe unagharimu Sh10. Pia unaweza kutuma barua pepe kwa: taifa@ke.nationmedia.com / swahilihub@ke.nationmedia.com