Ameungama kuwa hanipendi eti alinihurumia tu!

Na SHANGAZI

Imepakiwa - Friday, December 29  2017 at  08:34

Kwa Muhtasari

Nilipomuuliza msichana ninayempenda juzi alikiri kuwa hanipendi na eti alinikubali kwa kunihurumia tu; nifanyeje?

 

SHANGAZI AKUJIBU

Ameungama kuwa hanipendi eti alinihurumia tu!

HUJAMBO shangazi? Kuna msichana ambaye tumekuwa na uhusiano kwa miezi kadhaa sasa na nimekuwa nikishuku penzi lake kwangu kwani haonekani kufurahia. Niliamua kumuuliza juzi na akakiri kuwa hanipendi eti alinikubali kwa kunihurumia tu. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ninaamini sasa umeondoa dukuduku moyoni kuhusu hisia za msichana huyo kwako. Uhusiano usiokuwa na mapenzi kutoka pande zote mbili hauwezi kuendelea kwa hivyo itabidi ujiondoe katika uhusiano huo ili utafute mwingine anayekupenda.

Anataka nigharamie mtoto na nilimuacha kwa kutembea nje

KWAKO shangazi. Nilikuwa na mke na tukazaa mtoto lakini tukaachana. Miezi kadhaa iliyopita niligundua ana uhusiano wa kimapenzi na mwanaume fulani na kwa sababu hiyo nikaacha kugharamia malezi ya mtoto. Sasa anatishia kunipeleka kortini. Je, hiyo ni haki?

Kupitia SMS

Kama hamjatalikiana rasmi na hajaolewa na mwanamume mwingine, huyo bado ni mke wako na ana haki ya kudai kutoka kwako gharama ya malezi ya mtoto wenu. Huyo aliye naye ni mpenzi tu wala si mumewe. Ni heri uendeleze tu jukumu hilo badala ya kuanza kuvutana kortini.

Mama yangu hataki niolewe kwa kuhofia nitamuachia upweke

SHIKAMOO shangazi! Nina umri wa miaka 28 na bado sijaolewa na wala sina mpenzi. Mama yangu hajaolewa na mimi ndiye mtoto wake wa pekee. Natamani sana kuolewa lakini mama yangu amekuwa akipinga akisema nikiolewa nitamuachia upweke. Mbali na kuwa mimi ni binti yake, sisi ni marafiki wakubwa sana na ninaelewa hisia zake. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Inaonekana kuwa mama yako anajali maisha yake kuliko yako katika ushauri wake huo. Hali kwamba hakuolewa haina maana kuwa wewe pia hufai kuolewa. Ninaamini alikuwa na sababu nzuri ya kutoolewa. Ni haki yako kuchagua kuolewa au kutoolewa na hafai kukuamulia jambo hilo ambalo ni muhimu sana katika maisha yako.

Nimekuwa na mkosi wa kupata wanaume wasio waaminifu

KWAKO shangazi. Mimi sijui nina mkosi gani! Nilimuacha mwanamume mpenzi wangu mwaka uliopita nilipogundua alikuwa na wengine wawili. Nimepata mwingine majuzi, naye pia nimegundua ana mwingine. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Sidhani una mkosi; hiyo ni bahati mbaya tu. Jamii yetu imejaa walaghai wa kimapenzi na si wanaume tu bali pia wanawake. Si jambo rahisi kumpata mpenzi mwaminifu; kwa hivyo itabidi uwe na subira unapoendelea kutafuta. Habari njema ni kwamba badi kuna watu waaminifu.

Tumekuwa pamoja miaka miwili na bado haamini nampenda

SHIKAMOO shangazi! Nina mpenzi wa dhati na ninaamini ndiye atakuwa mume wangu baadaye maishani. Tatizo ni kuwa bado anashuku penzi langu kwake ilhali huu ni mwaka wa pili wa uhusiano wetu na nimemhakikishia mara nyingi kuwa ndiye chaguo la moyo wangu. Anasema ataamini ninampenda siku tutakayofunga ndoa. Nifanyeje ili aniamini?

Kupitia SMS

Hali kwamba mpenzi wako anasubiri kwa hamu siku mtakayofunga ndoa ni ishara kamili kuwa anakupenda kwa dhati kwa hivyo usione vibaya. Unachohitaji kufanya ni kuendelea kumhakikishia kuwa yeye ndiye chaguo lako hadi siku hiyo itakapowadia ili ashuhudie ndoto yake ikitimia.

Ni mwaka mmoja tangu tuachane na bado sijamsahau

KWAKO shangazi. Kuna mwanamke tuliyekuwa wapenzi lakini uhusiano wetu ukavunjika karibu mwaka mmoja uliopita. Tatizo ni kuwa nimeshindwa kumsahau na hali hiyo imenifanya hata nishindwe kutafuta mpenzi mwingine. Nifanyeje kumuondoa moyoni ili niweze kuendelea na maisha yangu?

Kupitia SMS

Ni jambo la kawaida kwa uhusiano kuvunjika ingawa mara nyingi huacha mhusika au wahusika wote na majeraha moyoni. Hatua ya kwanza ya kuondoa mawazo kuhusu mpenzi mliyeachana ni kukubali kuwa uhusiano umevujika. Pili, ni kuchukua hatua ya kutafuta uhusiano mpya.

Kama unalo swali lolote unalohitaji ushauri, tuma kwa nambari ya simu ya 21603 ukianza na neno SHANGAZI. Kila ujumbe unagharimu Sh10. Pia unaweza kutuma barua pepe kwa: taifa@ke.nationmedia.com / swahilihub@ke.nationmedia.com