Kiswahili sanifu na kaida za ushairi wa kimapokeo

Na CHRIS ADUNGO

Imepakiwa - Tuesday, April 18  2017 at  14:17

Kwa Mukhtasari

KATIKA utunzi wa ushairi wa kimapokeo unaofuata kaida za arudhi, mambo yanakuwa magumu zaidi kwa uteuzi wa vipashio vya maneno, maana kunaingia haja ya vipimo vya maneno kwa mujibu wa mizani. 

 

Vipimo hivi vya maneno, kwa upande mmoja, vinahitaji urefusho maumbo au maumbile ya maneno fulani (kama kauli fupi lisilotendeka inaweza kurefushwa kwa lahaja ya Kipemba kuwa lisijalotendeka).

Kwa upande mwingine, vinahitaji mbano wa maumbo na maumbile ya maneno husika (kama kauli ndefu alikuwa mzuri inaweza kufupishwa kwa misingi ya lahaja ya Kipemba iwe kauli ali mzuri).

Pia kuna vipimo vya urari wa sauti na vina, uvokali na ukonsonanzi.

Kwa mfano, iwapo mshairi anahitajia urari wa kina cha -po kutokana na kauli yenye mwelekeo wa Kiswahili Sanifu sisahau kamwe ambapo hakuna kina hicho -po, katika lahaja ya Kipemba tungeliweza kukipata kwa kugeuza umbile la neno sisahau kuwa sisahaupo na kupata kina cha -po tunachokihitajia.

Au mshairi angehitaji upachapacha wa uvokali unaopatikana kwa kuweka kwa ukaribu mfwatilizo wa vokali kama katika shairi la Aambaye la diwani ya Jicho la Ndani (84) ambamo neno nyamaa lenye uvokali mwishoni linatokana na lahaja ya Kipemba:

Aambaye aamba, aamba likazagaa,
Aambaye aamba, aamba lenye kufaa,
Aambaye aamba, aamba mawi balaa,
Aambaye aamba, pasi na jema nyamaa.

Katika diwani hii, kwa makusudi mwandishi anaamua kutoka nje ya mstari wa matumizi ya Kiswahili Sanifu kwa sababu, akijua asijue, hatimaye anahisi uhuru wake wa uteuzi umefumbika.

Kutokana na kuchota kutokana na lahaja ya Kipemba anajisalimisha na pingamizi nyingi sana za kujenga mizani kaidi, urari mkorofi na ujengaji wa kimuziki unaozuka kwa kujali mbinu ya uvokali na ukosonanti.

Diwani hii imeingiza lahaja ya Kipemba kwenye mashairi mengi ili kuweza kufaulu katika utekelezaji wa mbinu hizi za arudhi katika ushairi wa Kiswahili.

Tutatoa mfano mmoja ambao umesheheni, uvokali, ukonsonanti, urefusho na mkabo wa mizani, vina na usambamba – mbinu zote hizi zinatokana na shairi moja Akianza, Umalize. Ubeti mmoja tu wa shairi hili unatosheleza mbinu zote hizo:

Akutenzaye mtenze, ajuwe kutenzwa nini
Akuchezaye mcheze, muingize mchezoni
Mpuuzi mpuuze, hana haja ya thamni
Sivyo ‘takuja mwilini, akwanzaye mmalize

Kwa maneno mengine, mshairi anayeogelea kwenye Kiswahili Sanifu na lahaja nyengine anapata uhuru na wepesi mkubwa zaidi wa uteuzi wa maneno, mpangilio wa maneno na sauti kuliko yule ambaye anajikita kwenye Kiswahili Sanifu tu.

Katika hoja hii, tunaona kuwa mtunzi kaelemea sana kwenye lahaja ya Kipemba, lahaja iliyomlea na kumkuza na ambayo inampa uhuru tuliouzungumza hapo juu.

Katika kutia mkono ndani ya lahaja hii, tunaona anavyocheza na maneno ya kila siku lakini yenye sura tafauti, yenye msikiko adimu na yenye ladha ya kimuziki.

Hii lakini si kusema kwamba mshairi huyu anatoka nje ya Kiswahili Sanifu kwa ukamilifu – hasha.

Washairi wengi wakiemo Ahmad Nassir Juma Bhalo na Abdilatif Abdalla, wana mtindo wa kuchanganyisha Kiswahili Sanifu na lahaja.

Lahaja inapohitajika na Kiswahili Sanifu kinapohitajika, Kiswahili Sanifu kinafanya usanii kuchapukia sana kiladha.