Tabia yake ya kuniomba pesa yanifanya nimshuku

Na SHANGAZI AKUJIBU

Imepakiwa - Thursday, December 28  2017 at  10:21

Kwa Muhtasari

Shangazi nina mwanamke mpenzi lakini mahitaji yake ya pesa yameanza kunishinda.

 

SHANGAZI AKUJIBU

Tabia yake ya kuniomba pesa yanifanya nimshuku

SHANGAZI nina mwanamke mpenzi lakini mahitaji yake ya pesa yameanza kunishinda.

Sababu ni kuwa wiki haimaliziki kabla hajaniomba pesa na ninapokosa anakasirika. Ninampenda lakini nimeanza kushuku kuwa labda hanipendi na nia yake ni kuninyonya pesa tu. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Ni vizuri kuwa umefungua macho na kung’amua kuwa huyo unayemuita mpenzi wako hana haja nawe ila anafuata pesa zako tu. Uhusiano unaolenga mambo mengine mbali na mapenzi hauwezi kudumu kwa hivyo ushauri wangu ni kuwa ujiondoe mapema la sivyo mwanamke huyo atakutafuna hadi utembee bila nguo.

Mpenzi aliniacha akaolewa na sasa anataka turudiane

SHIKAMOO shangazi! Kuna msichana tuliyekuwa wapenzi kwa miaka mitatu lakini akaniacha na kuolewa na mwanamume mwingine. Sasa anataka turudiane na hisia zangu kwake bado zipo. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Mapenzi yanaweza kumfanya mtu zuzu na kipofu akose kufikiria wala kuona. Ingawa unasema bado unampenda msichana huyo, ni muhimu kwanza utafute ni kitu gani kilichomfanya akuache na ni kwa nini sasa ameamua kumuacha huyo mwingine. Huenda kuna jambo fulani ambalo si sawa kwake na ni muhimu utahadhari usije ukajitafutia balaa.

Nahofia nimepima nyama iliyooza

HUJAMBO shangazi? Ni miezi miwili sasa tangu niingie katika uhusiano na mwanamke ambaye nampenda kwa moyo wangu wote. Sasa nimeanza kusikia fununu kutoka kwa watu kwamba hana msimamo amekuwa na msururu wa wanaume, wakichovya na kuhepa. Nifanyaje?

Kupitia SMS

Uamuzi wako utategemea tu ushahidi ulionao kuhusu mienendo ya mwanamke huyo. Huwezi kutegemea fununu kwa sababu zinaweza kuwa za kweli ama za uongo. Jipe muda umchunguze mwenyewe kimya kimya umjue vizuri ili ufanye uchukue hatua inayofaa. Inawezekana wanaoeneza uvumi huo wanaonea wivu uhusiano wenu.

Anataka mtoto nami bado niko shuleni

SHIKAMOO shangazi! Nimependana na kijana mwanafunzi wa chuo kikuu na mimi ninasoma shule ya upili. Amekuwa akitaka tuzae na sijui nitafanya nini kwa sababu sitaki kuacha masomo. Nishauri.

Kupitia SMS

Utafanya makosa makubwa kuzaa na kijana huyo kwani hajakuoa tena ni mwanafunzi kama wewe tu hana uwezo wa kugharamia malezi ya mtoto. Pili, masomo ni muhimu sana kwa maisha yako ya baadaye na huna budi kuyazingatia.

Alinifuata siku nyingi, kukubali akatoweka

KUNA mwanamume aliyenitaka kwa muda mrefu na hatimaye nilikubali tuwe na uhusiano. Lakini tangu siku niliyomkubali ametoweka kabisa sijamuona wala hajawasiliana nami. Inawezekana kuwa alinihadaa?

Kupitia SMS

Kama ni yeye mwenyewe aliyekuwa akikutafuta na sasa humuoni licha ya kumkubali, inawezekana amebadili nia yake kwako. Ushauri wangu ni kuwa usishughulike kumtafuta la sivyo ataona kama unajipendekeza kwake. Kama kweli anakupenda atakufuata yeye.

Mrembo atanifanya nimkosee rafiki

VIPI shangazi? Kuna msichana anayenipenda ingawa ninajua ana uhusiano na rafiki yangu. Mimi pia nampenda lakini sitaki kuvunja uhusiano wao na pia urafiki wangu na kijana huyo. Nishauri.

Kupitia SMS

Ingawa msichana huyo anakutaka na wewe pia unampenda, ni muhimu kuweka jambo hilo wazi usije ukamkosea rafiki yako. Mwambie mpange mkutane nyinyi watatu ili atangaze msimamo wake ili ujiondolee lawama kutoka kwa rafiki yako.

Nisaidie kumpata

SHANGAZI naomba usaidizi wako katika ukumbi huu. Kuna msichana tuliyesoma pamoja shule ya upili miaka kadhaa iliyopita na tangu tulipomaliza sijamuona tena. Nimejaribu kumtafuta lakini sijafaulu. Utanisaidia vipi?

Kupitia SMS

Sina namna ya kukusaidia kwani simjui wala sina nambari yake ya simu. Ninaamini bado unakumbuka jina lake kwa hivyo nakushauri unitumie ili tulichapishe hapa kwa matumaini kuwa akisoma ujumbe huo atawasiliana nawe.

Kama unalo swali lolote unalohitaji ushauri, tuma kwa nambari ya simu ya 21603 ukianza na neno SHANGAZI. Kila ujumbe unagharimu Sh10. Pia unaweza kutuma barua pepe kwa: taifa@ke.nationmedia.com / swahilihub@ke.nationmedia.com