Kiswahili ni asili

Na  Rahma Mahmoud

Imepakiwa - Monday, November 12  2018 at  10:29

 


Lugha iliyonawiri, leo inadidimia,

Potofu zilizojiri, lugha kutuharibia,

Ilizidi kushamiri, zama ilipotokea,

Kiswahili ni asili, acha kutuharibia.

 

Chanzo kilipoanzia, ubovu kupindukia,

Miandao asilia, wengi tumetumia,

Lugha wanajifungia, kisha inaendelea,

Kiswahili ni asili, acha kutuharibia.

 

Kama kawa naileta, wapi ilipoanzia,

Kamusi sijaikuta, kila nilipopitia,

Acheni wenu utata, lugha kutuchafulia,

Kiswahili ni asili, acha kutuharibia.

 

Bamaji hatamwagika, nabaki kuangalia,

Mnazidi kupinduka, asili mnakimbia,

Isije ikatoweka, kibou kikaenea,

Kiswahili ni asili, acha kukiharibia,

 

Wendi wanakitamani, nyinyi mnakifukia,

Lugha hii ya thamani, wengine hamjajua,

Basata mpo makini, mzidi kutuenzia,

Kiswahili ni asili, acha kutuharibia.

 

Nizidi kujifunza, Kiswahili kutumia,

Nisije nikajiponza, lugha kujiharibia,

Wazee waliitunza, njema wakatuachia,

Kiswahilini asili, acha kutuharibia.

 

Wapo wapi Waswahili, malenga naulizia,

Naomba mjadili, msije kupuuzia,

Utakuwa mlijadili, suala mkaliachia,

Kiswahili asili, acha kutuharibia.