Kiswahili kina uwezo wa kuinuliwa hadi kijisimamie chenyewe

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Sunday, April 23   2017 at  19:19

Kwa Mukhtasari

KINAPOLINGANISHWA na lugha nyinginezo za Kiafrika, bado Kiswahili kina bahati ya kuwa na waandishi wengi Waswahili walioandika fasihi ya Kiswahili kwa kutumia Kiswahili – Said Ahmed Mohammed, Mohamed Said Abdullah, Shaaban Robert, Ken Walibora, na orodha inaendelea. 

 

Wengi wa waandishi hawa wameandika kazi zao zote takribani kwa lugha ya Kiswahili pekee na zikajizolea sifa kubwa ulimwenguni kote, nyingine zikitafsiriwa kwa lugha za kigeni, kama ilivyo riwaya ya Kuli ya Shafi Adam Shafi.

Hata mwandishi Boubacar Diop ilimchukuwa muda kuamini kuwa anaweza kutoka nje ya lugha ya Kifaransa anayotumia kuandikia kazi zake na kugeukia lugha yake ya kuzaliwa nayo. 

“Nilipoanza kuandika, kamwe sikuwahi kufikiria kuwa kuna siku nitaweza kuandika riwaya kwa Kiwolof, kwa sababu nilikuwa siwezi. Siwezi tu. Ingawa nilifikiria kuwa ni jambo zuri kufanya, lakini mimi nisingeliweza. Kisha nikaamua kujaribu na nikaweza.”

Hivyo, tunaporejea lile swali la ikiwa kuna haja ya ‘kuiafrikanisha’ fasihi ya Kiafrika, pamoja na yote, jibu hadi sasa ni kwamba haja hiyo ipo, maana Waafrika wana utamaduni na hivyo fasihi yao ambayo ni tafauti kabisa na wengine, baadhi ya wakati haiwezi hata kusimulika kwa kutumia lugha isiyokuwa yao, maana fasihi ni pamoja na kuzielezea hisia za ndani mno za kibinaadamu.

Manu Chandaria, mwanzilishi na mwenyekiti wa makampuni ya Safal, ambayo kupitia kampuni yake tanzu ya Mabati Rowlings inashirikiana na Chuo Kikuu cha Cornell cha Marekani kutoa tuzo kwa waandishi wa Fasihi ya Kiswahili, anaamini kuwa Kiswahili kinaweza kuinuliwa na kujisimamia chenyewe.

“Tunataka kukisambaza Kiswahili. Ndilo jambo ambalo tunapaswa kulifikiria. Ndiyo lugha yetu ya kuelezea hisia zetu. Hatuwezi kuzielezea kwa namna nyengine. Unaweza kujaribu lugha zote, lakini hutaweza. Na kuumiliki utamaduni na fasihi yetu, lazima tuijuwe lugha hii.”

Na, kwa hakika, njia ziko nyingi ambazo lugha za Kiafrika zinaweza kutumiwa na Waafrika kusimulia fasihi yao wenyewe. Mojawapo ni tafsiri baina ya lugha moja ya Kiafrika kwenda nyingine na pia kwa waandishi wenyewe waliozowea kuandika kwa lugha za kigeni kuandika kwanza kazi hiyo hiyo kwa lugha ya Kiafrika.

Na kwa wale ambao bado wanaamini kuwa kuandika kazi za fasihi ya Kiafrika kwa lugha ya kigeni ndiko kunakowafanya wawe wa kimataifa na wasomi zaidi, mwandishi gwiji wa fasihi kutoka Senegal, Boubacar Diop, anawataka afikirie upya.

“Watu wanadhani ni rahisi kusahau asili yangu. Nakwenda tu moja kwa moja tu kuwa mtu wa ulimwengu na inakuwa hivyo. Nadhani ni sisi peke yetu tunaofikiria hivyo. Tuwe wakweli, tuna tatizo la kukosa kujiamini wenyewe.”

