http://www.swahilihub.com/image/view/-/4392590/medRes/1938408/-/j5oqtyz/-/maina.jpg

 

Ufafanuzi kuhusu matumizi mabaya ya lugha ya Kiswahili magazetini

Stephen Maina

Bw Stephen Maina. Picha/MAKTABA 

Na STEPHEN MAINA

Imepakiwa - Friday, June 8  2018 at  15:44

Kwa Muhtasari

 • Licha ya mahanjam yake hapo awali, kwamba angerejea nchini haikufikiriwa hata kidogo
 • Ni wasomaji wachache wanaofahamu maana ya neno “mahanjam”
 • Kwanza neno “mahanjam” asili yake ni Kiarabu
 • Pili, lina maana mbili tofauti. Maana ya kwanza ni kuwa na hamu au shauku kubwa ya kufanya mapenzi kama vile kuwa na nyege, ashiki, na kadhalika
 • Maana ya pili ni kuwa na machachari hasa mtu anapopata hasira
 • Ili kuwapa msamiati unaofahamika na wengi tungetumia neno ‘machachari’ likiwa na maana ya mtu mwenye hamasa kubwa ya kutenda jambo

 

HUU ni mwendelezo wa ufafanuzi kuhusu matumizi mabaya ya lugha ya Kiswahili tunayokumbana nayo kwenye magazeti lengo likiwa ni kuainisha makosa hayo na kuyapatia ufumbuzi. Kwa mfano imeandikwa:

 • “Wewe aliyekuambia anaondoka ni nani?” Katika mazungumzo, muundo huu unakubalika lakini katika maandishi inafaa kuliacha neno ‘wewe’ na ukaanza moja kwa moja na kuandika,”Aliyekuambia anaondoka ni nani?”

 • “Mfumo wa uendeshaji wa klabu za soka nchini huku Simba na Yanga zikiwa ndio walengwa wakubwa.” Neno ‘wakubwa” limetumika mahali pasipohusika. Kwa usahihi nashauri neno ‘wakubwa’ litolewe na kuandikwa ‘wakuu’.   Kwa mfano,”…Simba na Yanga zikiwa ndio walengwa wakuu.”

 • “Washtakiwa 3 zaidi watambuliwa kwa kumshambulia mfanyibiashara”

  Yako makosa mawili katika sentensi hii. Kosa la kwanza ni kuandika tarakimu 3 badala ya kutumia maneno ‘watatu’. Tunatumia tarakimu wakati  tunaandika tarakimu kuanzia kumi na kuendelea. Kwa hiyo 1 hadi 9 huanndikwa kwa maneno lakini kuanzia kumi na kuendelea tunatumia tarakimu. Kosa la pili ni neno ‘mfanyibiashara’. Neno hili linasikika likitumika wakati wa mazugumzo lakini wakati wa kuandika linatakiwa kuadikwa ”mfanyabiashara” Inasikitisha kusoma mfanyibiashara katika ukurasa wa mbele wa gazeti maarufu katika taifa lenye wasomi wengi wa Kiswahili.

 • “Licha ya mahanjam yake hapo awali, kwamba angerejea nchini haikufikiriwa hata kidogo.” Ni wasomaji wachache wanaofahamu maana ya neno “mahanjam”. Kwanza neno “mahanjam” asili yake ni Kiarabu. Pili, lina maana mbili tofauti. Maana ya kwanza ni kuwa na hamu au shauku kubwa ya kufanya mapenzi kama vile kuwa na nyege, ashiki, na kadhalika. Maana ya pili ni kuwa na machachari hasa mtu anapopata hasira. Ili kuwapa msamiati unaofahamika na wengi tungetumia neno ‘machachari’ likiwa na maana ya mtu mwenye hamasa kubwa ya kutenda jambo.
 • Baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo ‘kutenguliwa’ na aliyekuwa Waziri Nape Nnauye, wananchi wengi walifurahia hatua hiyo.  Neno ‘kutenguliwa’ limetokana na neno ‘kutengua’. Kutengua ni kubatilisha, kutupilia mbali maafikiano yaliyofikiwa, nk. Neno linalofaa hapa ni kuengua kwa maana ya kutolewa kazini au kwenye shughuli fulani. Kwa mfano, Mkuu wa Mkoa amemwengua Juma kwenye jopo la watafiti kutokana na ubishi wake.  
 • Anahitaji matibabu zaidi lakini family yake imeshindwa ‘kumgharamia’. Tunapotaka kunyambua neno ni lazima tuanzie na kitenzi na siyo nomino. Kitenzi kinachofahamika ni gharimu na nomino ni gharama. Tunasema imenigharimu Sh10,000 kumtibu mwanangu. Kwa hiyo nimegharimia  Sh10,000 elfu kumtibu mwanangu. Kwa hiyo hatuwezi kupata kitenzi ‘gharamia’ bali ni ‘gharimia’.
 • ·      “ Kufuatia hoja hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Adelardus KIlangi alionekana akiteta na mawaziiri kadhaa ndani ya Bunge.”

