SEHEMU YA TATU YA USASA USASAMBU

Na WILLIAM HIMU

Imepakiwa - Monday, June 11  2018 at  08:04

Kwa Muhtasari

Kwa kiasi fulani suala la utandawazi limekuwa na matokeo hasi kwa watoto wetu wa kike na kusababisha kuwaathiri kimwili na kiakili.

 

UTANGULIZI

SUALA la utandawazi limekuwa ni jambo ambalo hatuwezi kuliepuka katika maisha yetu ya kila siku. Hata hivyo, suala hili limekuwa na matokeo hasi kwa watoto wetu wa kike na kusababisha kuwaathiri kimwili na kiakili. Kuingia kwa utandawazi kumewafanya vijana watumie muda wao mwingi kwenye mitandao ya kijamii na intaneti ambako wanajifunza mambo mengi ya ovyo. Utandawazi una faida nyingi katika maendeleo ya binadamu kijamii, kisiasa na pia kiuchumi ila kwa nchi nyingi za ulimwengu wa tatu utandawazi umekuwa ni kaa la moto kwani kila anayejaribu kulishika lazima limuunguze. Kwa kuona hayo yote mwandishi wa tamthiliya hii ameamua kuifungua macho jamii ili iweze kuchukua hatamu kuwanusuru watoto hasa wa kike.

 

Inaendelea sehemu ya Tatu

 

Mama Mwanaharusi: Kwa nini?

Mama Mwanaharusi: (Anatania) Naona pazia limekushinda kushona.

Mama MwaNaharusi: Heee heeeee, umeona hili tu! Kabla sijakujibu lolote soma yale maneno kwenye fremu ya dirisha.

Mama Mwanawima: (Anasoma kwa sauti ya chini) Mgeni wangu karibu lakini uyaonayo na uyasikiayo yaache humu humu (Wote wanacheka.)

Mama Mwanaharusi: Aaaah ila mambo mengi shoga yangu, hapa kuna nguo nyingi za watu zinanisubiri.

Mama Mwanawima:  Mwanamke kazi na kujituma. Kuzaliwa masikini sio kosa, kosa ni kufa masikini.

Mama Wwanaharusi: Kweli ila hizi kazi zina changamoto, watu wengine wana visa utadhani ni waganga wa kienyeji

Mama Mwanawima: Changamoto gani tena? Kama hela si unapata?

Mama Mwanaharusi:   Hakuna kitu kinaniudhi kama mtu kuniletea nguo ambayo haijafuliwa, yaani unakuta nguo

imevunda, inanuka jasho kama mzoga lakini mtu hajali anataka umshonee.

Mama Mwanaharusi: Ubinadamu kazi shoga yangu, jamani nimekuja kumuulizia mwanangu hajarudi nyumbani mpaka saa hizi.  Sio kawaida yake! (Anaangalia saa yake.)

Mwanaharusi: Mimi leo sikuwa nao, hata nyumbani nimerudi mwenyewe ila skuli nilimuona yupo na Mwanakombo.

Mama Mwanaharusi: Mwanakombo huyu huyu au?

Mwanaharusi: Ndio huyu na Mwanahawa…

Mama Mwanawima: Mimi sitaki kabisa mazoea na ile familia.

Mama Mwanaharusi: Jambo la kushukuru ni kuwa tumeshajua aliko hivyo ni vyema ukamwangalie huko.

Mama Mwanawima: Haya jamani mimi ngoja niende huko kwa Mwanahawa.

(Anatoka mbio mbio kuelekea nyumbani. Kwa upande mwingine Mwanawima naye anakazana kurudi kwa mama yake anamuona kwa mbali akiagana na wanamume, anajibanza uchochoroni na kumuacha atangulie nyumbani… mama Mwanawima hasira zimempanda, anasononeka na kujilaumu kumsomesha mwanaye.)

Mama Mwanawima: (Anaongea mwenyewe) Afadhali hela zangu ningenunua vitenge kuliko kuhangaika namsomesha halafu anafanya ujinga.

(Anamuacha mwanaye atangulie kisha naye anamfuata nyuma nyuma anafika na kumkuta Mwanawima akiwa amelala.)

Mama Mwanawima: Wewe Mwanawima! Mwanawima niambie ulikuwa wapi?

Mwanawima:Nilikuwa skuli mama, nimerudi muda mrefu tu sijakukuta.

Mama Mwanawima:Mwendawazimu mkubwa wewe, usinifanye sina akili!

Mwanawima: (Kimya anainamisha kichwa chini.)

Mama Mwanawima: Hii ni aibu mwanangu, wale vijana uliokuwa nao ni kina nani?

Mwanawima: (Kimya anaona aibu hata kuinua kichwa chake.)

Mama Mwanawima: Usidhani kuna kijana anayekupenda pale, wote hohe hahe tu.

Mwanawima: Nisamehe mama…

Mama Mwanawima: Baba yako si unamjua vizuri lakini! Lazima nimwambie akunyooshe, siwezi kuvumilia huu uchafu.

Mwanawima: Hapana mama, naomba usimwambie baba.

(Analia na kuomba msamaha.)

Mama Mwanawima: Katika siku ambazo umeniudhi leo umeniudhi sana, nakuonea huruma jinsi baba yako atakavyokupiga.

Mwanawima: Nisamehe mama sirudii tena.

Mama Mwanawima: (Hasira zinaongezeka, anavua kiatu chake na kumpiga nacho kwa hasira) Haya rudia tena sasa.

(Mwanakombo naye anafika nyumbani kwao akiwa kachoka hoi, anaingia ndani kwao anakuta wazazi wake wanaangalia runinga, anawasalimia.)

Mwanakombo:  Shikamoo (Baba na mama wanaitikia) Marahabaa.

Mwanahawa: Ulikuwa wapi mpaka muda huu… Unajiona

umekua eee!

Mwanakombo: Hapana leo tulichelewa kutoka, mwalimu alisema tubaki.

Mwanahawa: Wewe jifanye umeota mapembe tu…

Mwinyikheri: Aaaah, muache apumzike kwanza.

Mwanahawa: Mimi hapo ndio nakosana na wewe mume wangu, huyu mtoto akiharibikiwa aibu itakuwa kwetu sote.

Mwinyikheri: Mtoto haombewi mabaya, futa hiyo kauli yako…

Mwanahawa: Haya, mimi yangu macho…

(Mwanaharusi anarudi kutoka skuli.  Akiwa njiani, Mwanawima anamwachia simu aongee na Dulla kisha wanatawanyika kila mmoja kwao. Mwanaharusi pamoja na uvumilivu wa kutotumia simu alishawishiwa akaanza kuongea na Dulla kwa shingo upande. Anafika nyumbani mbio mbio, anaingia ndani haraka haraka na kutoka nje huku mifuko ya sketi yake ikiwa imevimba kama tumbo la chura, mama yake anamuangalia kwa makini…)