Tuna mtoto na wazazi hawajui kuhusu ndoa yetu

Na SHANGAZI

Imepakiwa - Wednesday, December 27  2017 at  12:25

Kwa Muhtasari

Mimi na mpenzi wangu tulishindwa kuvumilia hadi tuoane na tukaanza kuishi pamoja.

 

SHANGAZI AKUJIBU

Tuna mtoto na wazazi hawajui kuhusu ndoa yetu

HUJAMBO shangazi? Mimi na mpenzi wangu tulishindwa kuvumilia hadi tuoane na tukaanza kuishi pamoja. Sasa nimechanganyikiwa kwani tayari tumezaa mtoto mmoja na hata wazazi wetu hawajui kuhusu uhusiano wetu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ulifanya makosa kuanza kuishi na mpenzi wako kama kwamba ni mke wako na wazazi wake wakijua hawatafurahia. Ushauri wangu ni kuwa uwaelezee wazazi wako kuhusu hali hiyo kisha mwende kwa wazazi wa mpenzi wako kuhalalisha uhusiano wenu.

Mpenzi amenishtua kuniambia eti ana mimba ya mwingine

VIPI shangazi? Mwanamke mpenzi wangu amenishangaza kuniambia kuwa amekuwa na uhusiano na mwanaume mwingine na sasa ana mimba yake. Ameniomba msamaha akidai eti hajui alivyoingia katika uhusiano huo na anajuta. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Mwanamke huyo ni muongo anakudanganya. Je, aliingia katika uhusiano mwingine akiwa usingizini hajijui, hajisikii na sasa amezinduka akapata ana mimba? Ninahisi amekuwa akiwapima ili achague mmoja kati yenu na aliyempa mimba amemtema, wewe sasa ndiye tegemeo lake. Tafakari hayo kisha uamue.

Ameniacha akidai amekuwa akiota nikiwa na wengine

SHIKAMOO shangazi! Mwanamume mpenzi wangu ameamua kuniacha akidai ameota mara kadhaa akinifumania na wanaume wengine. Anaamini kuwa hizo ni dalili kwamba nina wapenzi wa pembeni. Ukweli ni kuwa mimi sina mwingine ila yeye tu tena nampenda sana. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ni jambo la kushangaza kwa mtu kufanya maamuzi kwa kuongozwa na ndoto. Madai yake hayo hayana msingi kwani ndoto na hali halisi ni mambo tofauti kabisa. Inawezekana kuwa madai yake hayo ni kisingizio tu cha kukuacha kwa hivyo achana naye.

Uhusiano wa mume na kijakazi nyumbani unanitia wasiwasi

HUJAMBO shangazi? Ninashuku kwamba mfanyakazi wangu wa nyumbani ana uhusiano na mume wangu. Sababu ni kuwa naona wamezoeana sana na nimewapata mara kadhaa nyumbani wameketi wakipiga gumzo utadhani ni mtu na mkewe. Hali hiyo inanitia wasiwasi. Nishauri.

Kupitia SMS

Si jambo la kawaida kwa mwanamume mwenye nyumba kuwa na mazoea na mfanyakazi wa nyumbani kwa hivyo una sababu ya kuwa na wasiwasi. Ninaamini wewe ndiye unayeajiri wafanyakazi wa nyumbani kwenu kwa hivyo una uwezo wa kumwachisha kazi mfanyakazi huyo kama unahisi amekuwa tishio kwa ndoa yako.

Nashindwa kuelewa ni kwa nini mpenzi ameniacha ghafla

SHIKAMOO shangazi. Kijana ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka mitatu sasa amenigeuka ghafla akashikana na msichana mwingine. Nimekuwa nikitaka kukutana naye nimuulize sababu yake kunitendea hivyo lakini hapatikani kwa simu nadhani amebadilisha namba. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ninaelewa maumivu ya moyoni ambayo kijana huyo amekuachia kutokana na kitendo chake. Hata hivyo, usikose usingizi kwani hiyo ni hali ya maisha na imewapata watu wengi si wewe tu. Huyo sio mwanamume pekee duaniani; kuna wengine wengi tena bora kumshinda. Jaribu kumuondoa katika mawazo yako na ufungue moyo wako kwa uhusiano mpya.

Ananidharau kwa kuweka picha za warembo Facebook

VIPI shangazi? Nimeamua kumtema mwanaume mpenzi wangu kwa sababu nimegundua ananichezea na wasichana wengine pembeni. Amekuwa akiweka picha za wanawake tofauti katika ukurasa wake wa Facebook na nikimuuliza anadai eti ni marafiki tu. Ajabu ni kuwa mimi ni mpenzi wake na hajawahi kuweka picha yangu hapo. Nishauri.

Kupitia SMS

Usifanye pupa ya kuvunja uhusiano wenu kwa kumshuku tu mwenzako bila kuwa na hakika kwamba wanawake anaoweka picha zao katika Facebook ni wapenzi wake. Kama mwenyewe amekwambia ni marafiki, huna sababu ya kumshuku. Mwamini kwa sasa hadi utakapothibitisha.

Kama unalo swali lolote unalohitaji ushauri, tuma kwa nambari ya simu ya 21603 ukianza na neno SHANGAZI. Kila ujumbe unagharimu Sh10. Pia unaweza kutuma barua pepe kwa: taifa@ke.nationmedia.com / swahilihub@ke.nationmedia.com