Mtoto amekataa kabisa kutoka chumbani mwetu

Imepakiwa Tuesday January 23 2018 | Na SHANGAZI

Kwa Muhtasari:

Tabia ya mtoto inatunyima raha zetu chumbani ingawa mama yake haonekani kujali; nifanye nini?

SHANGAZI AKUJIBU

Mtoto amekataa kabisa kutoka chumbani mwetu

HUJAMBO shangazi? Nimeoa na mtoto wetu wa kwanza ni msichana ambaye sasa ana umri wa miaka mitano. Tatizo ni kuwa amekataa kabisa kutoka katika chumba chetu cha kulala ingawa ana chumba chake. Tabia yake hiyo inatunyima raha zetu chumbani ingawa mama yake haonekani kujali. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ingawa bado ni mtoto, binti yenu, katika umri wake huo, hafai kuwa akilala katika chumba chenu. Wewe na mke wako mna wajibu wa kumfunza kulala katika chumba chake. Kulingana na maelezo yako, ni kama kwamba mke wako hajaathiriwa na jambo hilo. Ni vyema uketi chini naye mlizungumzie na kupata suluhisho.

Najaribu kurekebisha mienendo ya mke wangu ila hanielewi

SHANGAZI mimi nimeoa na nimeishi na mke wangu kwa miaka miwili sasa. Lakini naona ameanza vinjia vingi na nikijaribu kumrekebisha hanielewi kabisa. Nampenda sana na sijui nitafanya nini.

Kupitia SMS

Sielewi unamaanisha nini ukisema mke wako ameanza vinjia vingi. Kama ni tabia ambazo unahisi zinaweza kuathiri vibaya ndoa yenu, basi mwelezee wazi awache ili kulinda ndoa yenu. Akishindwa kujirekebisha utaamua iwapo utaendelea kumvumilia ama mtakubaliana kuachana.

Nimechoshwa na tabia ya wazazi wa mke kuniomba pesa

SALAAM aleikum shangazi. Mimi nina mke na tumejaliwa mtoto mmoja. Tatizo ni kwamba wazazi wa mke wangu wananikosesha amani katika ndoa yangu kwa tabia yao na kuniombaomba pesa. Mara nyingi wanazonipigia simu huwa wanataka pesa tu. Nawaheshimu kama wakwe zangu lakini tabia yao hiyo inaniudhi. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ninaamini kuwa umekuwa ukimlipia mke wako mahari kuambatana na makubaliano kati yako na wazazi wake. Kama ndivyo, tabia ya wakwe si nzuri na hata inaweza kusababisha migongano kati yako na mke wako. Kama mke wako ana hisia sawa na zako kuhusu wazazi wake, unaweza kumtuma ashauriane nao kuhusu suala hilo

Niko tayari kumuoa lakini nahisi kama ana wengine kando

SHANGAZI nina umri wa miaka 23 na kuna msichana ambaye niko tayari kumuoa. Hata hivyo naona ni kama ana uhusiano na wanaume wengine kwa sababu hajawa akinionyesha mapenzi ya dhati. Je, nimuache ama nifanye nini?

Kupitia SMS

Sielewi unamaanisha nini ukisema hajawa akikuonyesha mapenzi ya dhati. Pili, inaonekana unadhania tu wala huna hakika ana uhusiano na wanaume wengine. Badala ya kukaa kimya tu huku ukimshuku, ni heri uketi chini naye mjadili suala hilo ili ujue hasa msimamo wake.

Nahofia mjakazi atapindua serikali ya mwajiri wake

KWAKO shangazi. Nimeoa na mke wangu alipata mtoto wa kwanza hivi majuzi na ikabidi aajiri mjakazi ili kumsaidia kwa kazi za nyumbani. Tatizo ni kuwa ameajiri msichana aliyekomaa na mrembo hata kumshinda. Mgeni asiyemjua mke wangu akija nyumbani kwetu atadhani mjakazi ndiye mwenye nyumba. Nahofia akiendelea kuishi kwetu nitamkosea mke wangu na sitaki. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kupitia kwa maelezo yako, umefichua udhaifu wako ambao labda mke wako haujui – kwamba wewe ni mwanaume mnyonge kwa wanawake warembo. Huo ni udhaifu mbaya, kwani, mbali na mjakazi wenu huyo, unaweza pia kunaswa kwa haraka na mwanamke mwingine yeyote mrembo, wakiwemo majirani zenu. Kwa hivyo, kumfukuza kijakazi wenu si dawa. Suluhisho ni wewe urekebishe mtazamo wako kwa kukubali kuwa umeoa na kuheshimu ndoa yako.

Ni makosa kuwa na uhusiano ilhali wazazi ni marafiki?

HUJAMBO shangazi? Nimekuwa na uhusiano na kijana tunayeishi mitaa jirani. Sasa nimegundua kuwa baba yake na baba yangu ni marafiki wakubwa. Je, kuna makosa tukiwa wapenzi?

Kupitia SMS

Urafiki wa wazazi wenu hauwezi kuathiri kwa vyovyote uhusiano wenu wa kimapenzi. Badala yake, urafiki wao unafaa kuchochea zaidi uhusiano wenu kwa sababu wakati ukifika kwenu kufunga ndoa haitakuwa vigumu kwa kila mmoja wenu kumtambulisha mwenzake kwa baba yake kwa sababu tayari wanajuana.

Share Bookmark Print

Rating