Kutokana na matumizi yake mapana ya kuweza kuwafikia mamilioni ya watu, Kiswahili kinatumika sana katika teknolojia za violezi, hasa kanda za muziki, video, redio, filamu za sinema, vipindi vya televisheni vya burudani na vya kielimu.

Matumizi haya yamesaidia kueneza Kiswahili duniani kote. Mathalani waimbaji mashuhuri kama Harry Belafonte na Miriam Makeba wamewahi kuimba baadhi ya nyimbo zao kwa Kiswahili na hivyo kueneza maneno ya Kiswahili kwa mamilioni ya watu nje ya Afrika.

Aidha, filamu nyingi za Kimarekani zenye kuhitaji lugha ya Kiafrika aghalabu hutumia Kiswahili (mfano The Lion King). Kiswahili pia kinatumika vilivyo katika tovuti kwa kupeana, kupeleka na kutafutia taarifa. Tovuti za Kiswahili zimezagaa duniani kote, nyingi zikiwa Marekeni na Ulaya, lakini hata Afrika zimeanza kusimikwa.

Kuna tovuti zenye kozi za kufundisha Kiswahili, kwa kusoma na kusikia kupitia kompyuta na zipo zenye kamusi za Kiswahili, makala au maelezo ya kitaaluma kuhusu Kiswahili.

Zipo injini za upekuzi (search engines) zenye kutumia Kiswahili (mfano Google). Juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanywa katika kukienzi Kiswahili katika nyanja za sayansi na teknolojia.

Miongoni mwa juhudi hizo ni kutekelezwa kwa Mradi wa Swahili Language Manager (SALAMA) kwa ushirikiano wa Taasisi za Taaluma za Kiswahili (TATAKI) na Chuo Kikuu cha Helsinki unaokusanya maneno na matini ya lugha ya Kiswahili ili kuunda kopora (kusanyo la data za lugha), na kisha kuyachanganyua kiisimu, kuyapatia tafsiri ya Kiingereza, na kuyahifadhi katika kanzi kwa ajili ya watumiaji.

Mradi wa DISROMA (CD –ROM) unaingiza baadhi ya machapisho na data muhimu za utafiti yakiwemo kamusi, rekodi za sauti, fasihi simulizi n.k. katika disketi za muundo wa ROMA zenye kuhifadhi taarifa nyingi na ziwezazo kusomwa na kompyuta.

Tayari kamusi mbili (Kiingereza-Kiswahili na Kiswahili-Kiingereza) zinapatikana katika disroma. Juhudi nyingine ni kutekelezwa kwa Mradi wa Kisahihishi/ kikagua-tahajia (spell-checker) cha lugha ya Kiswahili.

Utandawazi kama sehemu mojawapo ya maendeleo hayo umebadili mwelekeo wa jamii nyingi duniani. Mawazo ya watu wachache, utamaduni wao, mila na desturi zao, namna zao za kuishi kila siku, zimechukuliwa kuwa ndio mawazo na namna ya kuishi kwa watu wengi.

Kwa upande wa fasihi katika utamaduni unaobadilika, maendeleo ya sayansi na teknolojia yanatoa changamoto ili tuangalie upya dhana ya fasihi simulizi.

Hali ya mawasilinao ilivyo wakati huu wa utandawazi ni kichocheo cha mahitaji ya kuangaliwa upya kwa maana ya fasihi simulizi. Kucha za utandawazi zinatumika katika kukififisha Kiswahili ambacho kimeonekana kuwa tishio dhidi ya lugha za mataifa makubwa.

Wakati umefika sasa kuwa makini na mfumo huu mpya wa utandawazi ambao ni aina fulani ya kampeni ya kiutawala katika karne hii ya sayansi na teknolojia.

Utandawazi ni mbinu mbadala ya ukoloni mkongwe na ukoloni mamboleo. Utandawazi unaletwa kwetu kwa lugha laini na yenye matumaini mema.

Lakini kwa upande wa pili, nyuma ya pazia la utandawazi kuna kila dalili ya kukosa fursa ya kufaidi matunda ya utandawazi na hasa ikiwa tutakuwa wapokeaji tu wa matunda badala ya kuwa wachangiaji.