 • Matumizi ya neno ‘kufuatia’ yanaleta kichefuchefu kwani linatumika kimakosa na linaonekana katika maandishi rasmi kama kwenye hotuba za mawaziri bungeni, nk. Haya ni makosa na hatuna budi kufanya marekebisho mapema.

 • Kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili iliyotayarishwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), neno ‘kufuatia’ lina maana ya kuambatana kwa kwenda nyuma ya mtu mwingine. Kwa hiyo neno  ahihi hapa ni ‘kutokana na ‘.  Hivyo sentensi isomeke,”Kutokana na hoja hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Adelardus Kilangi alionekana akishauriana na mawaziri kadhaa ndani ya Bunge.”

 • Sentensi nyingine imeandikwa, “Pamoja na angalizo hilo, japokuwa baadhi ya mamlaka huchukua hatua, tunashauri zifuatiliwe kuongezeka kwa wimbi la utapeli katika kutoa elimu kuwabaini wahalifu.”
 • Neno japokuwa limezoeleka sana katika maandishi ya Kiswahili lakini katika ufasaha wa lugha matumizi sahihi ni ijapokuwa. Kwa kuwa linatumika kimakosa inabidi kujizoeza kutumia lililo sahihi ilikuekebisha kosa hili.

 • “Hizo ni zile za kuomba fedha.Lakini zipo nyingine zinazojaribu kucheza na saikolojia ya watu hasa wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali.”
 • Sehemu ya kwanza ya sentensi ya kwanza na ya pili zilitakiwa kuunganishwa kwa maana ya kuondoa alama ya nukta iliyopo na hivyo neno lakini lingekuwa kiunganishi cha mafungu hayo mawili. Vilevile ifahamike kuwa ni makosa kuanza sentensi kwa kutumia neno lakini kwani hutumika kuunganisha mafungu ya maneno na kamwe si kwa kuanza sentensi.

 • Yako mambo yanayotegemewa hasa yale yanayowagusa wadau wa bajeti kwa jumla.”
 • Neno “yanayotegemewa” limetumika vibaya.  Bada ya kutegemea ingefaa kuandika yanayotarajiwa” maana ya kutegemea ni kuegemea, kushikilia, nk. Kwa mfano tunasema,’Mtoto anamtegemea mzazi au mlezi wake kwa ajili ya matumizi muhimu,” au Zanzibar wanategemea karafuu kama zao muhimu la uchumi.”

 • Kutazamia au kutarajiwa ni maneno yanayofaa kutumika badala ya kutegemea.

 • “Japkouwa inaweza kuwa sio kubwa sana bado ni eneo zuri la mjadala wa kinapia.”

 • “Ni majira ya jioni shule imeanza na baadhi ya wanafunzi wameanza kurudi nyumbani.” Neno lisilofaa hapa ni ‘majiira’. Maana ya majira ni kipindi fulani cha mwaka. Kuna majira ya mvua, kipupwe,kiangazi, na kadhalika. Neno sahihi hapa badala ya majira ni kipindi, wakati, saa, na kadhalika.

 • “Nilmwambia wewe hauna simu” sahihi ni kuandika neno ‘huna badala ya hauna’.
 • Kwa mfano, "Nilimwambia wewe huna simu.”