Sababu ya kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia sekondari na vyuo

Na JENITHA WALTER, Mhariri Msanifishaji wa Swahilihub

Imepakiwa - Thursday, April 5  2018 at  11:38

Kwa Muhtasari

Wataalamu nchini Tanzania sasa wameshauri walimu wa masomo ya fizikia, biolojia, kemia, hisabati, jiografia, uraia na historia kutafsiri maarifa ya masomo hayo yaliyopo kwa lugha ya Kiingereza na kuyaandika kwa lugha ya Kiswahili.

 

TANGU enzi za Wakoloni lugha ya kufundishia elimu ya sekondari na vyuo ni lugha ya Kiingereza.

Kulizuka mgogoro mkubwa baina ya wanazuoni juu ya lugha ipi kati ya Kiingereza au Kiswahili inafaa kufundisha sekondari na vyuo. Wanazuoni waliotetea lugha ya Kiingereza madai yao yalijikita zaidi kuiponda lugha ya Kiswahili kuwa haina misamiati na istilahi za kutosha kutokana na istilahi nyingi hususan za masomo ya sayansi na maarifa mengi kuandikwa kwa lugha ya Kiingereza hivyo Kiingereza ni lugha bora ya kufundishia.

Lugha ni sehemu ya utamaduni. Lugha hutumika kuelezea utamaduni wa jamii husika. Wanazuoni waliotetea lugha ya Kiswahili, hoja zao zilijikita katika kuhimiza uzalendo na kupinga ukoloni, kudumisha umoja na kuongeza kiwango cha ufaulu kwani elimu ya kikoloni ilijikita katika kupunguza idadi ya wanafunzi kadri kiwango cha elimu kilivyopanda (umbo la piramidi).

“Kimya kingi kina mshindo” wahenga walisema na “ukiona kobe kainama ujue anatunga sheria”.

Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Saam (UDSM)) kwa kimya cha muda mrefu wameamua kujibu mashambulizi ya mgogoro huo kwa vitendo. Wamewatumia walimu wa masomo ya fizikia, biolojia, kemia, hisabati, jiografia, uraia na historia kutafsiri maarifa ya masomo hayo yaliyopo kwa lugha ya Kiingereza na kuyaandika kwa lugha ya Kiswahili.

Miswada ya vitabu hivyo imechapishwa na kuwasilishwa kwenye Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni mchango na msisitizo wa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Mrisho Kikwete juu ya matumizi ya Kiswahili katika sekta za umma.

 

SABABU ZA KUTUMIA KISWAHILI KUFUNDIA ELIMU YA SEKONDARI NA VYUO

Sababu zipo nyingi ikiwa ni pamoja hizi zilizojadiliwa kama ifuatavyo:-

Kuongeza kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi

Wanafunzi wengi wanashindwa kufanya vizuri katika mitihani yao kwa sababu ya lugha ya Kiingereza. Baadhi ya maarifa wanayo kutoka shule ya msingi lakini wanashindwa kuyatumia maarifa hayo kutokana na kushindwa kutumia lugha ya Kiingereza. Sekondari ni mwendelezo wa shule ya msingi hivyo kutumia lugha ya Kiswahili kufundishia kutaongeza kiwango cha ufaulu maradufu.

Tunapaswa kujua kwamba kujua Kiingereza sio kujua maarifa. Kuna baadhi ya shule binafsi wanasoma watoto wa Kizungu wanaoongea Kiingereza mfululizo lakini wanashindwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao. Kujua lugha ya Kiingereza sio kujua maarifa. Tunatakiwa tujiamini na kukithamini Kiswahili chetu kufundishia ili kukuza kiwango cha ufaulu.

 

Kuongeza hali ya kupenda kujisomea

Kwa kuwa vitabu vya masomo yote vitakuwa vimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili, wanafunzi watapenda kujisomea kwani hawatatumia nguvu nyingi kuelewa au kuhangaika kutafuta watu wa kuwasaidia kutafsiri kilichoandikwa.

 

Mchango chanya kwa wanajamii katika ujifunzaji

Kiswahili ni lugha ya Taifa na lugha ya mawasiliano miongoni mwa wanajamii. Wanajamii wana mchango chanya kutoa maarifa waliyo nayo kuwafundisha wanafunzi. Kwa mfano; kKuna baadhi ya wazazi wanawasomesha watoto wao shule binafsi lakini wao hawajui Kiingereza. Wanashindwa kuwafundisha na kuwasaidia kufanya kazi za nyumbani kwa kuwa wanafundishwa kwa Kiingereza. Kama mtoto anafundishwa kwa lugha ya Kiswahili ni rahisi kwa wazazi au walezi  kumfundisha na kumsaidia mtoto kitaaluma.

 

Wanafunzi kuelewa kwa urahisi

Mwanafunzi akifundishwa kwa lugha ya Kiswahili ataelewa kwa urahisi kwani mwalimu atakuwa anafundisha na kutoa mifano halisi iliyopo katika mazingira halisi kwa kuwa lugha ni sehemu ya utamaduni. Kuelewa huambatana na kumbukumbu. Mwanafunzi atakumbuka alivyofundishwa na kusababisha kufaulu vizuri kwenye masomo yake.

 

Mwanafunzi kuwa na mawanda mapana katika kujieleza

Kwenye maswali ya insha mwanafunzi atakuwa na mawanda mapana ya kueleza na kuchambua mambo kwa undani kwa kuwa anatumia lugha yake ya Kiswahili anayoifahamu vizuri pamoja na kuelewa kwa undani maarifa aliyopatiwa na mwalimu. Mara nyingi kwa kufundishia lugha ya Kiingereza wanafunzi wanashindwa kujieleza hivyo alama zitapungua katika insha.

 

MCHANGO HASI WA LUGHA YA KIINGEREZA

Kiwango kidogo cha umilisi wa lugha ya Kiingereza kwa walimu

Walimu wengi wa shule za sekondari wana maarifa mazuri ya masomo wanayofundisha ila hawana umilisi mzuri wa lugha ya Kiingereza. Kutumia lugha ya Kiingereza kufundishia imesababisha wanafunzi kukariri na siyo kuelewa. Utamkuta mwalimu anafundisha somo la Jiografia ila anafafanua maarifa hayo kwa lugha ya Kiswahili. Lugha ni chombo cha kuwasilisha maarifa, hivyo mwalimu akitumia lugha ya Kiswahili kufundishia kwanza atakuwa huru kufundisha maarifa aliyokuwa nayo. Pili, wanafunzi wataelewa zaidi kuliko kukariri kwa lugha ya Kiingereza.