http://www.swahilihub.com/image/view/-/4392590/medRes/1938408/-/j5oqtyz/-/maina.jpg

 

Lugha ya Kiswahili katika magazeti

Stephen Maina

Bw Stephen Maina. Picha/MAKTABA 

Na STEPHEN MAINA, Swahilihub

Imepakiwa - Friday, May 4  2018 at  14:54

Kwa Muhtasari

Napenda kuwafahamisha wasomaji kuwa ili kurekebisha makosa ni muhimu tushirikiane kutoa elimu na hamasa.

 

BAADHI ya wasomaji wa magazeti ya Kiswahili hivi karibuni wamenikumbusha kuhusu umuhimu wa kuzingatia lugha sanifu katika kuandika magazetini au kutangaza kwenye redio na runinga.

Hali hii imetokana na makosa mengi yanayojitokeza magazetini na ambayo yanawakera wasomaji ambao ni wakereketwa wa lugha ya Kiswahili.

Napenda kuwafahamisha wasomaji hawa kuwa ili kurekebisha makosa haya ni muhimu nao pia tushirikiane kutoa elimu na hamasa kwa wenzao kuhusu tunu hii ambayo viongozi na waasisi wa nchi yetu wamepigania kabla na wakati wakuoigania uhuru wetu.

Washauriwe  kurejea kwenye jarida la Kiswahili tulilotayarisha na ambalo limepitiwa na wahariri wa gazeti la Mwananchi na pia mabingwa wa ubora wa Kiswahili katika Kampuni ya Nation Media Group huko Nairobi, Kenya. Jarida hili linapatikana katika Tovuti ya Kiswahili inajulikana kama Kitovu cha Kiswahili (www.Swahili hub.com) na jina la jarida hili ni “Mwongozo kwa Wanahabari.” Huu ni mkusanyiko wa makosa yatokanayo na uandishi kwenye magazeti yakifuatiwa na marekebiisho ya makossa hayo yanayohusu tahajia, miundo, mpangilio na matumizi sahihi ya lugha ya Kiswahili. Pia kuna orodha ya baadhi ya istilahi na misamiati ya kisheria. Ulioandaliwa mahsusi kwa wanahabari wanaopenda kujiendeleza.

Iko sehemu inayoeleza kwa ufasaha kuhusu miiko ya uandishi pamoja na misingi ya kisheria ambayo mwandishi anapaswa kuifahamu na kuizingatia ili kujikinga na matatizo ya kisheria anayokumbana nayo katika kutekeleza wajibu wake.

 Inawezekana waandishi wanapoanza kuandika wanakosa umakini na wanaboronga makala zao hasa kwa upande wa isimu ya lugha na pia fasihi. Wahariri wanaopitia makala za waandishi hao wanatakiwa  wawe na busara ili kuhakikisha kuwa lugha ya Kiswahili iliyotumika ni sanifu kabla ya kuruhusu makala  hizo kuchapishwa kwenye magazeti.

Kwa kuanzia wanaopaswa kuondoa  dosari zinazotokana na makosa ya isimu na fasihi ya lugha ya Kiswahili ni wahadhiri na pia wakuu wa vyuo vinavyowasomesha wanahabari hayo. Yako maswali ya kujiuliza:

Kwanza ni je, wahadhiri wa Kiswahili na wakuu wa vyuo vya uandishi wa habari wanafuatilia kwa makini mihutasari inayotakiwa kutumika kufundisha lugha ya Kiswahili kwa wakurufunzi wao?

Pili, je, wahadhiri hawa wana ujuzi wa kutosha wa fasihi  na isimu ya Kiswahili?

Tatu, je, wahadhiiri hawa wanajiandaa vya kutosha kabla ya kuingia darasani?

Nne, je, wana vifaa vya kufundishia na kujifunzia lugha  kama video, kanda za kunasia sauti, vipaza sauti, maabara za lugha  kwa ajili ya kufundisha fonolojia na hasa kiimbo na matamshi sahihi  na kupiga vita lafudhi isiyo sahihi?

Tano, je, wakurufunzi wanapata muda wa kutosha kufanya mazoezi ndani ya darasa na pia nje ya darasa kwa maana ya kuwepo kwa vituo vya kufanyia mazoezi nje ya vyuo kama vile kampuni za kuchapisha magazeti na pia vituo vya kutangaza habari kama redio na runinga?

Sita, je, miiko ya ufundishaji lugha inazingatiwa, kwa maana ya kutochanganya lugha hasa lugha za kigeni badala ya kutumia lugha ya Kiswahili kuzungumza au kwa kuandika?

Saba, je, wanachuo wanafahamishwa utamaduni wa Waswahili kwa maana ya matumizi ya lugha ya Kiswahili yanayozingatia mila na desturi za Waswahili?

Haya yote yakizingatiwa, kinachofuata ni ufuatiliaji wa wanachuo hawa baada ya kuhitimu mafunzo yao ili  kuona kama kilichofundishwa chuoni kinaendena na hali halisi huko kazini. Ipo haja ya kufuatilia wahitimu hawa baada ya kuhitimu na kuajiriwa, wawe wanapata mafunzo ya mara kwa mara wakiwa kazini baada ya kipindi fulani kwa lengo la kuwapiga msasa na kuwambusha wajibu wao na pia kuwaongezea maarifa na ujuzi pale penye upungufu.

Hivi karibuni nilisoma kwenye mitandao ya kijamii habari kuhusu msanii ajulikanaye kwa jina la Roma Mkatoliki. Mwandishi  huyu aliandika:

a)  Nyimbo iliyo sababisha roma kutekwa ni hii hapa, “Imevuja”.

Ukichunguza sentensi hiyo hapo juu utagundua kuwa  ina makosa kama yafuatayo:

i)                 Neno ‘nyimbo’ ni wingi wa neno ‘wimbo’. Waandishi wengi wanashindwa kutofautisha maneno haya mawili katika umoja na wingi. Kwa mfano:  “Wimbo uliosababisha Roma atekwe ni huu hapa.” Sentensi hii iko katika umoja.

ii)              Jina la mtu huanza kwa herufi kubwa. Kwa hiyo neno roma lilitakiwa lianze kwa herufi kubwa kama ‘Roma’.

iii)           Iliyosababisha ni neno moja. Mwandishi alitenganisha maneno ‘iliyo’ na ‘sababisha.’ Hili ni kosa.

iv)           “… hii hapa!” Neno lililotumika ni …”hii hapa” badala ya “huu hapa”.

 Kwa hiyo sentensi sahihi ni: “Wimbo uliosababisha Roma atekwe huu hapa.”

b)  Sentensi nyingine: “Aliyekuwa akiibia Serikali takriban Sh 7 milioni kwa dakika amepandishwa  mahakamani.” Hapa kuna kosa la kimantiki. Si jambo la kawaida  mtuhumiwa hupanda mahakamani. Kwa kawaida mtuhumiwa anapelekwa mahakamani na  kuhukumiwa. Akiwa mahakamani mtuhumiwa anahojiwa na Hakimu na Mwendesha Mashataka akiwa kizimbani. Kwa hiyo ni makosa kuandika kuwa “…amepandishwa mahakamani” bali “amepandishwa kizimbani” huko  mahakamani.

c)   Angalia sentensi hii: “Kuchelewa kwa demokrasia chanjo cha migogoro mingi Afrika.” Hapa inawezekana mwandishi ameathiriwa na lugha yake ya kwanza. Hivyo badala ya kutumia neno “chanzo” ameandika “chanjo”. Maneno haya yanatofautiana katika maana. Ipo haja ya kujiepusha na athari za lugha nyingine hasa lugha mama. Kwa hiyo isomeke “ chanzo” badala ya “chanjo”

d)  ‘Mvutano huo ulikuja baada ya mke wa marehemu kutaka kupewa haki ya kuzika mwili wa marehemu mumewe.”Hii ni sentensi yenye utata. Kwa usahihi yako baadhi ya maneno yanayoweza kuwakilishwa  kwa kutumia maneno machache.  Kwa mfano  “kuzika mwili wa marehemu mumewe” ingefaa iandikwe “kumzika mumewe”. Vilevile “mvutano ulikuja” ungeweza kuandikwa “mvutano ulijitokeza” au “ulitokea mvutano…”

Mwisho, inashauriwa kutumia maneno rahisi na ya kawaida badala ya kutumia maneno magumu. Kwa mfano”:

-        Mashabiki wa Simba walitoka Uwanja wa Taifa Dar es Salaam roho kwatu baada ya Simba kucheza kwa kiwango bora. Neno kwatu halimo katika kamusi ya Kiswahili Sanifu ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI). Neno hili limepachikwa tu na mwandishi

bila kujali kama litaeleweka au vipi.

Mfano mwingine:

-        Tulishuhudia Zanzibar ikiondoka kwa kupeleka vijeba.

Hapa neno vijeba halieleweki. Kwa nini mwandishi aliamua kulitumia?

-        Wanawake waaswa kujiunga na saccos.

Nini maana ya kuasa?

Kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili ya mwaka 2017 iliyotayariswha na Bakita kwa kushirikina na Kampuni ya Longhorn ya Kenya neno asa lina maana ya kukanya, achisha kufanya jambo, kataza kufanya jambo na kadhalika.

Kwa mfano, “Mwanangu nakuasa uache ulevi.”

Katika muktadha wa maelezo yaliyoandikwa kwenye sentensi hii, kuasa ilikusudiwa kuwa ni kuhimiza au kushawishi. Hivyo kupotosha maana iliyokusudiwa. Ilikusudiwa kuwahimiza wanawake wajiunge na saccos.

Upotoshaji huu unaofanywa na waadishi unapaswa kupigwa vita.